Dar es Salaam. Wataalamu wa mawasiliano, afya ya akili na uchumi wameonya kuwa, utegemezi wa Watanzania katika mitandao ya kijamii umefikia kiwango cha kutisha kiasi cha kuathiri uamuzi wao wa kila siku, kuanzia namna wanavyotumia fedha, mtazamo wa maisha, wa kisiasa na kijamii.
Ongezeko la matumizi ya simu janja na kasi ya majukwaa kama TikTok, Instagram na Facebook limeibua kile wataalamu wanachokiita uamuzi unaoendeshwa na roboti.
Licha ya mitandao hiyo kuwa sehemu muhimu ya mawasiliano na uchumi, lakini wataalamu wanaonya kama haitatumika kwa uangalifu, inaweza kugeuka kuwa chanzo cha uamuzi mbaya unaoathiri mustakabali wa watu na Taifa kwa jumla.
Hali hii, kwa mujibu wa tafiti mbalimbali, inaathiri hasa vijana, wanawake na watu wa mijini, ambao hutumia kati ya saa tatu na tano kwa siku kuangalia maudhui mtandaoni.
Hivi karibuni, mtaalamu wa mawasiliano, Dk Mwanahamisi Juma amesema tatizo la utegemezi wa mitandao ya kijamii si suala la starehe tu, bali limekuwa chanzo cha uamuzi mwingi usiokuwa na tija.
“Mitandao imekuwa kama mshauri binafsi wa watu wengi. Wanaamua nini wanunue, wavae nini, waishi vipi, hata mawazo yao kuhusu ndoa na siasa yanachochewa zaidi na kile wanachokiona kuliko kile wanachofikiria,” amesema.
“Mfano, mtu anaona video ya watu wakisifu aina fulani ya kiatu, anakinunua bila kuuliza ubora au kulinganisha bei au kijana anaona video ya ‘mahusiano mazuri’ mtandaoni, anaanza kuhisi yake hayatoshi bila kujua video hizo zimepangiliwa.”
Amesema algoriti hizo za mitandao zimeundwa kupendelea maudhui yanayozalisha hisia kali hasira, mshangao au furaha na ndiyo yanayotawala zaidi kwenye machaguo ya mtumiaji husika.
“Hii inaua uwezo wa kuchuja taarifa. Mtu anapokea taarifa nyingi haraka bila muda wa kuzifanyia uchambuzi. Ukitaka kujua kwa nini watu wanafanya uamuzi mbaya wa kifedha au kijamii, angalia wanayotazama mitandaoni,” ameeleza.
Athari katika uamuzi ya kifedha
Mtaalamu wa uchumi, Georgina Mwakalinga amesema katika utafiti usio rasmi alioufanya miongoni mwa vijana, amebaini zaidi ya asilimia 60 huamua kununua bidhaa fulani baada ya kuiona ikivuma kwenye TikTok au Instagram, mara nyingi bila kuzingatia bajeti.
Mtaalamu huyo amesema mitandao imekuja na kile anachokiita uchumi wa uamuzi wa haraka, Watanzania wananunua bidhaa kwa msukumo wa papo hapo.
“Mtu anaona video ya sekunde 15 ya bidhaa fulani, anabofya link, anafanya malipo. Hili limeongeza matumizi ya fedha kupita kiasi, hasa miongoni mwa vijana wanaotaka kuendana na kile kinacho ‘trend’. Ni mtego wa kihisia,” amesema.
Akitolea mfano katika hilo, amesema bidhaa kama vipodozi ‘vinavyovuma’ au nguo za ‘challenge’ za TikTok hununuliwa sana hata kama hazihitajiki, na mara nyingi ni ghali kuliko uwezo wa mtumiaji.
Inaathiri vipi afya ya akili
Kwa upande wa afya ya akili, athari zimekuwa kubwa, wataalamu wanaeleza utegemezi wa mitandao umesababisha kuongezeka kwa msongo wa mawazo, shinikizo la kuiga maisha ya wengine na hali ya kutoridhika na maisha halisi.
Mtaalamu wa afya ya akili, Dk Mariam Mtawa amesema algoriti za mitandao zinaleta picha na video zilizohaririwa vizuri, maisha ya anasa, miili iliyo isiyo na dosari na mafanikio ya haraka.
Mtaalamu huyo amesema hali hiyo inawafanya wengi wajione bado hawajafika, jambo linaloibua msongo wa mawazo na kushuka kwa kujithamini.
“Tatizo siyo tu kutumia mitandao muda mrefu, bali kuishi maisha ambayo hayako kwenye uhalisia. Vijana wengi wanajilinganisha na ‘lifestyles’ zinazotengenezwa na influencers. Hii inajenga shinikizo la kuishi maisha ambayo uwezo wao hauendani nayo matokeo yake ni msongo wa mawazo na kujiona duni,”amesema.
Mshauri wa masuala ya familia na vijana, Sarah Mushi amesema vijana wengi wanaishi kwa kujilinganisha na watu walio kwenye mitandao bila kuelewa, wengi wao wanaonesha upande mzuri tu wa maisha.
“Unapomlinganisha kijana wa kawaida na mtu anayeishi na kamera, unamwingiza kwenye mashindano yasiyo na mwisho. Vijana wanachagua kazi, mavazi, hata mahusiano kwa kuiga kile wanachoona. Hili linawatesa sana kisaikolojia,” amesema.
“Watu wengi wanatafuta faraja mtandaoni kwa sababu huko kuna ‘likes’, ‘shares’ na ‘comments’. Lakini faraja hiyo ni ya muda mfupi mno. Kadiri mtu anavyotegemea uthibitisho kutoka mtandaoni, ndivyo anavyopoteza uwezo wa kushughulikia hisia zake bila msaada wa nje.” amesema.
Amesema kumekuwa na ongezeko la wanawake vijana wanaohisi hawatoshi bila kufuata mitindo ya urembo inayovuma mitandaoni, jambo linalowasukuma kutumia fedha nyingi kupita uwezo wao.
Mbali na masuala ya urembo na matumizi, mitandao inatajwa pia kuathiri kwa kiasi kikubwa uamuzi wa kisiasa na kijamii.
Mchambuzi wa masuala ya siasa, Festo Mkumbo amesema algoriti za mitandao zina uwezo wa kueneza taarifa kwa kasi kubwa kuliko vyombo vya habari vya kawaida, na mara nyingi bila uthibitisho.
“Taarifa za uongo, video zilizohaririwa au hoja zinazopotosha zinaweza kuunda maoni ya umma haraka mno. Watu huamini kile kinachowafikia kwanza, na mara nyingi hawachukui muda wa kuhakiki.
“Hii ni hatari. Inaweza kuongeza migawanyiko katika jamii, hasa wakati wa masuala yanayogusa hisia kama siasa, elimu au dini,”amesema.
Mathalani kipande kifupi cha video kinachokatwa vibaya kinaweza kumharibia mtu taswira au kuchochea chuki katika jamii. Pia, wakati wa uchaguzi, taarifa zisizo sahihi huzagaa na kuathiri chaguzi na maelewano.
Mwanasaikolojia Saida Lema amesema hali hiyo inasababisha watu kupoteza uwezo wa kujitegemea katika kufikiria.
Amesema jamii inazidi kutegemea mitandao kwa kila jambo, hali inayoondoa uhuru wa kufikiri.
“Leo mtu anataka kununua nguo anaingia TikTok. Anataka kufunga ndoa naangalia nini kinafanyika mtandaoni katika eneo hilo maarufu trends. Anataka kuanza biashara anaangalia video za watu wanaoonesha mafanikio. Hatuangalii tena mazingira halisi ya maisha yetu,” amesema Saida.
Mwanasaikolojia huyo anaonya bila miongozo ya wazi ya elimu ya matumizi ya mitandao, kizazi kijacho kitapoteza kabisa uwezo wa kufanya uamuzi kwa kuzingatia hali halisi, uzoefu na tafakuri.
Kukabiliana na hilo mwanasaikolojia huyo ameshauri Serikali na taasisi za elimu kuanzisha elimu ya matumizi sahihi ya mitandao kuanzia shule za msingi.
“Serikali na taasisi za elimu zinapaswa kuingilia kati sio tu kuanzisha elimu ya matumizi ya mitandao, lakini pia kuunda miongozo ya maadili ya mitandao kwa vijana. Tunahitaji mchakato wa mafunzo unaoanzishwa mapema ili vijana waendelee kuwa na uwezo wa kuchambua maudhui wanayoyaona.
“Msisitizo wangu mwingine ni kwa watumiaji wa mitandao kujenga tabia ya kuchunguza taarifa kabla ya kuziamini, usifanye uamuzi wa kifedha na kijamii kwa shinikizo la kile kinachovuma mitandaoni,” amesema Saida.