Simiyu. Serikali itatoa hati za kimila 6,000 kwa wakulima na wafugaji katika halmashauri sita za Mkoa wa Simiyu, ikiwa ni hatua ya kuongeza thamani ya maeneo yao, kuimarisha utunzaji wa mazingira na kuongeza uwezo wa jamii kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumza leo Jumapili Novemba 23, 2025 wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wakulima na wafugaji, Meneja wa mradi wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi mkoani Simiyu, Mhandisi Gogadi Mgwatu amesema mradi huo unalenga kurejesha uoto wa asili kwa kupanda miti na nyasi za malisho.
Amesema utoaji wa hati za kimila utarahisisha upangaji bora wa matumizi ya ardhi, kutenganisha maeneo ya kilimo na malisho pamoja na kuwezesha upandaji wa miti kupitia mfumo wa ngitili.
Mfumo wa ngitili ni utaratibu wa hifadhi na urejeshaji wa malisho na miti kwenye maeneo ya vijijini, hasa unaotumika katika mikoa ya kanda ya magharibi kama Shinyanga na Simiyu.
“Mara nyingi migogoro hutokana na ukosefu wa mipaka na umiliki rasmi wa ardhi. Hati hizi 6,000 zitawasaidia wakulima na wafugaji kuwa na maeneo yenye uhakika, kuongeza thamani ya ardhi yao na kuweka mfumo bora wa utunzaji wa mazingira,” amesema.
Kwa upande wake, Raymond Makanga kutoka Mradi wa Simiyu Climate Resilience amesema zaidi ya wakulima na wafugaji 200 kutoka halmashauri zote sita wamepewa mafunzo ili kuhamasisha utunzaji wa mazingira na kurejesha uoto wa asili.
“Mabadiliko ya tabianchi yameathiri uzalishaji, hivyo jamii inapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuhifadhi mazingira na kupanda miti,” amesema.
John Machibya, mkulima kutoka Wilaya ya Bariadi, amesema hatua ya kupatiwa hati za kimila inawapa matumaini mapya.
“Kwa muda mrefu tumekuwa tukilima bila uhakika wa umiliki. Kupata hati kutatupa nguvu ya kuwekeza zaidi, kupanda miti na kutumia ardhi kwa mpangilio,” amesema.
Naye Julius Ntimba, mkulima na mfugaji kutoka Wilaya ya Meatu, amesema elimu waliyopewa itasaidia kupunguza uharibifu wa mazingira.
“Hapa tulizoea kuchoma moto tukidhani tunatengeneza malisho. Lakini tumejifunza kuwa miti na maeneo ya malisho ya mifugo kwa mfumo wa Ngitili yanaweza kutoa malisho mengi zaidi na kuzuia mmomonyoko wa ardhi,” amesema.
Kwa upande wake, Sofia Nyambalya mfugaji kutoka Wilaya ya Itilima, amesema hati za kimila zitapunguza migogoro ya mipaka.
“Migogoro imekuwa ikituchosha. Tukipata hati, kila mmoja atajua eneo lake na sehemu maalum za malisho bila kuvamia mashamba ya wengine,” amesema.
Utekelezaji wa mpango wa Ngitili, unaohusisha uhifadhi na upandaji miti katika maeneo maalumu ya malisho, unatarajiwa kupunguza athari za ukame, kuongeza uzalishaji na kuboresha mfumo wa ikolojia katika maeneo ya wafugaji.