Dar es Salaam. Kamati ya Uongozi ya Chama cha ACT – Wazalendo, imejifungia kwa siku moja visiwani Zanzibar, kujadili masuala mbalimbali ikiwamo ya tathmini ya hali ya kisiasa baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29,2025.
Mwananchi leo Jumapili Novemba 23, 2025 imedokezwa kuwa, huenda kikao kikajadili na kutoa uamuzi wa chama hicho kuingia au kutoingia katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) ambayo ipo kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, iliyofanyiwa maboresho mwaka 2010.
Kikao cha kamati ya uongozi ni cha kwanza kufanyika tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu na kuongozwa na Dorothy Semu ( kiongozi wa chama) pamoja na wajumbe waandamizi akiwamo Zitto Kabwe, Othman Masoud (mwenyekiti wa chama) na Ado Shaibu (katibu mkuu).
Katika kikao hicho kilichofanyika katika ofisi ndogo za makao makuu ya ACT – Wazalendo, Vuga Mjini Unguja, chama hicho kimetoa picha zinazowaonesha viongozi wao wakiendelea na kikao hicho bila kueleza kwa kina ajenda za kikao hicho.
Kwa kawaida kamati ya uongozi huwa na vikao vinavyotoa uamuzi kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu mwenendo wa chama hicho.
Kufanyika kwa kikao hicho, kumetanguliwa mfululizo wa matukio mbalimbali yakiwamo ya mwanasheria mkuu wa chama hicho, Omar Said Shabaan kutangaza kuwa ACT – Wazalendo itafungua mashauri 25 katika Mahakama Kuu ya Zanzibar kupinga matokeo ya uchaguzi ya uwakilishi na ubunge.
Kesi hizo zinahusisha majimbo ya uchaguzi 25 kati ya 50 yaliyopo Pemba na Unguja.
Katika uchaguzi huo, ACT- Wazalendo ilishinda majimbo 10 huku Chama cha Mapinduzi (CCM) ikishinda majimbo 40 kati ya 50 yaliyopo Zanzibar.
Tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu, Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman amekuwa na mfululizo wa ziara za kuzungumza na wanachama na viongozi wa chama hicho Pemba na Unguja, kujadili yaliyojiri siku ya uchaguzi mkuu.
Kwa nyakati tofauti Othman amekuwa akieleza wazi kutokubaliana na matokeo ya uchaguzi huo, hata hivyo amewataka wanachama kuwa watulivu katika kipindi hiki, akisisitiza chama hakitafanya uamuzi wa kujiunga na SUK bila kuwashirikisha.
Othman alisema ACT – Wazalendo, itaendelea kusimama kudai uchaguzi huru, haki na ushirikishwaji wa kweli wa wananchi katika uamuzi unaohusu mustakabali wa Taifa.
Katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025 ulioshindaniwa na wagombea 11 wa kiti cha urais, Dk Hussein Mwinyi wa CCM alishinda kwa kura 448,892 sawa asilimia 74.8 akifuatiwa na Othman aliyepata kura 139,399 sawa na asilimia 23.22.
Novemba 13, 2025 akihitimisha ziara yake Pemba, Othuman alifichua namna ACT – Wazalendo walivyoandikiwa barua na Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Zena Said inayowataka kupeleka jina la Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.
Akizungumzia hilo, Othuman alisema hawajapeleka jina hilo hadi sasa, kwa madai ya kutoridhika na mazingira ya kisiasa yaliyopo visiwani humo.
Hata hivyo, siku hiyo hiyo, Rais Mwinyi alitangaza baraza lake la mawaziri huku akiacha nafasi za wizara nne, zikiwa ni maalumu kwa ajili ya ACT-Wazalendo ambacho ndio chama cha upinzani visiwani humo.
Wizara hizo ni Utalii na Mambo ya Kale, Afya, Biashara na Maendeleo ya Viwanda na Wizara ya Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Zanzibar.
Dk Mwinyi alisema nafasi hizo zitakuwa wazi kwa siku 90 kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar na kama ACT-Wazalendo hawatapeleka majina, atateua kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya siasa, wamesema uwepo wa kikao cha kamati ya uongozi chenye wajumbe zaidi 10, unaongeza joto la kupata ufumbuzi wa ACT-Wazalendo kuingia au kutoingia SUK.
Inaelezwa kuwa, kauli za Dk Mwinyi za hivi karibuni zinaongeza chachu kwa viongozi wa chama hicho kufanya uamuzi chanya kuhusu SUK, ikizingatiwa Othman ameshafanya ziara ya kusikiliza wanachama kuhusu yaliyojiri.
Novemba 10, 2025 akizindua Baraza la Wawakilishi, Dk Mwinyi alisema yupo tayari kutekeleza maridhiano na kuunda SUK.
“Nitaheshimu maridhiano na nipo tayari kuyatekeleza na kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984,” alisema Dk Mwinyi.