Umasikini ni nyenzo kubwa kwenye migogoro ya watu. Unaweza kutokea mzozo wa kawaida, pengine watoto jirani wamepigana. Mama aliye masikini huweza kuwaza mbali kama “Au kwa sababu wao wana hela ndio wananipigia mwanangu?” Hivyo ugomvi wa matajiri wawili, au wa masikini dhidi ya masikini mwenzake unaweza kusuluhishwa kwa urahisi kuliko ugomvi baina ya tajiri na masikini.
Haya ni matokeo ya ukandamizaji wa haki ulioanzwa karne nyingi zilizopita. Mataifa makubwa yalipokuja kuliteka bara la Afrika, yaliwaleta watu wao kusimamia shughuli zao pamoja na kukusanya kodi. Watu hao walikosa ubinadamu kabisa na kuwachukulia wenyeji sawa na takataka. Walionyesha wazi kuwa jeuri waliyoitumia ilitokana na tofauti ya uwezo baina yao.
Thamani ya mtu ilipimwa kutokana na ukwasi wake. Baada ya Tanganyika kujipatia uhuru, tofauti hiyo ilimlazimisha Baba wa Taifa kuzindua Azimio la Arusha. Lengo lilikuwa kupunguza tofauti kati ya matajiri na masikini. Kwa maono yake ya mbali, aliuona ujamaa kuwa ndiyo njia sahihi ya kufuata. Lakini kutokana na kunyanyasika kwa muda mrefu, wazawa hawakuliona hilo. Waliona kuwa wanadumishwa kwenye udhalili.
Ni jambo lililo wazi kuwa akili ya tajiri hunyosha mambo kutokana na kujiamini. Mara nyingi malengo yao hutimia kwani wao huwekeza kwenye mambo wanayoyakusudia. Lakini kwa masikini, hali huwa tofauti. Anaweza akashindwa kufikia malengo kutokana na akili yake kuyumbayumba. Akiwa shuleni, atafikiria kutafuta pesa za kuikimu familia badala ya kuwekeza akili kwenye masomo.
Hii ndiyo sababu ukimwuliza mtoto wa tajiri matarajio yake ya ukubwani, anaweza kukueleza bila kutafuna maneno. Anayajua malengo yake, na anajua apite njia gani ili kuyafikia. Lakini mwulize masikini uone jinsi kona na breki zitakavyokuwa nyingi. Kwanza hajui hata kama atahitimu masomo yake vizuri; pale alipo kasimamishwa masomo kwa ukosefu wa ada. Usije ukashangaa masikini mtu mzima hajui yeye ni nani!
Unafika wakati akili ya masikini huganda, inagoma kufikiria mbinu mpya za kujikwamua. Hapa sasa ndipo afya ya akili yake hupungua na kuweka uadui na changamoto zinazomjia. Kila anapopata changamoto hujiuliza “Au kwa sababu sina hela?” Katika hatua hii, hasira zake huwa karibu sana, na huweza humkasirikia yeyote anayehitaji msaada kutoka kwake (hata mwanaye anayeumwa).
Mtu mwenye fedha anaweza kuongezewa bei ya mafuta akiwa kituoni. Atauma mdomo kidogo tu, kisha akachukua hatua za kuangalia kwenye vituo vingine vya jirani. Akikuta hali ni hiyohiyo kwenye vituo vyote, atapiga moyo konde, atajaza mafuta kwenye gari. Lakini kaa mbali kidogo unapomtajia nauli mpya masikini akiwa ndani ya daladala. Kwanza huujui ugomvi wake na mkewe uliotokana na kuwaacha watoto na njaa.
Nilisikiliza kwa makini maelekezo ya Waziri Mkuu kwa sekta ya afya, alipotembelea kwenye Hospitali ya Dodoma. Alitoa maagizo kuwa kinamama wajawazito wasicheleweshewe huduma hata kama watakosa baadhi ya vifaa. Ni hasara kubwa kumpoteza mama pengine na mwanaye mtarajiwa, ati kwa sababu amekosa shilingi laki mbili za kufanyia upasuaji. Hili naliweka pamoja na lile la majeruhi kutohudumiwa kwa kukosa PF-3.
Niliyaunganisha hayo na ahadi zako kwenye kampeni uliposema Serikali itatoa Bima ya Afya kwa kila Mtanzania, na lile la kutozuiliwa kwa miili inayodaiwa na Hospitali. Hii imekaa vizuri sana, ila nina machache ya kuchangia ili Serikali na wananchi wake masikini wakutane kwenye kiwanja kimoja. Nahisi kama kuna jambo linahitaji kusukumwa.
Ombi likitolewa na Mkuu ni amri kwa wapokeaji. Ninaamini Serikali ikimwomba Wakala wa Bima ya Afya awape huduma Watanzania wote, utekelezaji wake hautachukua siku mia moja. Sekta ya afya inawagusa masikini wengi, tena hasa wale wasio na uwezo wa kupata Bima. Wanapotakiwa kulipia matibabu, ndipo kengele ya hatari ya kumpoteza mpendwa wao inapogonga.
Jambo lingine linalowaua masikini ni kutosomana kwa mifumo ya kimatibabu, au sintofahamu ya wahudumu. Masikini wasio na bima ya mgonjwa wao, watachangishana kwa mbinde na kupata laki mbili kwa ajili ya kipimo chake. Baada ya kulipia, majibu yanawaelekeza kwenda kwenye Hospitali ya Rufaa. Huko tena watatakiwa kuanza mbinde za kuchangia upya kipimo kilekile.
Nadhani si peke yangu ninayejiuliza: Huu ndio mfumo wa tiba zetu ulivyo, au kila Hospitali imeweka lengo la kukusanya fedha zaidi kutoka kwa wagonjwa? Kulingana na maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano, kila hatua iliyofikiwa na hospitali ya kwanza inatakiwa kusomeka vizuri na hospitali zingine. Vipimo ni vilevile na madaktari ni walewale.
Mimi naamini kuwa vipimo vinahitajika kuanzwa upya, pale daktari wa Rufaa anapogundua kuwa mgonjwa hakutibiwa kwenye Hospitali iliyosajiliwa. Kimaadili Hospitali iliyosajiliwa huwa na madaktari wenye ithibati. Hivyo sikutegemea Muhimbili wakatae vipimo vya Moganzira.
Haya si mageni. Ni maisha ya kila siku ya Watanzania masikini. Kwa maoni yangu, mambo haya yakirekebishwa mapema yanaweza kufuta kabisa tofauti za wananchi na Serikali yao. Wananchi wameaminishwa na wakaamini kuwa Serikali yao inaweza, sasa inapokuwa kinyume hawakawii kujiuliza “Au kwa kuwa Serikali ina uwezo na sisi wananchi hatuna?”
