BAO la dakika 16 la Mganda Peter Lwasa limeiwezesha Pamba Jiji kupata ushindi wa tatu katika Ligi Kuu Bara na kukwea hadi kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo ikifikisha pointi 12 kupitia mechi saba.
Pamba ilipata ushindi huo mbele ya Fountain Gate kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini hapa ukiwa ni mechi pekee iliyopigwa leo Jumapili kwa ligi hiyo inayozidi kushika kasi nchini.
Matokeo hayo yameifanya Pamba kuchupa kutoka nafasi ya tano hadi kileleni ikiing’oa Mashujaa iliyokwea hapo juzi baada ya kuitungua Mbeya City kwa bao 1-0.
Wenyeji waliotoka kulazimishwa sare ya 1-1 na Singida Black Stars katika mechi iliyopita uwanjani hapo, ilianza pambano hilo kwa kasi ikiwa na lengo la kutoka na pointi tatu nyumbani, japo Fountain nayo ilijitutumua na kujibu mashambulizi.
Hata hivyo, dakika ya 16 kombinesheni mzuri baina ya Mkenya Mathew Momanyi na Lwasa raia wa Uganda iliisaidia Pamba kupata bao ambalo lilidumu hadi mapumziko, licha ya Fountain kupambana kutaka kulirudisha.
Kipindi cha pili timu zote zilifanya mabadiliko kadhaa ya wachezaji na kuongeza kazi ya mechi hiyo, lakini bado haikuweza kubadilisha matokeo kwani Pamba ilitoka wababe na ushindi wa 1-0.
Pamoja na kupoteza mechi hiyo, Fountain italaumu safu ya ushambuliaji kwa kushindwa kutumia nafasi ilizotengeneza katika dakika zote 90 na kuwafanya wenyeji kushindwa kupumua licha ya kuongoza kwa bao kwa muda mrefu.
Bao la Lwasa ni la tatu kwake msimu huu na kumfanya sasa alingane na nyota wawili wa JKT Tanzania, Saleh Karabaka na Paul Peter waliofunga pia idadi hiyo ya mabao katika Ligi hiyo iliyofikisha jumla ya mechi 44 tangu ilipoanza rasmi Septemba 17 mwaka huu.
Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea tena keshokutwa Jumatano kwa mechi moja tu itakayozikutanisha KMC na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa KMC Complex, huku kila moja ikitoka kupoteza mechi ya mwisho, wenyeji wakicharazwa 1-0 n JKT Tanzania na Mtibwa kufungwa 2-0 na Yanga.