Watanzania waitwa kupima magonjwa yasiyoambukiza bure

Dar es Salaam. Watanzania wameombwa kujitokeza kwa wingi katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam kuanzia Ijumaa, Novemba 28 hadi Jumapili, Novemba 30, 2025, kupima magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) bure.

Katika kambi hiyo kutafanyika uchunguzi wa magonjwa mbalimbali ikiwemo kiharusi, magonjwa ya moyo, saratani, kisukari na shinikizo la juu la damu. Kutatolewa pia matibabu ya awali, huku wagonjwa watakaohitaji uchunguzi au matibabu zaidi wakipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Amana.

Kambi hii imeandaliwa na GSM Foundation kwa kushirikiana na Hospitali ya Amana.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa asilimia 71 ya vifo duniani sawa na vifo milioni 41 vinasababishwa na magonjwa yasiyoambukiza. Nchini Tanzania, magonjwa haya yanachangia takribani asilimia 33 ya vifo vyote, yakichochewa na uvutaji tumbaku, kutofanya mazoezi, unywaji pombe kupita kiasi, ulaji usiofaa na uchafuzi wa hewa.

Akizungumza Jumanne, Novemba 25, 2025, wakati wa utiaji saini wa ushirikiano huo Hospitali ya Amana, Kaimu Mganga Mfawidhi, Dk Mafele Ihoyelo, amesema magonjwa yatakayopimwa pia ni ya koo, pua na masikio, meno, ngozi, macho, saratani ya shingo ya kizazi, saratani ya matiti na magonjwa ya watoto.

“Wananchi watakaohitaji huduma zaidi wataelekezwa Hospitali ya Amana na tutaendelea kuwahudumia hadi wapone,” amesema.

Amesema kambi hiyo itatumia kifaa cha body composition analysis kinachopima hali ya mifupa, nyama, ngozi, maji mwilini na kiasi cha mafuta ili kutathmini hatari ya kupata magonjwa yasiyoambukiza.

“Kipimo hiki kitaonesha uwiano wa viungo vya mwili na kutoa ushauri wa kitaalamu kuhusu namna ya kujikinga,” amesema Dk Ihoyelo.

Ameongeza kuwa Watanzania wanapaswa kuchangamkia fursa hiyo, akibainisha kuwa magonjwa yasiyoambukiza yako miongoni mwa magonjwa 10 yanayoongoza kwa kusababisha vifo duniani, hata kwa watu wenye umri chini ya miaka 20.

“Kwa sasa watu wengi wanakula vyakula visivyo salama kiafya. Nashauri kula vizuri, kufanya mazoezi na kupumzika ipasavyo ili kujikinga,” amesema.

Watu 300 kupata bima bure

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Bima kutoka Galco Insurance Brokers, Emmanuel Bugabu amesema watu 300 watapatiwa bima ya afya bure, ili kuhakikisha wanapata huduma za matibabu kwa uhakika.

Mkurugenzi wa GSM Foundation, Faith Gugu, amesema kambi hiyo inalenga kupunguza mzigo wa magonjwa yasiyoambukiza kwa kuwafikia wananchi wengi zaidi.

“Kati ya watu 300 watakaopata bima, watoto 100 ni kutoka mazingira magumu katika vituo vya kulelea watoto, wanawake 100 na wazee 100,” amesema.