KOCHA wa TRA United, Mrundi Etienne Ndayiragije, ameweka rekodi mbili na timu hiyo baada ya ushindi wa bao 1-0 juzi Jumamosi dhidi ya Tanzania Prisons katika mechi ya Ligi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, mjini Tabora.
Bao la dakika ya 55 la Ramadhan Chobwedo limemfanya Ndayiragije kushinda mechi ya kwanza na kikosi hicho msimu huu, ila ni ushindi wa kwanza pia kwa TRA katika Ligi, tangu iliposhinda mara ya mwisho dhidi ya Dodoma Jiji iliyowanyoa bao 1-0 Februari 28, 2025.
Hii ina maana kuwa, tangu Februari 28 TRA United (zamani Tabora United), ilicheza mechi 11 mfululizo za Ligi Kuu Bara kuanzia msimu wa 2024-2025 hadi huu wa 2025-2026 bila ya ushindi na kilichofanywa na Ndayiragije kimevunja mwiko huo na kuandika rekodi mpya kwa kocha huyo.
Katika mechi hizo 11 za Ligi Kuu ambazo timu hiyo haijashinda kuanzia msimu uliopita hadi sasa, ilipoteza saba na kutoka sare nne, ambapo safu ya ushambuliaji ya kikosi hicho ilifunga mabao manne tu na yenyewe kuruhusu 21.
NDAYI 01
Kabla ya ujio wa Ndayiragije, timu hiyo ilianza msimu huu ikiwa na kocha msaidizi, Mkenya Kassim Otieno, aliyeiongoza katika mechi tatu za Ligi Kuu, ambapo kati ya hizo alitoa zote sare, akifunga mabao mawili na kuruhusu pia mawili.
Akizungumza baada ya mechi hiyo, Ndayiragije, amesema ni jambo la furaha kwake kuanza na ushindi katika mechi ya kwanza, ingawa moja ya mambo anayoshukuru ni jitihada za wachezaji walizoonyesha, kwa sababu hajapata muda mrefu wa kukaa nao.
Ndayiragije amejiunga na timu hiyo baada ya kuachana na Polisi Kenya, Oktoba 29, 2025 baada ya kudumu kwa siku 333, tangu ateuliwe kikosini humo, huku akiipa ubingwa wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) msimu wa 2024-2025.
Kocha huyo aliipa Polisi Kenya ubingwa huo ukiwa ni wa kwanza kwa kikosi hicho katika historia tangu kilipopanda daraja 2021 na kuzima utawala wa Gor Mahia iliyochukua mara mbili mfululizo kuanzia msimu wa 2022-2023 na 2023-2024.
Ndayiragije aliyezifundisha Mbao FC, Azam, KMC na timu ya taifa, Taifa Stars, ni miongoni mwa makocha wenye uzoefu mkubwa na Ligi Kuu Bara kutokana na timu alizofundisha, jambo lililochangia kukabidhiwa kikosi hicho, akishirikiana na Kassim Otieno.