Hasira na chimbuko lake kwenye ndoa

Dar es Salaam. Hasira ni hisia nzito zinazoambatana na maumivu ya moyo.

Ingawa ni mojawapo ya hisia tulizo pewa zawadi na Mwenyezi Mungu, kila mtu anapokuwa na hasira mara nyingi matokeo yake huwa sio mazuri.  Takwimu zinaonyesha kuwa hasira ni sababu ya pili kwa ukubwa inayosababisha ajali nyingi katika nchi zilizoendelea hususani Marekani.  Hasira imewapa majeraha, vidonda, michubuko na maumivu watu wengi hususani watoto walioumizwa na wazazi wao, wake walioumizwa na waume zao, wafanyakazi walioumizwa na mabosi wao, mifano ni mingi.

Hasira pia imekuwa chanzo cha kuvunjika kwa ndoa na familia nyingi, hasa pale ambapo wanandoa wote au mwanandoa mmoja anaposhindwa kuzitumia hasira hizo vema.

Wakati wowote hasira au hali ya kutofautiana inapojipenyeza katika mjadala au mazungumzo yoyote, hufanya hali kuwa ngumu katika kufikia suluhisho.

kama ningekuuliza, hasira ni nini, ungenijibu nini?  Je, una maelezo sahihi ya kuelezea hasira au unajua tu kuipata na kuitumia? 

Ingawa tumeona awali  kuwa hasira ni hisia nzito na zenye maumivu ya ndani, lakini ni vema kujua kuwa zinaweza kuambatana na hisia nyingine mbaya kama vile machungu, visasi, ukali, vinyongo.  Hapa ndipo pale mtu anapoweza kulipuka kama bomu, kisa tu alikuwa ameficha hasira tele moyoni.

Hasira inaweza kumpeleka mtu kufanya uharibifu, kuvunja au kulipiza kisasi. Hasira huzalisha vita, chuki na maumivu ya moyo pia.  Hasira huzalisha vita baridi, huzalisha kususiana, hisia kama hizi zaweza kukujia hasa pale unapohisi kudharauliwa, kutukanwa, kudhalilishwa au kukosewa heshima.

Aina hii ya hasira hujitokeza pia katika uhusiano hata wa ndoa na hali huwa ngumu sana.

Hatari ya hasira hasa katika uhusiano hujionyesha pia katika jitihada za wapendanao hao kujaribu kuishughulikia au kuipooza hasira hiyo. Mfano wako wanaojifanyisha kama vile hawajakasirika, wanajaribu kuiweza au kuizika hasira yao, lakini kile wanachokizika bado ni hai na kwa kitambo kidogo kitawalipukia na kuwaharibu kupitia magonjwa kama vidonda vya tumbo, magonjwa ya kupooza, mshutuko wa moyo, shinikizo la damu.

Hasira inayozikwa, kwa kawaida inabaki ikiwa hai katika nafsi. Wengine wanajaribu kushughulika nayo kwa kujiachia, kuji “express” wanavyotaka na wanavyojihisi.

Wanafikiri kuwa hii itawasaidia zaidi, lakini tabia hii inakutenga na marafiki zako, wapendwa wako na hata ndugu zako, kila mmoja anakaa mbali  na wewe kwa jinsi wanavyokujua unavyokuwa ukikasirika.

Wengi wetu hujisikia vibaya sana mara baada ya kuzicheuwa hasira zetu, mara baada ya kujiachilia unabaki ukijihisi aibu moyoni, unajihisi kukosa furaha, wengine huirudisha hasira juu yao wenyewe na kuanza kujichukia, kujidharau na kujiona wasiofaa na wasio na kitu kabisa.

Hasira huwa tatizo kubwa hasa inapochukua mikondo miwili ifuatayo,   Mkondo wa kwanza ni pale mtu anapoionyesha hasira kwa kupitiliza na mkondo wa pili ni pale mtu anapoimeza, kuifukia, au kuificha hasira yake.

Mara nyingine mkondo huu  wa pili hufanywa pasipo hata anayefanya kujua anafanya nini na kwa athari gani, na kwa hivyo wengine hujikuta wanajiumiza na kutojitendea haki.

Tunapokasirika kupitiliza hasira zetu zinahama mikononi mwetu, zinaanza kutuendesha sisi, sio sisi kuziendesha hasira hizo. Hapa fujo hujitokeza, majeraha na maumivu pia hudhihirika..

Yawezekana umeijua na kuizungumzia hasira kwa muda mrefu, lakini hujajua ukweli unaohusu hasira na yumkini ukweli huu ukawa tofauti na kile ulichokifahamu kuhusu hasira.

Hasira sio tatizo na wala sio hisia kuu bali ni dalili tu ya kitu kinachoendelea ndani ya mtu. Kuionyesha au kuiachilia hasira yako kwa umpendaye au mhusika yeyote hakuipunguzi hasira ile bali kuipalia makaa ili iwake vizuri.

Jinsi tunavyoitumia hasira yetu ni kitu kinachotakiwa kujifunza. Hii inamaanisha unaweza ukajifunza njia au namna mpya za kukabiliana na hasira yako na hivyo kuiweza na sio yenyewe ikuweze. 

Mwenzako au mpenzi wako hawajibiki kwa chochote katika kukukasirisha, bali wewe unawajibika.

Unajisikia vipi baada ya kuufahamu ukweli huu? Kumbuka kuwa, utendaji kazi wa haya unayoyopata hapa utakusaidia sana katika kuongeza kiwango cha amani na utoshelevu katika uhusiano na maisha yako kwa ujumla.

Hasira ni kile kitu tunachokiita hisia ya upili (Secondary emotion) sio hisia ambazo ndio msingi au za kwanza. Ni mchakato mzima wa kutuma ujumbe kukuambia kwamba, kuna kitu kinaendelea ndani yako. Hasira husababishwa na hofu, maumivu au kuchanganyikiwa.

Unaweza kuwa na hofu kuwa mpenzi wako atakuzidi nguvu, uwezo au sauti, unaogopa kupelekeshwa au kutawaliwa, unaogopa kudharauliwa au kutoheshimika, basi kwa kujilinda na hofu hii unajikuta unawaka kwa hasira.

Wakati wowote unapojihisi kuwa na hasira jiulize, je kuna kitu unachokiogopa?  Hofu yangu ni nini? Hisia zangu zikoje? 

Usihofu kumwambia mpenzi wako unavyohisi hofu fulani na kujua kama  yuko tayari mliongelee.  Mwambie ni bora mliongelee kuliko ujikute unakarisika.