Dar es Salaam. Kipindi cha kusubiri matokeo ya mitihani ya kidato cha pili na cha nne, ni hatua muhimu katika safari ya elimu ya mtoto.
Mara nyingi muda huu huwa mrefu na huambatana na changamoto mbalimbali, ikiwamo kupungua kwa mwamko wa kusoma, kujiingiza katika makundi yasiyofaa, au kusahau kabisa maarifa aliyojifunza.
Hii ndiyo sababu mzazi anapaswa kutambua nafasi yake ya msingi katika kuhakikisha mtoto anautumia muda huo vyema, bila kupoteza mwelekeo wa masomo na malengo yake ya baadaye.
Shaibu Hamza, mtaalamu wa masuala ya malezi anasema mzazi anatakiwa kuhakikisha mtoto anaendelea kuwa kwenye utaratibu wa kujifunza.
“Ingawa mtihani umekwisha, mtoto anaweza kuandaliwa ratiba nyepesi ya kujisomea ili kuendeleza umilisi wa masomo aliyoanza kuyaelewa shuleni,” anasema Hamza.
Anasema ratiba hiyo isiwe ya kumchosha, bali iwe na mazingira rafiki yanayomwezesha kukumbuka na kujifunza bila shinikizo na anaongeza kuwa mzazi anaweza kumsaidia mtoto kutenga muda wa kupitia mada alizoziona kuwa ngumu, kufuatilia mihutasari au kufanya majaribio kupitia vitabu au mitandao ya elimu.
Naam, Hamza anakumbusha jambo jema. Kipindi hiki karibu familia nyingi zina hawa watoto ambao wamefanya mitihani ya kidato cha Pili na cha Nne ambao wako nyumbani wameshahitimu.
Hivyo nimeona kuna umuhimu wa kuungana na kauli ya Hamza kuwa, ni muhimu mzazi akaendelea kuwasiliana kwa ukaribu na mtoto kuhusu malengo yake ya kielimu.
Mazungumzo ya mara kwa mara yanaweza kumsaidia kubaki na mtazamo chanya, kutambua mustakabali wake na kujenga nidhamu binafsi.
Katika mazungumzo hayo, mzazi anaweza kumsaidia mtoto kutafakari aina ya mchepuo anaoupenda atakapofikia hatua inayofuata, pamoja na fursa zinazopatikana katika uwanja wa elimu na ajira.
Hii nayo humsaidia mtoto kutambua kuwa kipindi cha kusubiri matokeo sio likizo ya kupumzika kupita kiasi, bali sehemu ya maandalizi ya safari ndefu ya masomo.
Aidha, mzazi anapaswa kumuhusisha mtoto katika shughuli za kujenga stadi mpya. Kipindi hiki kinaweza kutumika kumpa maarifa ya vitendo kama vile kompyuta, ufundi mdogo, utunzaji wa bustani, usomaji wa vitabu vya ziada, au kujifunza lugha mpya.
Wataalamu wanasema stadi hizi humjenga mtoto kifikra na kumsaidia kuimarisha uwezo wa kufikiri kwa mantiki, jambo ambalo ni muhimu kwa maendeleo ya kitaaluma.
Kupitia shughuli hizi, mzazi humuepusha mtoto na mazingira ya kukaa bila kazi ambayo mara nyingi yanaweza kumvuta kwenye vishawishi visivyofaa.
Katika kuhakikisha mtoto hasahau masomo, mazingira ya nyumbani yanapaswa kuwa rafiki kwa kujifunza. Mzazi anaweza kujipa jukumu la kuweka utaratibu unaozuia kelele zisizohitajika, filamu nyingi au michezo ya mtandaoni ambayo huondoa umakini.
Ingawa watoto wanahitaji muda wa kupumzika, kuwepo kwa uwiano kati ya burudani na kusoma ni muhimu, kusudi kumuepush na uzembe wa kiakili unaoweza kumfanya mtoto akose mwelekeo wa masomo anaporejea shule.
Kipindi cha kusubiri matokeo pia kinaweza kuwa nafasi ya kumjengea mtoto maadili na tabia njema. Malezi mema yanachangia pakubwa katika maendeleo ya kitaaluma.
Mzazi anaweza kumfundisha umuhimu wa muda, nidhamu, kuheshimu watu na kujituma. Tabia hizi zinapojengeka mapema, huwa msingi thabiti wa mafanikio ya kielimu na hata ya maisha. Hivyo, malezi ya tabia yanapaswa kupewa kipaumbele sawa na pale anapokuwa shuleni.
Vilevile, ni muhimu mzazi kufuatilia mwenendo wa marafiki wa mtoto wakati wa kusubiri matokeo. Katika kipindi hiki, vijana hujihusisha zaidi na marafiki, hivyo mzazi anatakiwa kuhakikisha mtoto anakaa na kundi linalomjenga kiakili na kimaadili.
lisilo sahihi linaweza kumshawishi mtoto ajihusishe na vitendo visivyofaa kama vile matumizi ya dawa za kulevya, uvivu au mienendo inayopoteza mwelekeo wa maisha. Ushirikiano wa karibu kati ya mzazi na mtoto humsaidia kijana kujiweka mbali na mazingira hatarishi.
Kusubiri matokeo kunaweza kumfanya mtoto kuwa na wasiwasi, hususan endapo alikabiliwa na changamoto wakati wa mitihani. Kwa kuonesha upendo na kumtia moyo, mzazi humsaidia mtoto kubaki mtulivu na kujiamini. Hii humjenga kisaikolojia na kumfanya awe tayari kwa hatua inayofuata.
Kwa ujumla, wajibu wa mzazi wakati mtoto anasubiri matokeo ni mkubwa kuliko inavyodhaniwa.
Mzazi anayemsaidia mtoto kupanga ratiba, kumjengea maadili, kumhusisha katika stadi mpya, na kumtia moyo humsaidia kijana kuendelea kukua kisomo na kimtazamo.
Hii inamwezesha kurudi shule akiwa na ari mpya ya kujifunza na uwezo wa kukabiliana na changamoto za masomo kwa ujasiri na uthabiti.