Hatari kwa watoto wenza kuishi mbalimbali

Canada. Ni jambo la kawaida kusikia au kushuhudia wanandoa wanaoishi maisha ya utengano usio na ulazima. Mara nyingi hutenganishwa na majukumu ya kazi au shughuli nyingine za kujenga maisha.

Wapo pia wanaoishi mbali kwa sababu za mila na tamaduni. Kwa mfano, katika baadhi ya jamii bado kuna imani kwamba familia inapaswa kuwa na mashamba au mifugo maeneo ya vijijini walikozaliwa, na mara nyingi kinamama ndiyo hupelekwa kuangalia mali hizo.

Huwa unasikia mtu akisema, “Mke wangu yuko kijijini kuangalia ng’ombe na mashamba.” Lakini ndoa haikufungwa ili mmoja awe mtunza mali na mwingine aishi mjini. Ilifungwa ili wawili hawa waishi karibu, wakishirikiana katika kila hatua ya maisha.

Ingawa hali ya maisha inaweza kuwalazimisha wanandoa kuishi mbali, swali la kujiuliza ni kama hiyo ndiyo njia pekee ya kufanikisha malengo yao bila kujitesa, wala kuwatesa watoto.

Je, wanaochagua au kulazimika kuishi mbali wanatambua madhara ya mpangilio huo? Hakuna njia mbadala inayoweza kuwaweka pamoja huku wakijenga uchumi wao?

Inafahamika kwamba kipato ni msingi muhimu wa ustawi wa familia. Hata hivyo, si busara kuruhusu jitihada za kiuchumi zitawale kila jambo hadi kuhatarisha misingi ya ndoa.

Kwa yeyote anayejua ladha na changamoto za maisha ya ndoa, utengano wa muda mrefu unaweza kuwa chimbuko la kuyumba kwa uhusiano na wakati mwingine kuvunjika kabisa.

Mbali na hilo, kuishi mbali huleta hali ya upweke kwa wanandoa na kwa watoto, jambo linalozua changamoto katika malezi. Baadhi ya makabila nchini Kenya, hususan Wakikuyu na wengineo mbali na yale ya Pwani, wana utamaduni wa kwenda mijini kutafuta riziki huku wakiwaacha wake zao kulea watoto peke yao vijijini.

Athari yake ni kwamba watoto hukua wakiwa karibu zaidi na mama, na kumtazama baba kama mgeni ingawa ndiye anayehangaikia maendeleo yao kutoka mbali.

Pindi watoto wanapokua, mara nyingi wazazi hao hujikuta wakitegemea msaada kutoka kwao, lakini watoto hao wamekosa muunganiko wa kihisia na hawako tayari kutoa msaada uliotarajiwa.

Ukweli ni kwamba sisi sote tunawapenda watoto wetu. Hata hivyo, upendo huo unaweza kugeuka mzigo pale tunapowakosea maandalizi ya kisaikolojia na kiuzoefu kwa maisha ya baadaye, hasa tunapowazoesha kutegemea kila kitu bila kujishughulisha.

Wazazi wengi huhangaika kuwaachia watoto mali nyingi, lakini mali hiyo huishia kufujika kwa sababu watoto hawakuandaliwa kuikabili dunia.

Urithi mkubwa si fedha, si mashamba, si majumba; ni kuwaandaa watoto kifikra, kimaadili, na kisaikolojia ili waweze kusimama wenyewe maishani.

Wazazi wengi ambao leo ni watu wazima hawakurithi chochote zaidi ya kulelewa na kuandaliwa kwa nidhamu na bidii na hayo ndiyo yaliyowafanikisha.

Hata hivyo, wazazi wengine, baada ya kupitia magumu wakiwa wadogo, hutumia mafanikio yao kuwakinga watoto kupita kiasi wakiamini kuwapa maisha laini ndiyo njia bora.

 Lakini kufanya hivyo mara nyingi kunawafanya watoto wakose uhalisia wa maisha. Wengine huwasomesha watoto katika mazingira ya kifahari kwa sababu wao hawakupata nafasi hiyo, bila kutafakari kama mazingira hayo yanawajenga au yanawapoteza.

Matokeo yake, mtoto anapomaliza shule, wazazi wanagundua wamemwandaa katika njia isiyoendana na hali halisi ya maisha, wakianza kumwona kuwa mzembe bila kutambua chanzo cha tatizo. Masuala haya ya malezi ya kisasa yanahitaji mjadala mpana zaidi.

Zaidi ya changamoto za malezi, kuishi mbalimbali kunafungua milango ya vishawishi katika uaminifu wa ndoa. Tendo la ndoa ni sehemu muhimu katika uhusiano, na wanandoa wanapokosa ukaribu wa kimwili kwa muda mrefu, changamoto hii huwa halisi. Ingawa si haki kuwahukumu wanaoanguka katika vishawishi, ukweli unabaki kwamba mazingira ya kutengana kwa muda mrefu yanaongeza hatari hiyo. Wako wanaodumu kuwa waaminifu licha ya umbali, na wako wanaoishi pamoja lakini bado wanasaliti. Hili linabaki kuwa changamoto kwa kila wanandoa kutafakari na kujiuliza namna ya kulilinda penzi lao.

Kwa ujumla, kuishi mbali kama wanandoa kuna madhara makubwa kwa wao wenyewe na kwa watoto wao. Ni muhimu kutanguliza uhusiano, umoja wa kifamilia, na malezi bora badala ya kuendeshwa na hofu ya kesho ya watoto.

Kama wazazi waliweza kupitia ugumu na wakasimama, basi hata watoto wao wataweza wakipewa maandalizi sahihi.