BAADA ya ushindi wa mabao 2-0, Kocha mkuu wa Namungo, Juma Mgunda amesema kikosi hicho kimerudi kwenye ushindani katika Ligi Kuu Bara, huku akiwapongeza wachezaji kwa kuamua kutimiza vyema wajibu.
Ushindi ilioupata Namungo umeifanya kufikisha pointi tisa kwenye mechi saba ilizocheza ikishinda mbili, sare tatu na kupoteza michezo miwili.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mgunda alisema mchezo haukuwa rahisi kwani wachezaji walilazimika kufanya kazi kubwa kuhakikisha wanatimiza kile walichoelekezwa mazoezini.
“Bado tuna safari ndefu kuhakikisha tunafikia malengo yetu, lakini nafikiri hiki tulichokipata dhidi ya Dodoma Jiji kimeturudisha kwenye morali,” alisema na kuongeza:
“Mchezo ujao tutakuwa ugenini dhidi ya Mbeya City. Ni muda sahihi kufanyia kazi upungufu mchache niliouona dhidi ya Dodoma Jiji kabla ya kuvaana na City.”
Mgunda alisema ligi ni ngumu kwa kuwa timu zote zimefanya maandalizi vizuri hususan katika mbinu na usikivu wa wachezaji na ndivyo vinavyoamua matokeo ndani ya dakika 90 za mchezo, hivyo anaamini watakutana na Mbeya City bora ambayo itawapa ushindani.
“Hakuna timu rahisi zote ni bora na ndio maana zinashiriki Ligi Kuu. Utofauti ni ubora wa ushindani ndani ya dakika 90, mbinu bora na ushindani wa wachezaji 22 uwanjani ndio unaamua matokeo.”