Kasoro za ushahidi zamweka huru aliyedaiwa kusafirisha dawa za kulevya

Arusha. Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Dar es Salaam, imemuachia huru raia wa Comoro, Ahmed Abdou, aliyeshtakiwa kwa makosa ya kusafirisha dawa za kulevya.

Mshtakiwa ambaye katika nakala ya hukumu anasomeka pia kwa jina la Ahmed Mohamed, alishtakiwa kwa makosa mawili ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya methylene -dioxy-pyrovalerone (MDPV). Katika kosa la kwanza alisafirisha kilo 4.52 na la pili gramu 103.03.

Hukumu ilitolewa Novemba 20, 2025 na Jaji Sedekia Kisanya na nakala yake ilipakiwa kwenye mtandao wa mahakama.

Kosa la kwanza anadaiwa kutenda Machi 4, 2024, eneo la Posta wilayani Ilala, mkoani Dar es Salaam na la pili Machi 20, 2024.

Jaji Kisanya baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili, amesema mshtakiwa hana hatia kutokana na upande wa Jamhuri kushindwa kuthibitisha mashtaka pasipo kuacha shaka.

Katika kuthibitisha kesi Jamhuri ilikuwa na mashahidi 11 na vielelezo 12. Mshtakiwa alikuwa shahidi pekee wa upande wa utetezi na hakuwa na kielelezo chochote.

Kumbukumbu za mahakama zinaonyesha Februari 27, 2024 shahidi wa nane ambaye ni karani wa Shirika la Posta Tanzania, Constantine Manyanda na shahidi wa tano, Ofisa Mkuu wa Forodha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wakiwa kazini ofisi za Posta Dar es Salaam, walipokea vifurushi kutoka uwanja wa ndege.

Ilidaiwa wakati wakiendelea kutekeleza majukumu yao, ofisa usalama wa posta walichukua vifurushi ili kuvichunguza ikabainika mfuko mmoja ulikuwa na vifurushi vitatu vilivyotiliwa shaka.

Mahakama ilielezwa kwenye skana vifurushi hivyo vilionyesha ndani kulikuwa na punjepunje na jina la mpokeaji Ahmed na namba yake ya simu.

Shahidi wa nane alitoa taarifa kwa msimamizi wake, Victoria Kambona aliyemuagiza avihifadhi akisubiri maelekezo zaidi.

Februari 28, 2024, shahidi wa tatu H27332 Koplo Jackson Shambwe ambaye ni Ofisa wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) alipata taarifa kuhusu vifurushi hivyo kupitia mtoa taarifa ambaye hakutajwa.

Ilielezwa vifurushi hivyo vilitoka Uholanzi na kuelekezwa kwa Ahmed.

Jalada la uchunguzi namba DCEA/PE/05/2024 lilifunguliwa akidai aliendelea kufanyia kazi taarifa zilizopatikana ikiwamo kupiga simu kwa namba iliyokuwa imeandikwa kwenye vifurushi hivyo.

Alidai simu ilipokewa na mtu aliyejitambulisha kwa jina moja la Ahmed, aliyethibitisha anatarajia kupokea kifurushi kupitia ofisi ya Posta.

Shahidi alidai mawasiliano yaliendelea hadi Machi Mosi, 2024 wakakubaliana aende kuchukua vifurushi vyake.

Machi 2, 2024 shahidi huyo wa tatu alikutana naye ofisi ya Posta akamweka chini ya ulinzi, akaomba awepo shahidi wa kujitegemea akapatikana shahidi wa 10, Amedeus Tukunjoba, aliyekuwa ndani ya eneo la Posta wakati huo.

Alidai alifanya upekuzi kwa mshtakiwa akapata simu nyeusi aina ya Samsung iliyokuwa na laini mbili na hati ya kusafiria ya Comoro yenye jina la Ahmed Bacar Abdou.

Machi 4, 2024 shahidi huyo wa tatu alianza uchunguzi akiwa na amri ya upekuzi iliyotolewa na Kamishna Mkuu wa DCEA.

Alimpeleka mshtakiwa kwa shahidi wa nane, ambako alikiri kwenda kufuata vifurushi vilivyotoka Uholanzi.

Vifurushi hivyo vilipelekwa ofisi ya DCEA vikakabidhiwa kwa shahidi wa tisa, ASP Johari na viliingizwa kwenye rejista ya vielelezo na kupelekwa kwa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA). Majibu yalionyesha ni dawa za kulevya.

Kumbukumbu za ushahidi zinaonyesha wiki mbili baadaye, Machi 20, 2024 DCEA ilipokea taarifa mpya kuhusu kifurushi kingine kilichoelekezwa kwa mshtakiwa katika kesi hii.

Katika tukio hilo, shahidi wa nne Ramadhan, alipewa jukumu la kufuatilia, akiwa na mshtakiwa Posta alikabidhiwa boksi dogo la kaki na kufanya taratibu za uhakiki.

Baada ya ukaguzi mbele ya shahidi wa kujitegemea ndani ya boksi kulikuwa na kifurushi cheupe kilichokuwa na kitambaa cha rangi ya fedha na mfuko wa nailoni ukiwa na chembechembe nyeupe zilizoshukiwa kuwa dawa za kulevya.

Jalada la uchunguzi namba   DCEA/IR/18/2024 lilifunguliwa na kifurushi kiliwasilishwa GCLA, ikabainika ilikuwa dawa za kulevya aina ya MDPV gramu 103.03.

Mshtakiwa alikiri mara kadhaa amekuwa akisafiri hadi Tanzania kununua nyanya, vitunguu na bidhaa zingine.

Alisema uzungumzaji wake wa lugha ya Kiswahili ulikuwa mdogo.

Alidai alikamatwa Feri akielekea Kigamboni baada ya kuzuiwa na mtu aliyemuuliza iwapo yeye ndiye Ahmed Mohamed, jina ambalo alilikana.

Mshtakiwa alidai watu zaidi waliongezeka akakamatwa na kupelekwa kwenye chumba kimoja, kisha akahamishiwa kingine kilichokuwa na masanduku na kulazimika kusaini nyaraka asizozielewa.

Alidai alipokataa alipigwa kisha akarejeshwa chumba cha kwanza, akiwa hana shati na kufungiwa ndani.

Alikana vielelezo vilivyotolewa mahakamani akidai hajawahi kuwaona baadhi ya mashahidi wa upande wa mashtaka, ingawa aliwatambua wachache kutoka eneo la Posta, akiwemo shahidi wa tatu.

Ahmed alikana kusaini kwa maandishi au dole gumba, akidai mawasiliano yote yalikuwa ya Kiswahili bila mkalimani.

Alidai asingeweza kusaini chochote asichokielewa, hivyo aliiomba mahakama imuachie huru.

Jaji Kisanya amesema baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili wajibu wa mahakama ni kuchambua, kutathmini na kuamua iwapo upande wa mashtaka umethibitisha kesi pasipo kuacha shaka.

Amesema ni wajibu wa upande wa mashtaka kuthibitisha shtaka bila kuacha shaka yoyote, isipokuwa pale ambapo sheria inatamka vinginevyo.

Amesema miongoni mwa masuala mahakama inayozingatia ni iwapo mshtakiwa aliagiza vifurushi hivyo, iwapo mlolongo wa ulinzi ulitunzwa ipasavyo.

Jaji amesema katika ushahidi wa upande wa mashtaka inaonyesha vifurushi viliandikwa Ahmed Bacar Adou na inakuwa vigumu kuelewa kama Ahmed Mohamed, Ahmed Bacar Adou na Ahmed Bacar Abdou, kama ni mtu mmoja anayeshtakiwa katika kesi hiyo.

Amesema hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa mshtakiwa aliombwa na ofisa wa posta au forodha, kutoa hati ya kiapo inayoeleza tofauti kati ya majina yaliyotajwa na jina linaloonekana kwenye hati ya kusafiria.

“Kutokana na maelezo hayo, ilikuwa ni wajibu kwa upande wa mashtaka kuthibitisha kuwa mshtakiwa ni yuleyule aliyewasiliana na shahidi wa tatu au vinginevyo, kwamba namba walizowasiliana naye zilisajiliwa kwa jina lake kama inavyotakiwa chini ya kifungu cha 101 cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta,” amesema.

Jaji amesema kutokana na kukosekana kwa usajili huo ilikuwa lazima kubainisha kwa uthabiti kuwa mshtakiwa ndiye aliyekuwa akitumia namba hizo zilizokuwa kwenye simu inayodaiwa kuwa ya mkononi ambayo haikutolewa kama kielelezo.

Amesema mlolongo wa ulinzi wa vielelezo ulivunjika tangu mwanzo kwa sababu upekuzi ulifanyika bila shahidi huru.

Jaji amesema kesi hiyo haijathibitishwa kwa kiwango kinachohitajika bila shaka yoyote, hivyo amemuachia mshtakiwa huru na kuamuru arudishiwe hati yake ya kusafiria.