Simiyu. Kwa miaka mingi, wanafunzi wanaochukua masomo ya sayansi wamekuwa wakikumbwa na changamoto za miundombinu, uhaba wa walimu wenye utaalamu na mazingira yasiyo rafiki kwa kujifunzia.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Rais Samia Suluhu Hassan alipolizindua Bunge la 13 Novemba 14, 2025, Serikali imepanga kuanza maboresho yanayolenga elimu inayojikita katika ujuzi, hususan kwenye masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM).
Rais Samia alisema dhamira ya Serikali ni kuongeza idadi ya wanasayansi wabobezi katika maeneo ya sayansi ya data, akili unde, sayansi ya kompyuta na teknolojia za viwanda.
“Tutatumia Mfuko wa Samia Scholarship kusomesha wanasayansi hawa ndani na nje ya nchi. Hatua hii itaenda sambamba na kukamilisha shule maalum za sekondari za wasichana wa sayansi na shule za vipaji za wavulana katika kila mkoa,” alisema.
Wadau wa elimu waliozungumza na gazeti hili wanasema kukamilika kwa ujenzi wa shule maalum za wasichana wa sayansi na shule za vipaji kwa wavulana, kutafungua fursa mpya za kulea kizazi cha wataalamu, wavumbuzi na wanasayansi.
Mwalimu Godwin Kitonka anasema hatua hiyo ni ishara ya dhamira ya Serikali kuongeza ushiriki wa wasichana katika masomo ya sayansi yaliyotawaliwa na wanaume kwa muda mrefu.
“Kwa miaka mingi wasichana wamekosa mazingira rafiki ya kukuza vipaji vyao kwenye masomo ya sayansi. Kujengwa kwa shule hizi kutawajengea kujiamini, kuondoa vikwazo vya kimazingira na kijamii, na hatimaye kuongeza idadi ya wataalamu wanawake nchini,” anasema.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Profesa Michael Mwasenga, anasema shule za vipaji maalum kwa wavulana, zitachochea ubunifu na kuwaandaa vijana kushindana kimataifa katika masuala ya teknolojia na uvumbuzi.
“Dunia ya leo inahitaji vijana wabunifu katika uhandisi, kompyuta, fizikia, hisabati na sayansi nyingine za msingi. Shule hizi zitakuza kizazi kipya cha wavumbuzi watakaoisukuma Tanzania kutoka uchumi wa kawaida kuelekea uchumi wa ushindani wa kimataifa,” anasema Profesa Mwasenga.
Aidha, baadhi ya wadau wametoa rai ya kuweka mizani kati ya uwekezaji katika shule maalum na uboreshaji wa shule za kawaida, hususan shule za kata zinazobeba sehemu kubwa ya wanafunzi.
Mkurugenzi wa Shirika la Elimu kwa Wote Mkoa wa Simiyu, Zainabu Mrope, anasisitiza kutowasahau wanafunzi wanaosoma katika mazingira yenye changamoto.
“Mpango huu ni mzuri na wa kupongezwa, lakini tusisahau shule za kata. Tukizingatia shule maalum pekee, tunaweza kuwaacha nyuma watoto wengi wenye vipaji lakini wasiopata nafasi. Serikali iendelee kuboresha shule zote bila ubaguzi,” anasema.
Naye Ofisa Elimu – Takwimu na Vifaa wa Wilaya ya Maswa, Bakari Geoge, anasema ujenzi wa shule maalum utapunguza msongamano katika shule za kawaida ambazo mara nyingi hukabiliwa na maabara zisizo na vifaa vya kutosha.
“Uwekezaji huu utakuza nidhamu ya kitaaluma na kuboresha mazingira ya ujifunzaji,” anaeleza.
Anaongeza kuwa Serikali imekamilisha hatua kubwa za ujenzi wa miundombinu katika shule hizo, ikiwa ni pamoja na mabweni, maabara, madarasa ya kisasa, maktaba, maeneo ya Tehama na majengo ya utawala.
“Kama utekelezaji utaendelea kwa kasi hii, Tanzania itakuwa katika nafasi nzuri ya kuandaa rasilimali watu bora kwa maendeleo ya Taifa,” anasema.
Mchambuzi wa masuala ya elimu, Nicholaus Machunda, anasema mradi huo unaweza kuinua ufaulu katika masomo ya sayansi, iwapo utaambatana na upatikanaji wa vifaa vya kisasa, walimu waliobobea na programu za ushauri kwa wanafunzi.
“Mpango huu unapaswa kuendana na kampeni ya kuwahamasisha wazazi kuwaunga mkono watoto wao hususan wasichana kuchagua masomo ya sayansi bila kuogopa dhana kwamba masomo haya ni magumu au hayawafai,” anasema.
Mkazi wa Bariadi, Masunga Chenya, anasema matarajio ya wazazi yameongezeka zaidi kufuatia msimamo wa Serikali kuboresha elimu ya sayansi.
“Katika familia yangu nina watoto wawili wanaopenda sana masomo ya sayansi, lakini mazingira ya shule yao ya kata si rafiki. Shule hizi maalum zitawasaidia kufikia uwezo wao halisi. Hii ni fursa muhimu kwa familia nyingi nchini,” anaeleza.