SIKU njema huonekana asubuhi. Hii ipo kwa refa bwa’mdogo kutoka Libya, Zakaria Ibrahim Al-Ghaithy (15) ambaye alikuwa kivutio katika fainali za Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kwa timu za Shule (ASFC 2024) zilizofanyika mjini Unguja, Zanzibar.
Katika fainali hizo zilizomalizika mwishoni mwa mwezi uliopita, Al-Ghaithy alikuwa gumzo kutokana na uwezo wake wa kupuliza kipyenga kwa ustadi na kufanya uamuzi katika staili ya kusisimua.
Sio tu kwa mashabiki waliohudhuria fainali hizo, lakini ubora wa kazi za dogo huyo ziliwakuna hadi wachezaji wenzake, makocha na viongozi sambamba na Rais wa Caf, Dk Patrice Motsepe aliyefurahishwa na misimamo yake wakati wa majukumu yake.
Mwanaspoti limefanya mahojiano na mwamuzi huyo na anabainisha ilikuwa ndoto yake kuchezesha fainali na mechi kubwa Afrika.

“Namshukuru Mungu kwa kutimiza ndoto zangu, nikiwa mwamuzi wa akiba yaani ‘4th official’ katika mchezo wa nusu fainali timu za wasichana kati ya Uganda na Morocco,” anasema na kuongeza;
“Wengi wananishangaa nikiwaambia ni mwanafunzi, hawaamini kutokana na kile ninachokifanya uwanjani, hiyo ni moja ya ndoto zangu ambazo haziwezi kukatishwa na masomo yangu, lazima nisome ili niwe bora zaidi.
“Nilianza kufanya kazi ya uamuzi wa nne nchini Libya na jamii yangu ilikuwa inaonyesha kama hainielewi hivi, baadaye wakaja wakakubali uwezo wangu.

Pamoja na kuipenda kazi hiyo na kuifanya kwa nidhamu, anasema haiwezi kukosekana changamoto, kwani wapo ambao hawakubaliani na anachoamua wakati mwingine, kulingana na muonekano wa mwili wake kuwa mdogo.
“Ukiachana na hilo, nina changamoto ya kiafya, ingawa siwezi kuiweka wazi, licha ya umri wangu kuwa mdogo, hakuna jambo litakalokatisha ndoto zangu, badala yake kila jambo nalichukua kwa upande wa kunijenga.

Anaongeza: “Ipo siku nitakuwa mwamuzi wa kimataifa, ninawaza ndoto kubwa, ndio maana nafanya bidii kwa ukubwa wake, ili kuendana na kile ninachokitamani siku moja kitokee, nikija kuwa mkubwa naamini nitachezesha Kombe la Dunia.”
Mashindano ya Soka ya Shule za Afrika ya CAF ya kuendeleza viongozi wa baadaye wa Afrika, yalianzisha warsha mbalimbali ikiwamo ya Waamuzi Vijana wa CAF na Al-Ghaithy alihitimu pamoja na waamuzi wengine wadogo kutoka mataifa mbalimbali Afrika. Kati ya marefa walioendesha warsha hiyo ni Janny Sikazwe kutoka Zambia.
Kwa upande wake, Sikazwe anasema lengo la kuwafundisha vijana ni kuandaa marefa wazuri kwa siku zijazo, akisisitiza hakuna njia ya mkato zaidi ya kuwapa misingi mizuri.
“Lengo la warsha hii ni kuandaa kizazi kijacho kwa manufaa ya soka la Afrika na dunia kwa jumla, tumefurahi kuona shirikisho la soka linaandaa michuano hiyo kwa watoto na kuweka warsha mbalimbali zikiwemo hizo za kuwajengea uwezo marefa chipukizi,” anasema Sikazwe na kuongeza;

“Soka la Afrika linahitaji vijana waandaliwe wakiwa wadogo ili kuwapa uwezo wa kujiamini zaidi. Nashauri kila nchi ianzishe warsha kama hizi ili tupate marefa wazuri kwa ajili ya michuano mbalimbali ikiwemo kuchezesha Kombe la Dunia.”