Wazembe wafukuzwe, wasihamishwe | Mwananchi

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba ametaka mfanyakazi yeyote wa umma atakayebainika kuwa mzembe au mla rushwa asihamishwe, bali afukuzwe kazi moja kwa moja.

Mtendaji Mkuu huyo wa Serikali ametoa kauli hiyo leo, Jumatatu Novemba 24, 2025 alipozungumza baada ya ziara ya kutembelea miundombinu iliyoathiriwa na vurugu za Oktoba 29.

Amesema hakuna sababu ya mtumishi wa umma anayekosea kuhamishwa kituo cha kazi, ilhali Tanzania ina vijana wa kutosha watakaoweza kufanya kazi kwa uadilifu.

“Kama zamani tulikuwa tunahamishahamisha enzi hizo hatukuwa na watu wa kutosha, sasa hivi vijana tunao wengi.

“Ambaye anafanya kazi vizuri mpeni sifa zake, lakini wazembe wavivu wala rushwa asihamishwe asiharibu wilaya hii akapelekwa nyingine, mfukuzeni,” amesema.

Kuhusu vurugu za Oktoba 29

Ametumia jukwaa hilo, kutoa pole kwa walioathiriwa na tukio la vurugu za Oktoba 29 mwaka huu, akisema kuna madhara ya upotevu wa maisha na kati yao wapo ambao hawakuhusika, lakini walifariki dunia.

“Kwenye imani yangu damu ya mtu asiye na hatia kumwagika sio baraka. Hili jambo lituelekeze Watanzania tuangalie upya hatua zetu tunazochukua,” amesema.

Amesema ndio maana kwa ukubwa wa jambo hilo, Rais Samia ameunda tume na kwamba Watanzania wanapaswa kuiunga mkono.

“Tumuunge mkono Rais Samia kwenye tume hii, tuwaunge mkono wajumbe wa tume tuwape ushirikiano ili jambo hili liweze kutupa undani wa tukio hili na tujue hatua stahiki za kuchukua,” amesema.

Tume hiyo, imezinduliwa Novemba 20, 2025 ikipewa majukumu ya kuchunguza sababu ya maandamano, idadi ya waliopoteza maisha, madai ya waandamanaji kulipwa na kauli za viongozi wa vyama vya siasa. Kazi hiyo imetakiwa kuikamilisha ndani ya miezi mitatu.

Wajumbe katika tume hiyo ni, Jaji mstaafu, Mohamed Chande Othman (Mwenyekiti), Balozi Ombeni Sefue, Dk Stergomena Tax, Jaji mstaafu Profesa Ibrahim Juma na Balozi Radhia Msuya.

Wengine ni Balozi Paul Meela, Mkuu wa Jeshi la Polisi mstaafu, Said Mwema na Balozi David Kapya.

Mtendaji mkuu huyo wa Serikali, amesema tukio kama hilo linaweza kuhusishwa na sababu ndogo za kiuchaguzi na nyinginezo, lakini kwa undani linahitaji umakini.

“Tanzania si mali ya Serikali wala sio mali ya vyama vya siasa, vipo kwa sababu kuna nchi inaitwa Tanzania.

“Tanzania ni mali yenu Watanzania, nimefuatilia tukio na nimefuatilia hapa nilipopita ni vigumu kuamini kwamba haya yametokea nchini kwetu na baadhi ya watu wanachukulia kwa udogo,” amesema.