KUNA dakika 180 muhimu leo kwa mashabiki wa Simba na Watanzania kwa jumla na za kwanza zitakuwa Uwanja wa Benjamin Mkapa Simba atakapokuwa mwenyeji wa Petro Atletico ya Angola, huku zingine zitakuwa pale DR Congo wakati Azam FC itakapokuwa mgeni wa Union Maniema.
Bahati mbaya sana mechi hizo mbili zote zitaanza muda mmoja saa 10:00 jioni, huku Simba itakuwa ni mechi ya kwanza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Azam ikiwa ni Kombe la Shirikisho hatua kama hiyo.
Tuanze na Simba, ambayo inataka kutunza malengo yao inafahamu itakutana na mpinzani mgumu yenye rekodi kubwa kwenye mashindano haya na ilifika hatua ya nusu fainali msimu wa 2021-22.
Simba ambayo ilicheza Fainali ya Kombe la Shirikisho msimu uliopita, inataka kufika mbali kwenye ligi ya mabingwa na kihunzi chao cha kwanza kitaanza mbele ya Petro ambayo ni moja kati ya timu ngumu Afrika.
Mchezo huo unatarajiwa kuwa na vita ya katikati ya uwanja kutokana na timu zote kuwa bora eneo hilo hali ambayo itatengeneza presha kubwa kwa viungo na vikosi vyote viwili.
Kocha Dimitar Pantev tangu atue Simba moja ya mabadiliko yake aliyoyafanya sasa ni kuifanya Simba kuwa imara katikati ya uwanja akiweka viungo wenye akili ya kuzuia na wale wanaojua kufanya mashambulizi.
Ubora huo huo wanao pia Petro ambao wana viungo wenye ubunifu mkubwa na mawinga wenye mbinu na kasi wanaojua kutengeneza krosi nyingi kwenda lango la wapinzani.
Rekodi ambayo itamlazimisha Pantev kukuna kichwa kuhakikisha Simba inashinda ni ile ya kutoshinda nyumbani tangu atue klabuni hapo na ameshaiongoza timu yake kwenye mechi mbili bila kupata ushindi katika mashindano haya.
Kwenye mechi tano za mwisho za Afrika Simba ikiwa nyumbani imeshinda mbili dhidi ya Stellebosch (1-0) na ile dhidi ya Al Masry (3-0) huku zingine tatu dhidi ya RS Berkane, Gaborone United na Nsingizini Hotspurs zikiisha kwa sare.
Petro nao hawana rekodi nzuri sana ugenini na kwenye mechi zake tano za mwisho Afrika imeshinda mbili dhidi ya Stade d’Abidjan (0-2),Cercle DE Joachim (0-3) huku akipoteza dhidi ya Union Maniema (2-1) na kutoa sare mbili dhidi ya TP Mazembe na Al Hilal.
Simba imekuwa kwenye maandalizi makali dhidi ya Petro na taraifa mbaya kwao ni watamkosa kipa wao namba moja Moussa Camara ambaye ataufuatilia mchezo huo kwa mtandao akiwa Morocco, baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti akitarajiwa kuwa nje kwa miezi miwili.
Simba golini itaongozwa na kipa Yakoub Seleman huku kikosi chao kitawategemea mastaa wengine Jonathan Sowah, Morrice Abraham, Ellie Mpanzu na Kibu Denis mwenye mabao mawili hadi sasa kwenye mashindano hayo.
Petro walitua nchini juzi usiku kwa hesabu kali wakitarajiwa kutua leo huku kwa muda waliotangaza watakuwa hapa, itakuwa ngumu kwao kuwahi kufanya mazoezi kwenye uwanja wa mchezo.
Mchezo huop utaamuliwa na mwamuzi kutoka Cameroon Abdou Abdel Mafire ambaye anasifika kwa kujua kugawa kadi nyingi za njano kuliko zile nyekundu.
Azam wao watakuwa ugenini, watakapocheza mchezo wa kihistoria wa kwanza wa hatua ya makundi tangu klabu hiyo ianzishwe itakapokuwa mgeni wa Union Maniema.
Azam jeuri yao kubwa kwenye mchezo huo ina watu watatu ambao wanawajua wenyeji wao kuanzia kocha wao Florent Ibenge, msaidizi wake Anicet Kiazayidi na mshambuliaji wake Japhet Kitambala ambaye alikuwa mshambuliaji wa timu hiyo na hawa wote ni Wakongomani.
Maniema licha ya uzoefu wao mzuri kushinda Azam lakini hawana rekodi bora sana ikiwa nyumbani na kwenye mechi tano za nyuma ikiwa mashindano ya Afrika imeshinda moja pekee dhdi ya Pamplempusses ya Mauritius (2-1), ikipoteza moja (1-2) dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini lakini ikitoa sare tatu dhidi ya Royal Leopards, AS FAR Rabat na Raja Athletic.
Azam nao kwenye mechi zake tano za mwisho Afrika ikiwa ugenini imeshinda tatu na kupoteza mbili na timu zote zitakuwa na vita katikati ya uwanja kila moja ikionyesha kuwa na viungo bora.
Habari njema kwa Azam ni fundi wake tegemeo kiungo Feisal Salum ambaye alipata majeraha ya nyonga, afya yake imeimarika akitarajiwa kuwa sehemu ya kikosi cha matajiri hao mbele ya Maniema ambayo inamilikiwa na bosi wa zamani wa Ibenge Jenerali Amis Koumba, aliyewahi kuiongoza AS Vita.
Akizungumzia mchezo huo, kiungo wa Simba, Mutale alisema jana watajitoa vilivyo kuhakikisha alama tatu zinabaki Tanzania.
“Sisi kama wachezaji tuko tayari kwa hii changamoto. Tutajitoa kwa niaba ya kila aliyepo nyuma yetu, hasa mashabiki ambao wamekuwa nasi katika kila hatua,” alisema Mutale.
Kocha wa kikosi hicho, Seleman Matola alisema: “Malengo yetu msimu huu ni kufika nusu fainali. Naamini silaha yetu muhimu ni kutumia vyema mechi za nyumbani na hiyo ndiyo njia pekee na bora itakayotubeba kufanikisha hilo.”
Nyota wa Petro, Hugo Marques alisema jana kwamba licha ya kuziona mechi kadhaa za Simba, lakini ni ngumu kuzifanyia tathmini kwa sababu hatua hii ni ngumu na tofauti.
“Nawajua baadhi ya wachezaji wa Simba akiwemo Neo Maema kwa sababu nimecheza naye kule Afrika Kusini, ila kwa niaba ya wenzangu sisi tumekuja Tanzania kushindana,” alisema Hugo huku kocha wake, Mhispania Franc Artiga akisema licha ya kucheza na Simba kwa mara ya kwanza, lakini haihofii timu hiyo.
“Tutawakosa wachezaji, Pedro Aparicio, Macaiabo na Matheus Costa, ni pigo kwetu kwa sababu unapokuwa katika hatua hii unahitaji kuona nyota wote wakiwa katika hali nzuri ya kiakili na kimwili,” alisema Artiga.