Tafiti 41 kuisaidia Serikali majibu ya changamoto za kiuchumi

Mwanza. Serikali inatarajia kunufaika na matokeo ya tafiti 41 za ndani na nje ya nchi zinazolenga kutafuta majibu ya changamoto zinazoikabili uchumi wa Tanzania katika kipindi cha mabadiliko ya kijamii na kiuchumi duniani.

Kwa siku tatu, watafiti na wanataaluma kutoka Tanzania na nchi mbalimbali ikiwemo Lithuania, Eswatini, Afrika Kusini, Uingereza, Urusi na Algeria wanajadili mawasilisho 11 kuhusu ukuaji wa uchumi na mabadiliko ya teknolojia, huku watafiti wa ndani 41 wakiwasilisha tafiti zao.

Baada ya majadiliano, matokeo ya tafiti hizo yatakusanywa na kuchapishwa kwenye kitabu maalumu kitakachowasilishwa serikalini na wadau wengine kama mapendekezo ya kutatua changamoto zilizobainishwa.

Hayo yameelezwa leo Jumanne Novemba 25, 2025 na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Profesa William Pallangyo, katika kongamano la nne la usimamizi wa biashara na maendeleo ya uchumi linalofanyika jijini Mwanza kuanzia Novemba 25 hadi 27.

Kongamano hilo lenye kauli mbiu isemayo: Gunduzi, bunifu na biashara kwa maendeleo ya kiuchumi. limewaleta pamoja watafiti wanaojikita katika masuala ya biashara, teknolojia na ukuaji wa uchumi.

Profesa Pallangyo amesema wasomi wanapaswa kuchochea fikra mpya na kuishauri Serikali kuhusu hatua za kuchukua kukabiliana na changamoto za kiuchumi, hasa katika kipindi hiki ambacho dunia inapitia mabadiliko makubwa ya kiteknolojia.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Prof. William Pallangyo akizungumza leo katika kongamano la nne la usimamizi wa biashara na maendeleo ya uchumi, jijini Mwanza. Picha na Damian Masyenene

“Jumla ya machapisho 41 yatawasilishwa. Baada ya majadiliano, TIA itatengeneza kitabu kitakachopendekeza njia za kutatua changamoto mbalimbali za kiuchumi,” amesema.

Amesema kitabu hicho kitasambazwa serikalini, kwa taasisi za maendeleo na maktaba ili mawazo na mapendekezo ya watafiti yafikiwe na watumiaji halisi.

“Tunawahimiza wadau kuyachukua na kuyaweka katika lugha rahisi inayoweza kueleweka na wananchi,” amesema.

Profesa Pallangyo ameiomba Serikali kuyapokea matokeo ya tafiti hizo na kutoa ushirikiano ili yaweze kuleta manufaa katika sekta za uchumi, teknolojia na maendeleo endelevu.

Akifungua kongamano hilo, Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali, Benjamin Magai, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk Natu El Maamry Mwamba, amesema Serikali inatambua mchango wa watafiti katika kubaini na kutatua changamoto za wananchi.

Amesema Wizara ya Fedha itaendelea kushirikiana na taasisi za utafiti na kuangalia uwezekano wa kuongeza uwekezaji katika utafiti ili kuongeza ushahidi na takwimu zitakazosaidia kupanga sera.

“Nitakuwa balozi wa kuchochea utekelezaji wa mapendekezo ya tafiti. Wizara itaangalia namna ya kutenga fedha zaidi kwa ajili ya utafiti wenye tija,” amesema Magai.

Baadhi ya wanataaluma, watafiti, na wabobezi katika uchumi kutoka ndani na nje ya nchi wakifuatilia mdahalo wakati wakongamano la nne la kimataifa la usimamizi wa biashara na ukuaji wa uchumi ambalo limeandaliwa na Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), jijini Mwanza. Picha na Damian Masyenene

Amesema Serikali inatarajia kongamano hilo kutoa mapendekezo yatakayosaidia kupunguza changamoto katika sekta mbalimbali na kuongeza ufanisi wa kupanga mipango ya kiuchumi.

Kwa upande wake, mmoja wa watafiti wanaowasilisha tafiti hizo, Dk Shukurani Mgaya kutoka TIA Mbeya, amesema utafiti wake umechunguza changamoto zinazowakabili wahitimu wa vyuo vya ufundi stadi (Veta) katika kupata ujuzi unaokidhi mahitaji ya ajira.

Amesema kasi ya mabadiliko ya teknolojia imekuwa ikiathiri uwezo wa wahitimu kuendana na mahitaji ya soko la ajira.

“Tunashauri Serikali kushirikiana na wadau wa ajira ili kuhakikisha wahitimu hawaanzi kujifunza teknolojia kazini, bali wanatoka vyuoni wakiwa wameandaliwa vizuri,” amesema.