Wanane wakiwemo wa familia moja watupwa jela kwa mauaji

Arusha. Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Dodoma, imewahukumu watu wanane, wakiwamo ndugu wa familia moja kifungo cha miaka minne na wengine miaka miwili baada ya kupatikana na hatia ya kusababisha kifo cha Daud Kitonka.

Mahakama ilibaini kuwa marehemu aliuawa wakati washtakiwa wakijaribu kumpa somo kwa madai ya kumfanyia ukatili mkewe, ambaye pia ni miongoni mwa washtakiwa.

Katika shauri hilo, ilidaiwa kuwa washtakiwa hao walipanga na kutekeleza mpango wa kumpiga Kitonka kwa lengo la kumuonya kutokana na tabia yake ya kumdhulumu mke wake mkubwa mwenye umri wa miaka 59.

Waliohukumiwa ni Abson Mombasa, Zakaria Kitundu, Athuman Seif, Neema Makala (mpwa wa Emiliana), Rose Makala (mpwa wa Emiliana), Anna Kitonka (mtoto wa marehemu), Philipo Chidonga na Emiliana Mwandu (mke wa marehemu).

Abson, Zakaria, Athuman, Neema, Rose, Anna na Philipo wamehukumiwa kifungo cha miaka minne jela, huku Emiliana akipewa kifungo cha miaka miwili.

Mahakama pia ilimwachia huru mshtakiwa wa tano, Martha Kitonka (mtoto wa marehemu), kwa masharti ya kutotenda kosa lolote la jinai katika kipindi cha miezi sita.

Hukumu hiyo ilitolewa Novemba 19, 2025 na Jaji Evaristo Longopa, aliyesikiliza shauri hilo, huku nakala ya hukumu ikitarajiwa kupatikana kupitia mfumo wa mtandao wa Mahakama.

Washtakiwa wote tisa walikiri kosa la kuua bila kukusudia, kinyume na kifungu cha 195 na 198 vya Kanuni ya Adhabu. Mauaji hayo yalitokea katika Kijiji cha Kinanilya, Kata ya Kisisiri, Wilaya ya Iramba mkoani Singida.

Chanzo cha tukio hilo kilielezwa kuwa ni jaribio la kutoa adhabu ya somo kwa marehemu Kitonka, kutokana na madai ya kumfanyia mkewe ukatili.

Baada ya kukiri, upande wa Jamhuri uliiomba mahakama itoe adhabu kali kwa baadhi ya washtakiwa, hasa wale waliodaiwa kuhusika katika kupanga tukio hilo.

Upande wa Jamhuri ulidai kuwa mshtakiwa wa tano alipaswa kuchukua tahadhari ambayo ingeweza kuzuia madhara yaliyotokea, hivyo naye alistahili onyo sawa na wale waliotekeleza mpango huo.

Ilibainishwa pia mahakamani hapo kuwa silaha iliyotumika ilielekezwa katika maeneo nyeti ya mwili wa marehemu, hivyo washtakiwa walipaswa kupendekeza njia nyingine badala ya kutumia nguvu kupita kiasi.

Kwa upande wa utetezi, mawakili waliiomba mahakama kupunguza adhabu, wakieleza kuwa washtakiwa hawana rekodi ya uhalifu, wametubu na walishirikiana na polisi tangu walipokamatwa Septemba 2023.

Pia, walisisitiza kuwa washtakiwa ni nguvu kazi ya taifa na wamekaa mahabusu kwa zaidi ya miaka miwili.

Kuhusu Emiliana, mawakili wa utetezi walisema alikuwa mwathirika wa unyanyasaji wa kifamilia na umri wake ni mkubwa, hivyo kuomba apunguziwe adhabu, hoja ambayo mahakama iliizingatia kwa kumpa kifungo kifupi zaidi.

Jaji Longopa alisema Mahakama imechukua muda kutathmini kwa makini mazingira yote yaliyosababisha kifo cha Kitonka kabla ya kutangaza adhabu.

Alisema kisheria, adhabu ya juu kwa kosa la kuua bila kukusudia ni kifungo cha maisha jela, lakini Mahakama ina mamlaka ya kuangalia mazingira ya tukio na kutoa adhabu stahiki kulingana na uzito wa shauri husika.

Kwa mujibu wa Jaji Longopa, mazingira ya kesi hiyo yanaangukia katika kiwango cha kati cha kosa la kuua bila kukusudia, ambacho kwa kawaida adhabu yake huwa kati ya miaka mitano hadi 10 jela. Hivyo, alisema msingi wa adhabu ungeweza kuanzia miaka saba.

Hata hivyo, alieleza kuwa baada ya kuzingatia hoja za pande zote mbili, ikiwamo kukiri kwa washtakiwa, kujutia kwao makosa, na muda waliohudumu mahabusu tangu mwaka 2023 na Mahakama iliona sababu za kupunguza adhabu hiyo.

Alibainisha kuwa katika mazingira ya shauri hilo, washtakiwa wanane (isipokuwa Martha Kitonka) walikuwepo eneo la tukio na kila mmoja alichangia kwa kiwango fulani katika kitendo kilichosababisha kifo hicho.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa adhabu itazingatia tofauti za mazingira ya kila mshtakiwa, hasa kuhusu Emiliana ambaye ni mzee na mwenye changamoto za kiafya.

Kwa upande wa Martha, Jaji Longopa alisema kuwa ushahidi ulionesha hakuwepo eneo la tukio kwani wakati wa tukio hilo alikuwa Mpanda, mkoani Katavi, na alikamatwa alipohudhuria mazishi ya baba yake. Hivyo, Mahakama iliona muktadha wa shauri lake kuwa tofauti na kutoa uamuzi wa kipekee.

Baada ya tathmini hiyo, Mahakama iliwahukumu washtakiwa saba, Abson Mombasa, Zakaria Kitundu, Athuman Seif, Neema Makala, Rose Makala, Anna Kitonka na Philipo Chidonga, kifungo cha miaka minne jela.

Emiliana Mwandu, ambaye ni mke wa marehemu, alipewa kifungo cha miaka miwili kutokana na mazingira yake maalumu.

Aidha, Mahakama ilimuachia huru Martha Kitonka kwa masharti maalum. Kwa mujibu wa kifungu cha 38(1), (2) na (3) cha Kanuni ya Adhabu, anatakiwa kutokutenda kosa lolote la jinai kwa kipindi cha miezi sita kuanzia tarehe ya hukumu, vinginevyo atakabiliwa na hatua za kisheria.