:::::::::
Na Mwandishi wetu, Belem, Brazil
Afrika imeendelea kusisitiza hitaji la kuwepo kwa ufadhili wa uhakika, endelevu na wa kutosha kwa ajili ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, ikionya kuwa bila rasilimali za kutosha na msaada wa kweli katika utekelezaji, maamuzi yanayofikiwa katika majukwaa ya kimataifa yataendelea kubaki kuwa ahadi na maneno mazuri yaliyopo kwenye nyaraka pekee, bila kuleta mabadiliko kwa maisha ya mamilioni ya jamii zinazo athirika.
Akizungumza kwa niaba ya nchi 54 wanachama wa Kundi la Wajadiliano wa Afrika (AGN) katika mkutano wa kufunga wa COP30, ambapo mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu tabianchi ulipitisha uamuzi wake wa mwisho uliofanyika Belém, Brazil jana, Mwenyekiti wa AGN kutoka Tanzania, Dk Richard Muyungi, alisema Afrika inahitaji ufadhili wa kuaminika ili kubadilisha ahadi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kuwa hatua halisi za kimazingira.
“Licha ya hatua zilizopigwa katika Lengo la Kimataifa la Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi, ukosefu wa mifumo ya kifedha iliyo wazi na madhubuti unatishia kudhoofisha juhudi za Afrika za kulinda wananchi wake dhidi ya athari kali za mabadiliko ya tabianchi zinazozidi kuongezeka,” alisema Dk Muyungi.