Bahari inapomeza historia ya wakazi wa pwani -1

Tanga/Pemba. Kwa wenyeji wa Pangani, simulizi ya Kisiwa cha Maziwe ni kama vile taswira ya dunia inayobadilika mbele ya macho yao.

Miaka michache nyuma, Maziwe kilikuwa kisiwa chenye mandhari nzuri ya miti mikubwa iliyotoa kivuli, vibanda vya wavuvi vilikuwa vingi na kasa wakikitumia kutaga kwa wingi.

Leo hii mandhari ni tofauti, Maziwe si tena ile ya awali, imebaki kuwa fungu la mchanga linalozidi kusukumwa na mawimbi kwenye Bahari ya Hindi.

Mtoo Bin Mzee, maarufu Mzee Osama, mwenye umri wa miaka 89 ni miongoni mwa mashahidi wenye kumbukumbu ya kuibuka na kuzama kwa historia kisiwani hapa.

Anasimulia jinsi eneo la Ushongo lilivyokuwa na soko na vibanda vya wafanyabiashara kabla bahari haijayafagia hayo yote.


“Nyumba na minazi yote imemezwa na bahari,” anasema kwa sauti ya majonzi, akiongeza kuwa sasa hata mabaki ya kisiwa hayapo tena.

Kwa Juma Idd Hassan, maarufu Fundi Ten, mabadiliko haya hayakuja ghafla. Anakumbuka yalianza taratibu miaka ya 1970, kisha yakashika kasi 1980.

“Eneo la mita 300 lilikuwa na mivinje, lakini sasa limezama kabisa. Kama hatua zingechukuliwa wakati huo, huenda Kisiwa cha Maziwe kisingepotea,” anasema.

Anaelekeza macho yake Barabara ya Pangani iliyo umbali mfupi wa takribani kilomita moja kutoka bahari, akihofia siku ambayo mawimbi yataivamia.

“Kama Serikali haitachukua hatua ikiwamo kujenga ukuta wa kuzuia maji, muda si mrefu yatafika hadi Tanga Deco (jirani na barabara),” anasema.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Ushongo, Mwingia Mgaza, kwake kupotea kwa Kisiwa cha Maziwe si habari tu ya historia, bali ni pigo kwa mazingira na maisha.

Kasa waliokuwa wakitaga kwa wingi eneo hilo sasa hawapo na hata fungu la mchanga lililosalia linaendelea kupungua, anaeleza.

“Miaka ya 1978 hadi 1980, kasa walikuwa wanatagia pale Maziwe. Kadri miaka ilivyopita, kisiwa kiliendelea kuliwa kidogo kidogo hadi kimepotea kabisa,” anasema.

Anasema vijiji vya pwani kama vile Ushongo navyo vimeanza kuvamiwa na maji.

“Zamani pwani ilikuwa umbali wa mita 30 hadi 40 kutoka makazi, lakini sasa nyumba zipo ufukweni. Makaburi ya wazee wetu nayo yameshachukuliwa na bahari,” anasema.

Anasema kijiji kiliamua kushirikiana na Serikali kupitia kundi la Friends of Maziwe kulinda eneo hilo, kwa kupata msaada wa mafuta, posho na huduma ndogo za kijamii kwa walinzi wa mazingira.

Wananchi wakivuka katika eneo ambalo zamani ilikua nchi kavu, kwa sasa maji ya bahari yanafioka maeneo hayo, Pangani, mkoani Tanga.



Mashamba yaathiriwa Panza

Katika Kisiwa cha Panza, kilicho Kusini mwa Pemba, Zanzibar, simulizi ni ileile – kina cha maji kuongezeka, ardhi kupungua na maisha kubadilika.

Michirizi ya chumvi kwenye mashamba yanayoendelea kulimwa ni ushahidi wa uharibifu unaoendelea kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Kisiwa cha Panza ni miongoni mwa visiwa vidogo ambavyo watu wanaishi Kusini mwa Mji wa Pemba.

Licha ya kuwa na misitu ya mikoko, shughuli za kilimo na makazi, kisiwa hiki kimeanza kupoteza ardhi kutokana na kupanda kwa kina cha maji ya bahari.

Sheha Faki Makameanatazama mashamba ya Ndibani na Pungua kwa huzuni akisema: “Yote yamegeuka majangwa,”

Maji ya chumvi hayaruhusu kitu chema kuota na kila msimu nyumba nyingine huingia eneo la hatari.

“Baadhi ya nyumba ziko hatarini kufikiwa na maji, hasa kipindi cha maji kujaa. Mashamba ya eneo la Ndibani na Pungua hayatumiki tena kwa kilimo,” anasema.

Historia ya kisiwa hicho imeathiriwa, makaburi ya jamii za kale yaliyo karibu na bahari yamefunikwa na maji, huku maandiko kwenye mawe ya makaburi yakiwa bado yanaonekana.

Ali Mohamed Abdulla, yeye kumbukumbu za utotoni za uwepo wa minazi, migomba, samaki wengi baharini zimebaki kuwa historia.

Mwananchi akiwa pembeni mwa kibao kinachohamasisha upandaji wa miti na kukataza ukataji hovyo wa mikoko katika Pwani ya kisiwa cha Panza, Pemba.



“Zamani kulikuwa na minazi na migomba, leo hakuna kabisa. Maji ya chumvi yameharibu mashamba yote. Hata samaki wadogo na pweza wamepungua, maisha yamekuwa magumu,” anasema.

Ni mtazamo wake kuwa, ongezeko la watu kisiwani humo limechangia uharibifu wa mazingira, kwani miti ya mikoko na matumbawe vimekuwa vikitumika kwa ajili ya ujenzi na kuni, jambo linaloongeza kasi ya mmomonyoko.

Salum Khamis Hamad, mkazi wa Mtaa wa Mjanaza anasema: “Mabadiliko ni makubwa. Chumvi imeongezeka zaidi ya mita 30 kutoka ilipokuwa awali. Mashamba tuliyokuwa tunalima sasa yamezama na makaburi ya zamani yamefukiwa na maji.”

Juma Ali Mati, katibu wa Jumuiya ya Usimamizi na Uendelezaji wa Misitu Inayohifadhiwa Pemba, anaona mzigo mkubwa unaobebwa na kisiwa chenye watu 5,700 ambao wanategemea sana rasilimali zinazozidi kuharibiwa. Wananchi hao wanaojihusisha na uvuvi, kilimo na ufugaji.

Anasema kisiwa hicho kimeathirika kutokana na mabadiliko ya tabianchi na matumizi mabaya ya rasilimali.

“Sisi ni kisiwa, lakini mara nyingi hakuna jitihada za kufuatilia hali ya mazingira. Pia hakuna mradi wa moja kwa moja tunaoupata; tunajitolea kutoa elimu juu ya matumizi endelevu na kupanda miti katika maeneo yaliyoathirika,” anasema.

Anasema ukosefu wa ajira umesababisha wakazi wengi kukata mikoko na kuchoma mawe kwa ajili ya chokaa, jambo linaloongeza uharibifu wa mazingira.

Vilevile, kilimo cha mwani kinachowasaidia wanawake wengi kinachangia uharibifu kwa sababu miti ya mikoko hukatwa kutengeneza vipande vya kupandia.

“Miti ikikatwa, mawimbi makubwa yanapokuja yanavunja kingo na maji ya bahari kuingia juu zaidi,” anaeleza.

Anataja pia uharibifu wa matumbawe unaofanywa na wavuvi wasiofuata kanuni kuwa chanzo kingine cha kupungua kwa samaki.

“Wavuvi wanapovunja matumbawe, samaki wanapoteza mazalia yao na mawimbi yanazidi kuharibu mashamba na makazi,” anasema.

Mati anasema athari hizo zimeanza kuonekana hadi katika shule za sekondari na msingi za Kisiwa cha Panza, ambazo sasa maji ya bahari hufika mara kwa mara.

“Zamani hayakuwa yakifika huko, lakini sasa maji yanafika shuleni,” anasema.

Anasema eneo la Madauni na Ufunguni limeathirika zaidi, ambako takribani mita 200 zilizokuwa ukanda wa juu sasa zimo baharini.

“Mfano halisi ni makaburi ya Madauni ambako watu walikuwa wakizikwa, lakini kutokana na mawimbi makali na upepo, mifupa ya waliozikwa huibuka juu. Tunaikusanya na kuizika tena sehemu za juu zisizofikiwa na maji,” anasema.

Anaeleza eneo la Ufunguni, lililokuwa na mashamba makubwa ya minazi na viazi vitamu, sasa limezama kabisa.

“Tumeanza kupanda miti katika eneo lililobaki ili kupunguza kasi ya mmomonyoko. Takribani mita 200 zimechukuliwa na bahari. Tulipopima mwaka 2012 eneo lote lilikuwa hekta 9.6, lakini sasa limepungua sana,” anasema.

Anaeleza wananchi hawawezi peke yao kuzuia maji, kwani wakizuia sehemu moja maji hupenya upande mwingine, hivyo wanaendelea kutumia njia mbadala kama vile kupanda miti ili kupunguza mmomonyoko, upepo na mawimbi makubwa.

Mati anasema upande wa mashariki wa Kisiwa Panza umejengeka kwa udongo laini unaoendelea kumomonyoka, wakati kusini na magharibi kuna mawe makubwa ambayo hayaathiriwi kwa kiasi kikubwa.

“Mashariki na kaskazini ndiko maji yanapopata njia zaidi ya kupita,” anasema.

Anaiomba Serikali kupitia mamlaka husika iwasaidie kuzuia mmomonyoko huo.

Imeandikwa kwa udhamni wa Taasisi ya Gates Foundation

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.