Mbeya. Serikali imetoa zaidi ya Sh2.8 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya soko la kisasa la ndizi katika Kijiji cha Mpandapanda, wilayani Rungwe, Mkoa wa Mbeya.
Ujenzi huo utajumuisha jengo la baridi la kuhifadhia mazao, maegesho ya magari, migahawa, ofisi, na eneo la huduma za kifedha, lengo likiwa ni kurahisisha biashara na kuhifadhi mazao kwa usalama.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatatu, Novemba 24, 2025, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Rungwe, Renatus Mchau amesema mradi huu utakuwa suluhisho la wakulima kuuza zao la ndizi na kulihifadhi kwa usalama.
Mkurugenzi halmashauri ya Rungwe Renatus Mchau akisaini mkataba wa kuanza ujenzi wa Soko la kisasa la ndizi.
Mchau pia amesema kuwa Halmashauri imesaini mkataba na Kampuni ya Kagwa General Supplies Limited kutoka Mkoa wa Singida itakayolijenga soko hilo, na ujenzi unatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miaka miwili.
Ameitaka kampuni hiyo kutekeleza mradi ndani ya muda wa mkataba ili wananchi waweze kufurahia uwekezaji wa Serikali ya Awamu ya Sita.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Emmanuel Madafa, amesema mradi huo utajengwa kwa muda uliowekwa ili kuhamasisha na kuchochea shughuli za kiuchumi katika eneo hilo.
“Mradi wa soko la kisasa la ndizi utatumia kipindi cha miaka miwili, lakini niwahakikishie tunaukamilisha ndani ya muda husika na kuukabidhi rasmi,” amesema Madafa.
Kaimu Mkurugenzi wa Kampuni ya Kagwa General Supplies Limited, Emmanuel Madafa akisaini mkataba wa kuanza ujenzi wa mradi wa ujenzi wa soko la ndizi katika kijiji cha Mpandapanda Wilaya ya Rungwe mkoani hapa.
Kwa upande wake mkulima wa ndizi wa Kata ya Kiwira, Atupele Mwakyusa, amesema ujio wa mradi huo utawaondolea wakulima adha ya kufanya biashara katika maeneo yasiyo salama, hususan pembezoni mwa hifadhi za miundombinu ya barabara.