Dar es Salaam. Benki ya Diamond Trust (DTB) imeweka mikakati ya kupanda miti milioni moja hadi ifikapo mwaka 2030.
Tayari benki hiyo imeshapanda miti 150,000 kupitia ushirikiano na wadau mbalimbali, ikiwemo shule na jamii.
Ofisa Masoko wa DTB, Irene Daniel, akizungumza na Mwananchi leo Jumapili, Novemba 23, 2025, kuhusu mkakati huo, amesema unalenga kurejesha mifumo ya ikolojia, kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa na kuimarisha bioanuwai.
Amesema mkakati huo ni dhamira ya benki hiyo katika kuhifadhi mazingira na kuhimili mabadiliko ya tabianchi kwa muda mrefu.
Daniel amesema DTB imeimarisha juhudi zake za muda mrefu za uhifadhi kupitia ushirikiano mpya wa kimkakati na Lions Club.
“Tumeingia makubaliano ya kimkakati yanayolenga kulinda na kurejesha mazingira kwa kuongeza kwa kiasi kikubwa upandaji wa miti katika jamii za hapa nchini,” amesema.
Daniel amebainisha kuwa miche inayotumika katika mradi huo imetolewa na Caravans Cricket Club, akieleza jinsi taasisi mbalimbali zinavyoweza kushirikiana kwa ajili ya matokeo chanya ya kimazingira.
Akizungumza katika kazi ya upandaji miti uiliyofanyika jana, Novemba 22, 2025, katika Shule ya Sekondari Songoro Mnyonge, Kaimu Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Emmanuel Mafuru, ameeleza kufurahishwa kwake na DTB kwa kutoa miti ya kivuli na ya matunda itakayowanufaisha wanafunzi na wakazi wa maeneo jirani.
Aidha, ametaja changamoto zinazoendelea kuikabili shule hiyo, ikiwemo uhaba wa vitabu, upungufu wa madawati na viti, pamoja na uhitaji wa kuboreshwa kwa viwanja vya michezo na ukumbi wa chakula.
“Wakati miti ina mchango mkubwa katika kuboresha mazingira ya shule, msaada endelevu katika maeneo haya mengine utaboresha kwa kiasi kikubwa mazingira ya kujifunzia na ustawi wa wanafunzi,” amesema Mafuru.
Makamu Mwenyekiti wa Lions Club ya Dar es Salaam Sky, Badriya Osman, amesema dhamira ya klabu hiyo ni kuendeleza kampeni za mazingira nchini.
Amesema klabu inaendelea kusambaza miche kwa jamii, shule na taasisi mbalimbali ili kuhimiza utunzaji endelevu wa mazingira.
“Katika shule hii pekee, tumefanikiwa kupanda miti 200, ambayo 175 ni ya kivuli na 25 ya matunda, ambayo itatoa manufaa ya kimazingira na kijamii kwa muda mrefu,” amesema.
Wataalamu wa mazingira wamebainisha kuwa upandaji miti ni moja ya njia bora zaidi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Miti husaidia kunyonya hewa ukaa, kutoa oksijeni na kudhibiti joto.
Shuleni, miti ya kivuli hupunguza joto, kuunda maeneo mazuri ya kujifunzia nje na kuboresha ubora wa hewa. Miti ya matunda pia hutoa manufaa ya lishe na kiuchumi.
“Kuongezeka kwa uoto wa miti pia husaidia kuzuia mmomonyoko wa udongo, kuimarisha bioanuwai na kuboresha thamani ya mazingira kwa ujumla,” wamesema wataalamu.