Dar es Salaam. Waumini wa Kanisa la Ufufuo na Uzima la Askofu Josephat Gwajima wameendelea kumiminika kanisani hapo wakisubiri kukabidhwa ikiwa imepita saa kadhaa tangu Serikali ilipotangaza lifunguliwe jana Novemba 24, 2025.
Leo Novemba 25, Mwananchi ilifika kanisani hapo na kukuta baadhi ya waumini wakiwa kwenye uwanja wa kanisa wakisubiri maelekezo ya viongozi wao ili kuingia ndani ya kanisa hilo ambalo tangu Juni 2, 2025 lilipofungwa na kuzungushiwa utepe huku likiwa chini ya ulinzi wa polisi.
Tangu wakati huo waumini wa kanisa hilo wamekuwa wakifanya ibada katika maeneo tofauti, ikiwamo barabarani nje ya kanisa lao lililopo Kibo, Dar es Salaam na kwenye Kanisa la Kiluthel Afrika Mashariki (KKAM) ambako nako waliondolewa na Jeshi la Polisi kabla kuhamia Ukumbi wa Tanzanite na Kibo Park ambako nako waliondolewa na kuhamia maeneo mengine tofauti tofauti.
Kufunguliwa kwa kanisa lao ni kama kumewapa tumaini jipya waumini hao ambao leo wamekusanyika kanisani hapo wakisubiri kukabidhiwa kanisa lao, zoezi ambalo linatarajiwa kufanyika wakati wowote kuanzia sasa.
Wakiongozwa na mitume na maaskofu wa kanisa hilo, waumini hao wamekuwa na furaha huku wakitania utani wa hapa na pale na salamu ya kanisa hilo ya Majeshi Majeshi na ile ya Utukufu ndizo zimeshamiri, wengine wakisema wanasubiri tu utepe utolewe ili waingie kufanya usafi.
Bado jengo hilo lina utepe hadi mchana saa sita huku polisi wawili wakiwa ndani ya jengo hilo, mmoja akiwa ameshika silaha.