Nyama Choma Festival ilivyofana Butiama

Butiama. Mamia ya Wakazi wa Wilaya ya Butiama mkoani Mara wamejitokeza katika mashindano uchomaji nyama yaliyozinduliwa kwa mara ya kwanza wilayani huyo.

Mashindano hayo yaliyoandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi yalizinduliwa jana Juni 6, 2024 katika mnada wa Kiabakari kwa lengo la kuwainua kiuchumi wachoma nyama wadogo mkoani humo.

Katika mashindano hayo mbali na ushindani, pia watu waliohudhuria walipata fursa ya kuonja nyama kutoka kwa wachomaji mbalimbali walioshiriki.

Wananchi hao walipata fursa ya kuonja nyama za ng’ombe, mbuzi, kondoo na kuku na kila mchomaji alijitahidi kutumia mbinu anazozijua kuhakikisha nyama yake inakuwa tamu na kuvutia wateja wengi.

Mashindano hayo ambayo yameelezwa yatakuwa ni endelevu, kwa mara ya kwanza yaliwashirikisha washiriki 45 na mshindi wa kwanza lilikuwa banda la JKT Rwamkoma, likijishindia zawadi ya Sh500,000 na mshindi wa pili John Deus aliyejipatia Sh300,000, wa tatu Rama Hoteli akiambulia Sh150,000.

Baadhi ya vigezo vilivyotumiwa na majaji kuamua mshindi kwenye mashindano hayo ni pamoja na ladha ya nyama na ulaini wake pamoja na usafi wa mazingira yanayomzunguka mchoma nyama.

Vigezo vingine ni pamoja na unadhifu wa mchoma nyama, hali ya usafi wa vyombo pamoja na upatikanaji wa maji tiririka kwa ajili ya wateja kunawa na usalama wa nyama husika.

Hata hivyo, baadhi ya watu waliohudhuria kwenye mashindano hayo pamoja na kusema kuwa yamefana, wameomba maandalizi yajayo yaanze mapema, tofauti na haya ya sasa.

“Haya mashindano tumepata taarifa wiki moja iliyopita, ni wazo zuri sana kwa hiyo tunaomba wakati mwingine tupate taarifa mapema ili tuweze kujiandaa vizuri. Naamini hata zawadi zitakuwa kubwa zaidi ya hapa, ila huu ni mwanzo mzuri sana,” amesema Daniel Nyabange, mkazi wa Butiama.

Naye Petro Igenga amesema, “umeona namna watu walivyojitokeza kwa wingi kuja kushuhudia haya mashindano, hii ni dalili kuwa wengi wamelipokea suala hilo kwa mwitikio mkubwa, hivyo maandalizi yakianza mapema naamini watu wengi zaidi watajitokeza, yaani washiriki pamoja na walaji wa nyama,” alisema.

Mashindano hayo yaliyoanza saa 4 asubuhi hadi saa 12 jioni, yalikwenda sambamba na ulaji wa nyama choma ikisindikizwa na vinywaji mbalimbali—  laini na vyenye kilevi, huku wateja wakipata fursa ya kujinunulia bidhaa mbalimbali mnadani hapo.

Baadhi ya wachoma nyama hao   waliiomba Serikali kuwawezesha mitaji ili waweze kuboresha shughuli zao na hatimaye kuboresha vipato vyao.

Pia waliiomba Serikali kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya wachoma nyama wadogo, ili waweze kufanya shughuli zao kila siku, badala ya kusubiri siku za minada.

“Tunaomba tupate mikopo itakayotuwezesha kufanya shughuli zetu na hatimaye kuwa wachoma nyama wakubwa. Uwezo huo tunao kinachotukwamisha ni mitaji na maeneo maalumu,” amesema Kihengu Maro.

Maro amesema kutokana na kutokuwa na mitaji wanalazimika kununua nyama buchani kwa ajili ya kuchoma na kuwa endapo watawezeshwa mitaji, watakuwa na uwezo wa kununua ng’ombe, mbuzi au kondoo na kuchinja wenyewe, hivyo kuwa na uhakika wa kupata faida zaidi.

“Ukichinja ng’ombe unapata faida zaidi kuliko kupima buchani na kwa sasa bei ya ng’ombe mkubwa ni kati ya Sh700, 000 na 800,000, gharama ambayo ni kubwa na huuwezi kuimudu kama huna mtaji,” aliongeza.

Kwa upande wake Ramadhan Mkune, amesema ili waweze kukopesheka pia wanahitaji kuwa na maeneo maalumu kwa ajili ya kufanya shughuli zao, tofauti na sasa mbapo wengi wao wanasubiria siku za mnada pekee.

“Wengi wetu tunachoma nyama minadani na kama unavyojua mnada unakuwepo mara moja kwa mwezi na minada nayo si mingi, kwa hiyo tukitengewa maeneo maalumu tutafanya shughuli zetu kila siku, tena kisasa, na kuweza kukopesheka kwa urahisi,” amesema Mkune.

Akizindua mashindano hayo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Moses Kaegele amesema lengo la Serikali mkoani humo ni kutaka kuwawezesha kiuchumi wachoma nyama wadogo mkoani humo.

“Tunataka kuibua fursa za kiuchumi kupitia mifugo na mazao yake kama maziwa, nyama na ngozi, lakini kubwa zaidi ni kuwainua kiuchumi wachoma nyama wadogo waliopo ndani ya mkoa wetu,” amesema.

Kuhusu mitaji, Kaegele amesema upo uwezekano wa Serikali kuanza kutoa mikopo kwa makundi ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kupitia halmashauri, hivyo kuwataka wachoma nyama kujiandaa kutumia fursa hiyo ya mikopo.