Kipenye, Chamungu wana jambo Namungo

NYOTA wa Namungo, Cyprian Kipenye, amesema kati ya malengo aliyojiwekea na mchezaji mwenzake, Andrew Chamungu, ni kuhakikisha wanaendelea kufanya vizuri na kuendeleza pacha kali na timu hiyo, kama walivyofanya wakiwa na Songea United.

Wachezaji wote wawili wamejiunga na kikosi hicho msimu huu, baada ya kuachana na timu ya Songea United inayoshiriki Ligi ya Championship, huku msimu wa 2024-2025, Chamungu aliifungia mabao tisa, wakati Kipenye akiifungia matano.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kipenye amesema ushirikiano kati yake na Chamungu wakati wakiwa na Songea United na sasa Namungo, ni mwendelezo wao kutaka kufanya mambo makubwa zaidi msimu huu, licha ya ushindani mkubwa uliopo katika Ligi Kuu na pia wa kuwania nafasi ya kucheza.

“Tulipotoka tulipata nafasi ya kucheza sana katika kikosi cha kwanza ila hapa ni tofauti kwa sababu wapo wachezaji wengi na bora, hivyo, ili ucheze ni lazima ushawishi benchi la ufundi, jambo kubwa kwetu tumeshaanza vizuri,” amesema Kipenye.

Aidha, Kipenye amesema katika mechi ya Ligi Kuu Bara ambayo Namungo ilishinda mabao 2-0, dhidi ya Dodoma Jiji Ijumaa iliyopita alipewa Sh5,000 na Chamungu kwa lengo la kumpa motisha, baada ya kufunga bao moja akitokea benchini.

Katika mabao sita ya Ligi Kuu Bara iliyofunga Namungo msimu huu, nyota hao wote wawili wamechangia manne, ambapo Kipenye amechangia mawili, baada ya kufunga moja na kuasisti jingine pia moja, huku kwa upande wa Chamungu akiasisti mengine mawili.