Ushabiki wa vifo Okt 29 unafunika ubinadamu

Watanzania walipoteza maisha katika vurugu za Oktoba 29, 2025, na baada yake. Hilo halibishaniwi. Kuhusu idadi, bado kuna shida. Maamlaka bado hazijatoa ripoti kamili. Pengine Tume ya Uchunguzi (Enquiry Commission), iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan itamaliza utata.

Watanzania walipoteza mali zao. Wapo walioibiwa na kuvunjiwa vituo vyao vya kibiashara, kuna waliochomewa moto. Hili halibishaniwi. Ujumbe nyuma ya matukio ya wizi na uchomaji moto mali za watu binafsi, ulibeba chuki kubwa. Mjadala huu haupaswi kukwepwa.

Uharibifu mkubwa wa mali za umma ulifanyika. Miundombinu na mabasi ya usafiri wa mwendokasi, Dar es Salaam, viliharibiwa kwa mashambulizi ya mawe na silaha nyingine, na zaidi ni kuchoma moto. Uratibu wa matukio hayo, hautakiwi kutomulikwa, wakati wa mjadala wa matukio ya Oktoba 29 na madhara yake.

Oktoba 29, 2025, ilikuwa siku ya Uchaguzi Mkuu 2025 kwa Tanzania. Vyama 17 kati ya 18, vilishiriki uchaguzi. Mchana wa siku hiyo, matukio ya ghasia yalianza. Wasiwasi ulikuwa mkubwa. Zipo taarifa za watu kuwawinda waliojitokeza kupiga kura, kwa kuwakagua alama za wino ili kuwabaini waliopiga kura na kuwakata vidole. Hili pia si la kuepuka kujadili.

Kwa baadhi ya watu Oktoba 29, kitendo cha kujitokeza kupiga kura kwa ajili ya kutekeleza haki ya msingi ya kikatiba, kilikuwa kosa lenye kustahili kukatwa kidole. Fikra hizi zilitokea wapi? Kwa nini iliibuka aina hiyo ya mawindo miongoni mwa Watanzania? Tunaachaje kuzungumzia hilo?

Matukio ya Oktoba 29, 2025, hayakuibuka kama hadithi ya simba kuzaa, kwamba mvua inanyesha kipindi jua likiwaka. Yalikuwa matukio yenye mtiririko wa sanyansi kamili, wingu lilitanda, ndipo mvua ilinyesha. Swali ni hili; wingu la Oktoba 29, lilitanda vipi?

Jibu lipo kwenye matumizi ya mitandao ya kijamii. Wito wa baadhi ya watu wenye ufuasi mkubwa, kuhamasisha vijana kutoka “kuikomboa” nchi yao. Vijana waliambiwa nchi yao inaliwa na wachache, kwa hiyo lazima watoke kuzuia uchaguzi, na kumwondoa Rais Samia madarakani.

Mitandao ya kijamii ilitumika kuwaaminisha wananchi kwamba Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), lilikuwa tayari kwa ajili ya kumwondoa Rais Samia madarakani, kilichotakiwa ni watu waingie barabarani, halafu wanajeshi wangemaliza kazi yao. Sehemu hii ya hamasa haitakiwi kutofikiwa katika mjadala au ripoti yoyote ya Oktoba 29.

Mtu ambaye alihusika na uhamasishaji wa aina hii, ambao ulikwenda ndani zaidi na kuchokonoa utiifu wa vyombo vinavyolinda nchi, anaachwaje kutohojiwa na vyombo vya habari, aweze kueleza ni kwa nini alichagua njia ya hamasa ambayo imekuwa gharama kubwa kwa Watanzania?

Vipi kuhusu vijana walioingia barabarani wakiwa wamebeba silaha kabisa? Waliokuwa na madumu ya petroli na viberiti. Uratibu wa watu na zana hizo, unatakiwa kufanyiwa kazi ya kutosha.

Matukio ya Oktoba 29, hayatakiwi kuchambuliwa au kuripotiwa kwa taarifa za juujuu. Kazi kubwa, yenye mzunguko wa nyuzi 360, inapaswa kufanyika.

Zipo ripoti za idadi ya vifo mitandaoni. Mashirika ya habari ya kimataifa, Al Jazeera na BBC, yalimnukuu msemaji wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Brenda Rupia, kuwa waliopoteza maisha kwa makadirio ni watu 700. Wakati kukiwa na mshangao, vilevile kuhoji usahihi wa makisio hayo, namba zikaanza kupaa.

Kuna watu wakasema waliouawa ni 2,000, bado ikaonekana ni kidogo, ikapanda hadi 10,000. Wiki iliyopita niliona taarifa ya mtabdao mmoja Kenya, ikionesha kwamba idadi ya vifo ni 23,000. Kabla ya kujadili usahihi wa namba, swali ni moja; mbona ushabiki wa namba ya vifo ni mkubwa?

Yupo mtu anasema kwa mtindo wa kutaka watu watafakari kwamba ikiwa waliojitokeza barabarani hawakufika hata 1,000, iweje vifo viwe 700? Hapo anakumbusha kuwa watu wengi walikamatwa, na ndiyo ambao wamefikishwa mahakamani.

 Idadi ya waliokamatwa ni kipimo kuwa kulikuwa na ukamataji, na siyo msukumo wa kuua. Ndivyo alivyonijengea hoja.

Mtu huyo hataki hata kujadili idadi ya watu 10,000 au 23,000. Yeye anaona namba ya 700 ni upotoshaji mkubwa. Anaamini kuwa kuua watu 700 kwa risasi, siku moja, maana yake polisi walikuta watu kwenye kundi moja lenye idadi hiyo, wakamimina risasi hovyo.

Kupata idadi hiyo, kama kila mtu wastani wa kifo kwa mtu mmoja ni dakika 2, maana yake watu 700, wangeweza kuuawa ndani ya dakika 1,400. Hizi ni saa 23 na dakika 20. Yaani siku nzima, kasoro dakika 40. Namba hiyo ikurejeshe kwenye tafakuri ya watu waliongia barabarani, muda na idadi ya vifo.

Kuhusu vifo 10,000. Ikiwa kila kifo ni dakika 2, dakika 20,000 zitatumika. Hiyo ni sawa na karibu siku 14. Yaani nusu mwezi. Hesabu itakuonesha kwamba ili kufanikisha kuua watu 10,000 kwa siku moja, inatakiwa mambo mawili yatokee; kwanza mabomu (makombora) yatumike, na watu wakusanyike.

Ripoti ya CNN, imenukuu taarifa ya vifo 2,000. Video zao hazioneshi kundi japo la watu 20 kwa pamoja. Ni makundi ya watu wachache wakikimbia. Mazingira hayo ya video za CNN, yanaonesha kwamba kama polisi wangekuwa wanawakimbiza watu wawaue, wastani kifo kimoja, ungeweza kugharimu risasi tano. Hiyo ni sawa na SGM 250 za risasi 40 kila moja.

Mazingira hayo ya video za CNN, unaweza kupendekeza kuwa wastani wa kifo kimoja, ungeweza kuwa dakika tano. Maana yake, kupata vifo 2,000, ingechukua wiki nzima. Hapo maana yake kungekuwa hakuna kukamata, ni kusaka watu na kuwaua. Je, ni sahihi namba hiyo?

Jambo ambalo haitakiwi kupingana ni kwamba watu wamekufa. Ni kitu kibaya mno. Kinachotakiwa ni kuachana na ushabiki.