Makada sita Chadema waachiwa huru Mbeya, Chadema yatoa kauli

Mbeya. Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mbeya, imewaachia huru watuhumiwa sita ambao ni wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Mbeya waliokuwa wakituhumiwa kwa makosa mawili ya kula njama za kufanya kosa na uhaini.

Uamuzi wa kufuta shauri  la uchunguzi (P.I) 26722/ 2025 umetolewa leo Novemba 25 na Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya, Mtengeti Sangiwa baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) aliyewakilishwa na Wakili wa Serikali, Dominick Mushi kuiambia  mahakama hiyo hana nia tena ya kuendelea na kesi hiyo.

Watuhumiwa wote sita walikuwa wanatuhuma kwa makosa mawili ikiwa ni kula njama ya kufanya kosa kinyume cha sheria ya 384 ya kanuni za adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho ya mwaka 2023 na kosa la pili llilikua ni uhaini kinyume cha kifungu cha 39(2) (d) (2).

Wakili Mushi ameieleza Mahakama kuwa kwa mamlaka aliyonayo Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) chini ya kifungu cha 92(1) cha sheria ya mwenendo wa mashauri ya jinai haona haja kuendelea na kesi hiyo.

Kwa mujibu wa Wakili wa Serikali, Dominick Mushi ameliambia Mahakama kuwa watuhumiwa wote sita walishtakiwa kwa chini ya kifungu cha 92(1) cha sheria ya mwenendo wa mashauri ya janai sura ya 20 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2023 kwa makosa mawili ya kwanza kula njama ya kutenda kosa na pili ni kosa la uhaini.

Baada ya Wakili wa Serikali Dominick Mushi kueleza Mahakama, Hakimu wa Mahakama hiyo, Mtengeti Sangiwa amesema kwa mamlaka aliyonayo chini ya kifungu cha 92(1) cha sheria ya mwenendo wa mashauri ya jinai sura 20  kama ilivyofanyiwa marekebisho ya mwaka 2023 anawachia huru watuhumiwa wote sita.

Wakizungumza nje ya mahakama hiyo, Viongozi wa chadema wamesema mawakili wa chama hicho wamefanya kazi kubwa kuwatoa makada wao wakieleza kuwa bado wanaendelea kupambania haki.

Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa chama hicho Mbeya Mjini, (Bavicha), Hassan Mwamwembe amesema wanaendelea kukipambania chama kwani licha ya kuwachiwa makada hao, huenda wengine wakiendelea kukamatwa.

“Vijana sisi tuendelee kukipambania chama hadi pale itakapopatikana ukombozi, tunashukuru mawakili na chama chetu Taifa kwa kusaidia kuwatoa makada wetu,” amesema Mwamwembe.

 Katibu wa chama hicho Wilaya ya Mbeya Mjini, Joseph Kasambala amesema bado mapambano hayajaisha kwa kuwa wanapigania ukombozi na haki na kwamba hakuna mafanikio yasiyo na maumivu.

“Dunia imejua kilichofanyika na kadri tunavyokwenda tutapata tunachopigania, kuna watu wamekamatwa bila hatia kwakuwa kuna waliokamatwa kabla na wakati wa kupiga kura,” amesema Kasambala.

Akizungumza huku akitokwa na chozi, mmoja wa watuhumiwa walioachiwa huru, Andrew Kasesela amesema wamepitia magumu wanashukuru wananchi waliopambania kuachiwa kwao.

“Zaidi tunamshukuru Mungu kwa kutukinga na yaliyotokea hadi kuachiwa huru, haikuwa kazi nyepesi kwani tumepitia mazito sana,” amesema Kasesela.

Walioachiwa huru ni Andrew Kasesela, Adam Melele, Lusekelo Lugani, Daud Sent, Philemon Sanga na Paul Mwangama, ambao walituhumiwa kufanya makosa hayo kipindi cha Machi 1 hadi Oktoba 27 mwaka huu na watapaswa kuripoti kituo cha polisi.

Baada ya kuachiwa huru, nje ya mahakama hiyo, Askofu wa Kanisa la T. A. G, Kais Mwambona alifanya ibada maalumu kuwaombea watuhumiwa hao, huku wananchi na wafuasi wa Chadema wakishiriki tukio hilo.