Tanesco yazidi kufanya mageuzi maboresho ya umeme

Dodoma. Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi amesema Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limeendelea kufanya mageuzi katika kuboresha upatikanaji wa  huduma ya umeme nchini, hatua ambayo imeongeza imani na fursa mbalimbali za kiuchumi kwa wananchi.

Waziri Ndejembi amesema hayo jana Novemba 22, 2025, mkoani Dodoma katika kikao chake na viongozi wa Tanesco kilichokuwa na lengo la kufanya tathmini na kukumbushana majukumu muhimu ya kuwahudumia wananchi. Amewataka watendaji wa Tanesco kuongeza kasi na ubunifu katika kuwaunganishia wananchi umeme kama sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Misheni 300.

Ndejembi amesema ili mpango huo utekelezeke ipasavyo, ni lazima kuwachukulia hatua za kisheria makandarasi wote watakaobainika kuwa wazembe au kushindwa kuendana na kasi ya Serikali ya kuhakikisha kila Mtanzania ananufaika na huduma ya umeme.

“Nawapongeza Tanesco kwa kazi kubwa na nzuri ya kuwafikishia wananchi huduma ya umeme, lakini bado tuna kazi kubwa mbele yetu. Ongezeni ubunifu na mbinu bora za kuwaunganishia wananchi umeme kwa haraka. Ninaamini tukishirikiana na wadau wetu, tutafikia lengo la kuwaunganishia wateja milioni 1.7 kwa mwaka,” amesema Ndejembi.

Akizungumza katika kikao kazi hicho, Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba amemshukuru Rais, Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza katika miradi ya umeme ambayo imekuwa na dhamira ya dhati ya kuhakikisha, wananchi wote mijini na vijijini wanafikiwa na huduma ya umeme.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba amesema Tanesco imekuwa ikitekeleza miradi yake kwa viwango vya kimataifa, hatua inayofanya Tanzania kuwa kielelezo kwa mataifa mengine katika ujenzi na usimamizi wa miradi ya umeme.

Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco, Balozi Zuhura Bundala amesema shirika hilo lina watendaji wazalendo na wenye kujituma, wanaoendelea kufanya kazi kwa bidii.


Hata hivyo, amesisitiza kuwa bodi hiyo itaendelea kushirikiana na shirika ili kufikia malengo yaliyowekwa na Serikali.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Lazaro Twange amesema katika kipindi cha siku 100 za utendaji wa Rais Samia, Shirika litakamilisha miradi ya umeme  kwa kasi zaidi, ukiwemo mradi wa kuzalisha umeme wa jua wa Kishapu, ambao kwa sasa umefikia asilimia 83 ya utekelezaji.

“Katika kipindi cha siku 100 za Rais Samia Suluhu Hassan madarakani, tumejipanga kuhakikisha baadhi ya miradi ya umeme iwe imekamilika ukiwemo wa umeme wa jua wa Kishapu. Pia tunaendelea na mkakati wa kuwaunganishia wananchi umeme, lengo likiwa ni kuwafikia wateja milioni 1.7 kwa mwaka,” amesema Twange.

Kikao kazi hicho kimewahusisha viongozi wa ngazi ya juu wa Tanesco, mkurugenzi wa kanda, mameneja wa mikoa na wilaya.