Kigoma. Haijaisha mpaka imalizike. Ni usemi unaoweza kuelezea hatua ya wapigakura wanne wa Jimbo la Kigoma Mjini kufungua shauri la uchaguzi wakipinga ushindi wa mbunge wa jimbo hilo (CCM), Clayton Chipando maarufu Baba Levo.
Wapigakura hao wamewasilisha sababu 35 kuthibitisha kile wanachodai kuwa ubunge wa Baba Levo ni batili, hivyo ufanyike uchaguzi mdogo huku wakiwataja wasanii maarufu, Naseeb Abdul au Diamond Platnumz na Zuhura Soud maarufu Zuchu.
Katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 29, 2025, Baba Levo aliyeapishwa kuwa mbunge bungeni mjini Dodoma Novemba 11, alipata kura 35,727, akifuatiwa na mshindani wake wa karibu, Zitto Kabwe wa ACT Wazalendo, aliyepata kura 16,619.
Shauri hilo, lililofunguliwa Mahakama Kuu Kigoma Novemba 14, 2025, dhidi ya Msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo la Kigoma Mjini, Baba Levo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), inasikilizwa na Naibu Msajili Fadhili Mbelwa na itatajwa Novemba 26, 2025.
Katika shauri namba 28949 la mwaka 2025, wapigakura hao—Johary Kabourou, Loum Mwitu, Pendo Kombolela na Luma Akilimali, wanaiomba mahakama itamke kuwa uchaguzi wa ubunge Jimbo la Kigoma Mjini ni batili.
Wanaomba mahakama itamke msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo na wasaidizi wake wachukuliwe hatua za kinidhamu na kisheria kwa kuvuruga kwa makusudi mchakato wa uchaguzi kwa kuzingatia matakwa ya sheria.
Halikadhalika, wanaomba kufanyika uchunguzi wa kura kuthibitisha kuwa Baba Levo hakuwa mgombea aliyepata kura nyingi katika jimbo la Kigoma, na hivyo hakustahili kutangazwa kuwa mshindi, na uteuzi wake haukuwa halali.
Mbali na ombi hilo, wanaiomba mahakama itamuru kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa ubunge katika jimbo hilo, kulipa fidia ya gharama za kufungua na kuendesha kesi hiyo, pamoja na kugharamia mashahidi wa kesi hiyo.
Wanaiomba pia itoe tamko kwamba walalamikaji wamepatiwa msaada wa kisheria kutoka Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS) na wana mamlaka ya kisheria ya kufungua shauri bila kupitia mchakato wa kuweka dhamana ya uchaguzi.
Sababu za kufungua shauri
Kulingana na nyaraka zilizowasilishwa kortini, walalamikaji wanadai kuathiriwa kwa matokeo ya uchaguzi, kunatokana na kutozingatiwa kwa masharti ya sheria ya uchaguzi ya mwaka 2024 yaliyofanywa na msimamizi.
Kuhusu kutozingatiwa kwa masharti ya sheria ya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani ya mwaka 2024, walalamikaji wameorodhesha vitendo 13 vinavyodaiwa kufanyika na kuathiri uhalali wa uchaguzi wa mbunge wa Kigoma Mjini.
Wanadai kuwa mawakala wa ACT Wazalendo karibu vituo vyote walizuiwa kushiriki bila kuzingatia matakwa ya sheria, kuingia na Daftari la wapigakura ili kujiridhisha ikiwa inaruhusiwa kisheria, na waliondolewa vituoni, wengine wakakamatwa na Polisi.
Mbali na malalamiko hayo, wanadai mawakala walinyimwa nakala za matokeo, kulazimishwa kusaini fomu za matokeo kabla ya zoezi la kuhesabu kura.
Wanadai pia kuruhusiwa kwa upigaji holela wa kura usiozingatia sheria, taratibu na kanuni, ikiwa ni pamoja na mtu mmoja kupiga kura zaidi ya moja kwenye sanduku, na karatasi za kura kuchanwa kabla ya mpigakura kuingia kituoni.
Pia wanadai kuliruhusiwa upigaji holela wa kura usiozingatia sheria, taratibu na Kanuni ikiwa ni pamoja na kuurhusu mtu mmoja kuingia na vitambulisho zaidi ya kimoja akisema anawapigia kura watu wasio na uwezo wa kupiga kura na
Halikadhalika kuliruhusiwa upigaji holela wa kura usiozingatia sheria, taratibu na Kanuni ikiwa ni pamoja na kuruhusu watu kupiga kura bila kuzingatia taarifa zao katika kituo kama ni wapiga kura halali wa kituo alichoenda kupiga kura.
Wanalalamikia kufanyika kwa majumuisho ya kura ya siri bila kumjulisha mgombea wa ACT Wazalendo wala mawakala wake na kutobandika matokeo ya uchaguzi wa ngazi ya jimbo katika mbao za matangazo kama sheria inavyotaka.
Pia wanadai watu waliruhusiwa kuendelea kuingia kupiga kura kutoka nje zaidi ya saa 10:00 jioni bila ya kuwa wamepanga mstari ikiwemo katika Kituo cha Shule ya Msingi Kabingo Kata ya Gungu, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Wanalalamikia pia kuwa mawakala walitishwa kwamba hawapaswi kuhoji chochote wanachoona au kinachoendelea ndani ya vituo na na kulikuwa ujazaji wa fomu ya matokeo wenye kasoro na usiofuata taratibu kwenye kata.
Walalamikaji pia wanadai kutumika hoja za udini katika kampeni za uchaguzi, zinazodaiwa kufanywa moja kwa moja na Baba Levo.
kuwa Septemba 23,2025, Baba Levo katika mikutano yake ya kampeni alitamka kuwa “Dalali anashtaki Baba Levo anatoa rushwa anachangia madrasa, yeye ni Muislamu kwanini hachangii.”
Wanadai kauli hiyo ililenga kumchonganisha mgombea wa ACT Wazalendo na waumini wa dini ya Kiislamu kwamba Zitto hafai kuchaguliwa sababu haguswi katika kutoa michango kwenye shughuli za kiislamu.
Baba Levo anadaiwa alitumia lugha yenye lengo la kuharibu taswira na utu dhidi ya Zitto ambapo Septemba 24 na 25, 2025 akiwa jukwaani alitamka Zitto sio Mwami tena ni Mwamini na ndiyo jina analopaswa kuitwa, pia akamuita Dalali.
Pia September 9, 2025 mgombea wa CCM (Baba Levo) anadaiwa alitamka jukwaani kwamba; “mimi mke wangu huyu hapa. Dalali amewahi mtambulisha mke wake? Hawezi sababu ana wanawake kila kona si watagombana”.
Wanadai Baba Levo wakati wa mchakato wa kugombea na wakati wa kampeni, alishiriki yeye mwenyewe na pia kupitia viongozi na watu wake wa kampeni na kwa ufahamu wake na ridhaa na idhini yake katika vitendo vya rushwa.
Walalamikaji wanadai kwamba kati ya Septemba 25 na 26, 2025, Baba Levo akiwa jukwaani katika mkutano mkubwa wa kampeni kata ya Kibirizi, alitoa Sh1 milioni na kumpa mwanamke aliyetambulika kwa jina la Mwantum kama mtaji wa biashara.
Katika hati ya shauri hilo la uchaguzi, walalamikaji wameorodhesha matukio mbalimbali ambayo wao wanayatafsiri kama ni rushwa ikiwamo kutoa Sh2 milioni kwa Kanisa la Morovian Kigoma Septemba 20, 2025 kwa ajili ya ujenzi wa kanisa.
Kwamba Oktoba 27, 2025 katika ufungaji wa kampeni za Baba Levo, mshiriki wake aliyekuwa anamnadi na kumpigia kampeni ambaye ni Naseeb Abdul (Diamond Platnumz) aligawia fedha wananchi akiwa jukwaani na mgombea huyo.
Wanadai msanii anayefahamika kwa jina la Zuchu wakati anawasili Kigoma kwa shughuli za kampeni akiwa ameambata na Baba Levo, alitoa fedha kwa wapigakura wa jimbo hilo kwa nia ya kushawishi kuungwa mkono kwa Baba Levo.
Walalamikaji wanadai kuingizwa kwenye masunduku ya kupigia kura katika baadhi ya vituo, kura feki, kura zisizo halali na kura zilizopigwa bila kufuata utaratibu kwa lengo la kumnufaisha na zilizomnufaisha mlalamikiwa wa pili, Baba Levo.
Wanadai kuingizwa kwa kura feki na zisizo halali katika kata karibu zote, ikiwemo za Machinjioni, Kasingirima, Kitongoni, Gungu, Kibirizi, Buzebazeba, Kipampa, Mwanga Kaskazini, Kagera na Ruguba, na kumpa ushindi Baba Levo.
Kwamba kwenye baadhi ya vituo, Zitto Zuberi Kabwe wa ACT Wazalendo alishinda, lakini matokeo yaliebadilishwa na kuwekwa yasiyo na uhalisia.
Walalamikaji katika shauri hilo pia wanalalamika kuwa Baba Levo wakati wa mchakato wa kugombea na wakati wa kampeni, alishiriki yeye mwenyewe na watu wake wa kampeni, kwa ufahamu na idini yake, katika vitendo haramu.
Katika matendo hayo haramu, wanadai Baba Levo na watu wake walichana mabango na picha za wagombea wenzake ikiwa ni pamoja na za Zitto Kabwe.
Pia wanadai kufanya fujo na kutenda matendo ya jinai kulikofanywa na Baba Levo na mawakala wake ikiwa ni pamoja na kupiga wapigakura na mawakala, kutoa lugha chafu na matusi na kutishia watu na bastola.
Lakini wanadai siku ya uchaguzi, Baba Levo au kwa kupitia wapambe wake, aliongoza operesheni ya kuteka na kukamata wapigakura, wanachama wa ACT wazalendo kwa lengo la kuwatia hofu na woga ili wasijitokeze kupiga kura.