Lindi/Dar. Baadhi ya wakulima wa korosho wa mikoa ya Lindi na Mtwara wamelalamikia namna minada ya zao hilo inavyoendeshwa katika msimu wa mwaka 2025/26, wakidai kukosekana uwazi na ushirikishwaji.
Hata hivyo, Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika Lindi Mwambao, Nurudin Said amekana madai ya wakulima kutoshirikishwa, akisema mfumo wa minada unahitaji wawakilishi kutokana na ugumu wa kuwakusanya wote kwa wakati mmoja.
“Minada haiwezi kuwakutanisha wakulima wote kwa mara moja. Lindi Mwambao inafanya kazi na halmashauri zaidi ya moja, Kilwa, Mtama na Lindi Manispaa. Kila wiki tunafanya mnada kwenye halmashauri moja ili kuwakuta wakulima huko,” amesema Said.
Awali, wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, wakulima wamesema minada inafanyika kwenye ofisi za Serikali badala ya maeneo ya wazi kama ilivyokuwa awali, hali inayowanyima fursa ya kushuhudia mwenendo wa bei na mchuano wa wanunuzi.
Akizungumza hivi karibuni, mkulima wa zao hilo mkoani Lindi, Sharifu Juma amesema minada inapaswa kufanyika hadharani ili wajue bei halisi.
“Minada sasa inafanyika kwenye ofisi za Serikali kama za halmashauri au manispaa, tunasikia tu kuhusu bei ambazo haturidhiki nazo. Ni muhimu irudi kwa wakulima tujue soko linavyokwenda,” amesema Juma.
Mkulima kutoka Ng’apa, Ibrahim Mmwera amesema mfumo wa mtandao umeleta mkanganyiko kwa baadhi ya wakulima.
“Hadi leo mimi na wenzangu hatujui korosho zetu zimeuzwa kwenye mnada upi. Zamani minada ilikuwa wazi na wakulima walishuhudia bei,” amesema Mmwera.
Vilevile, wakulima wamedai kuwa, baadhi ya viongozi wa Vyama vya Ushirika vya Msingi (Amcos), wanaowawakilisha si wakulima halisi wa korosho, hivyo wanahisi uamuzi wao hauendani na masilahi yao.
“Wakulima tukishuhudia minada, tunajua iwapo bei inakidhi au la. Sasa tunapewa tu taarifa na bei inayotolewa ni ndogo,” amesema Muanya Saidi, mkulima mkazi wa Lindi.
Sesilia Mtatiro, mkulima wa Namangale amesema licha ya kupatiwa pembejeo bure, bado bei ya korosho inaendelea kuwa chini.
“Tunahitaji Serikali kufanya mazungumzo na wanunuzi ili kuwe na bei nzuri zaidi,” amesema.
Swahiba Bakari kutoka Tandahimba mkoani Mtwara, amesisitiza umuhimu wa minada kuendelea kufanyika vijijini.
“Minada ikifanyika mijini wakulima wengi hushindwa kuhudhuria. Ni muhimu irudi vijijini ambako ndipo wakulima wengi wapo,” amesema Mtatiro.
Kwa mujibu wa wakulima hao, bei ya juu ya korosho msimu wa mwaka jana ilikuwa Sh3,070 huku ya chini ikiwa Sh2,830.
Kwa msimu wa mwaka huu, bei ya juu ni Sh2,460 na ya chini ni Sh2,310.
Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika Lindi Mwambao, Nurudini Said amesema kama minada haifanyiki vijijini moja kwa moja, hufanyika kwenye maeneo ya kati na salama yanayofikika na wakulima.
“Ni kweli hatuendi vijijini moja kwa moja, lakini tunapoweka center (kituo) tunahakikisha wakulima wanafika. Uamuzi wa mwisho juu ya bei upo mikononi mwa wakulima wenyewe,” amesema Said.
Amepinga madai kuwa, viongozi wa Amcos hukubali bei ndogo kwa masilahi binafsi akisema: “Si kweli. Kila mnada uamuzi hufanywa na wakulima waliopo. Mfumo hauwezi kuwakusanya wote, lakini wawakilishi wao huamua bei.”
Akizungumzia madai kuwa Lindi Mwambao inapaswa kujadiliana na wanunuzi kuongeza ushindani wa bei Said amesema:
“Sisi hatufanyi usajili wa wanunuzi. Hilo linafanywa na Bodi ya Korosho na Soko la Bidhaa Tanzania (TMX). Wao ndio wanaowajua wanunuzi na idadi yao.”
Amesema mfumo wa mnada wa mtandao ni wa wazi na wa ushindani mkubwa.
“Wajibu wetu ni kuhakikisha kila mnada unapofanyika wakulima wanakuwepo na wanashiriki,” amesema Said.
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telak amesema minada michache ya mwanzo ililazimika kufanyika katika ofisi za Serikali kutokana na changamoto za mtandao.
“Tulipoanza minada, mtandao ulikuwa chini. Tuliamua kutumia ofisi za halmashauri ili kupata mawasiliano ya uhakika na kuzuia korosho zisiharibike kwa mvua,” amesema Telak.
Amesema lengo halikuwa kuwanyima wakulima uwazi, bali kuhakikisha minada inaendelea bila kuathiri ubora wa zao.
Kuhusu madai kuwa wakulima hawapo minadani amesema: “Nimezindua minada hapa Lindi na niliona wakulima wakishuhudia. Kwa hiyo si kweli kwamba hawashirikishwi.”
Akizungumzia kuhusu kushuka kwa bei ya korosho, Telak amesema kunatokana na tofauti za mahitaji na uzalishaji duniani.
“Huwezi kulinganisha bei ya mwaka huu na ya mwaka jana, bila kuangalia hali ya soko. Soko linafanya kazi kwa misingi ya biashara,” amesema Telak.
Amesema faida ya mkulima inategemea uzalishaji, “korosho ni biashara, ukilima kwa wingi utapata faida kubwa.”