Dar es Salaam. Wakati Rais Samia Suluhu Hassan akiizindua tume aliyoiunda kuchunguza yaliyofanyika wakati wa uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, wadau wamependekeza maeneo mengine muhimu ambayo wangependa tume hiyo iyaangazie kwenye uchunguzi huo.
Rais Samia aliunda tume hiyo Novemba 17, 2025 kwa ajili ya kuchunguza mambo yaliyosababisha vurugu zilizotokea siku ya uchaguzi, huku akiwataka kuchunguza kiini hasa cha vurugu kwenye maandamano ya vijana na haki wanazozitaka.
Licha ya Rais Samia kuwapatia vidokezo vyake, alieleza kwamba tume hiyo itapatiwa hadidu za rejea zitakazowaongoza kutekeleza majukumu yao katika kuchunguza jambo hilo kwa lengo la kutafuta suluhisho la kudumu.
Kwa mujibu wa Rais Samia, mapendekezo ya tume hiyo inayoongozwa na Jaji mstaafu, Mohamed Chande Othman, yatatumika kama ajenda kwenye Tume ya Maridhiano atakayoiunda baadaye kama alivyoahidi wakati wa kampeni.
Wakati tume hiyo ikianza kazi baada ya kuzinduliwa, wadau mbalimbali wamependekeza kuwa mbali na hadidu za rejea walizopewa, tume hiyo ifanyie kazi mambo muhimu ili kulitoa taifa hapa lilipo.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa George Kahangwa amesema tume ichunguze mauaji, ijue ni watu wangapi wameuawa, nani amewaua, nani aliyeagiza wauawe.
“Baada ya kuwa wameuawa, wamepewa heshima ya kiutu ya kuzikwa kwa heshima au miili imetupwa? Hilo moja peke yake linaweza kula muda mwingi wa tume, lakini ni jambo muhimu kabla ya mengine.
“Litahusisha kama walioua wanapaswa kufikishwa mbele ya vyombo vya haki au la. Kwa hiyo, yote tunayoyasikia kuhusu makaburi ya Kondo na mengine mengi, yachunguzwe,” amesema mwanazuoni huyo.
Profesa Kahangwa ametaja jambo jingine kuwa ni tume kuchunguza namna utekaji ulivyokuwa na nafasi kwenye maandamano ya Oktoba 29, mwaka huu. Amesema kabla ya uchaguzi, masuala ya utekaji yalikuwa yakilalamikiwa na wananchi kuhusu ndugu zao kutekwa.
“Wale waliopaza sauti zao wakatekwa, wako wapi? Nani aliyewateka? Kwa hiyo tume ishughulikie suala hili. Pia kuna suala lingine la watu wasiojulikana,” amesema.
Jambo la tatu, amesema tume ichunguze mfumo wa uchaguzi, namna ulivyo, iwe kwa kuchezewa au kama ulivyo. Amesema mfumo wa uchaguzi umekuwa ukilalamikiwa hata kabla ya uchaguzi wenyewe.
“Kwa vyovyote vile, suala la uchaguzi linalazimika kuwepo kwenye hadidu za rejea…tunaweza kurudi nyuma hadi mwaka 2020, hayo yote ndiyo yametupeleka kwenye shida ya uchaguzi wa 2025,” amesema.
Ameongeza kuwa mambo hayo matatu ya mauaji, utekaji na uchaguzi yakichunguzwa vizuri, yatatengeneza njia ya kwenda kwenye maridhiano au hoja zitakazolitoa taifa kwenye mkwamo.
Kwa upande wake, mchambuzi wa siasa, Hamduny Marcel amesema ni muhimu kwa tume hiyo kurejea kwenye maadili ya viongozi wa umma ili kubaini namna walivyochochea hasira za umma kutokana na mali wanazozimiliki.
“Moja ya kelele zinazopigwa ni kwamba viongozi wanamiliki mali nyingi. Kama mnakumbuka vizuri, hili ni miongoni mwa mambo yanayopigiwa sana kelele. Labda ni uongo, lakini uongo usipojibiwa, unapojirudiarudia, huonekana ni kweli.
“Siku ya uchaguzi, vituo vya mafuta vilichomwa, wakihusisha na kiongozi fulani. Mtu kuwa na mali si kosa, lakini kama mali hizo hazijapatikana kihalali na pengine wingi wa mali ukapitiliza mapato anayoyapata, lazima utie shaka,” amesema Marcel.
Ameongeza kuwa tume hiyo ichunguze namna Katiba ilivyosababisha ombwe hadi kutokea kwa vurugu siku ya uchaguzi. Pia, ameitaka ichunguze kauli za viongozi zilivyochochea vurugu hizo, kwani baadhi yao nao ni sehemu ya waliosababisha.
“Nidhamu ya matamshi, kutamka bila mipaka, hili ni jambo ambalo halikubaliki hata kidogo. Siyo watu wa upinzani tu, wakati mwingine hawa watu wa chama tawala huwa wanatamka maneno unasema, yanatoka wapi? Na hayachukuliwi hatua. Ni hatari kwa umoja wa taifa letu,” amesema.
Mkazi wa Tabata, Dar es Salaam, Haroun Ismail ameikumbusha tume kuchunguza namna tatizo la ajira lilivyokuwa chanzo kwa vijana wengi kuingia barabarani siku ya uchaguzi, jambo lililosababisha wengi wao kujeruhiwa au kupoteza maisha.
“Vijana wengi walioingia barabarani hawana ajira, wana hasira na maisha yao kwani wanaona kama wametelekezwa. Nadhani tume ichunguze jambo hili kwa kina ili kujua tatizo la ajira ni kubwa kiasi gani na nini kifanyike kuwainua vijana hawa,” amesema.