Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, toleo la mwaka 2010, inaelekeza kuundwa kwa SUK ambapo chama kilichoshinda kitashirikiana na chama chochote cha upinzani kilichotokea cha pili kwa wingi wa viti vya majimbo katika Baraza la Wawakilishi.
Wataingia au watasusa? Kuna faida gani wakiingia? Haya ni maswali yanayoulizwa na wadau wa siasa za Zanzibar endapo chama cha ACT Wazalendo kitaingia kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) ili kuunda Serikali ya pamoja na Chama cha Mapinduzi (CCM), kwa mujibu wa Katiba.
Hata hivyo, ni mara chache manufaa ya kushiriki kwa upinzani serikalini yanamulikwa. Pengine, baadhi ya watu hawajui kwanini SUK ilianzishwa visiwani Zanzibar, jambo linalowafanya kuona ushiriki wa upinzani wenye nguvu kwenye Serikali.
Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, toleo la mwaka 2010, inaelekeza kuundwa kwa SUK ambapo chama kilichoshinda kitashirikiana na chama chochote cha upinzani kilichotokea cha pili kwa wingi wa viti vya majimbo katika Baraza la Wawakilishi.
Ibara ya 9(3) ya Katiba hiyo inaeleza kwamba Muundo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar utakuwa wa Umoja wa Kitaifa na utendaji wa kazi zake utafanywa katika utaratibu utakaohakikisha kuendelezwa kwa umoja nchini na lengo la kufikia demokrasia.
Katika uchaguzi uliofanyika visiwani humo Oktiba 28 na 29, 2025, mgombea wa CCM, Dk Hussein Mwinyi alitangazwa mshindi katika uchaguzi huo kwa kupata kura 448,892 sawa na asilimia 74.8 ya kura zote.
Mpinzani wake wa karibu, Othman Masoud Othman wa ACT- Wazalendo alipata kura 139,399 sawa na asilimia 23.22 kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).
Pamoja na matokeo hayo, ACT Wazalendo kilifanikiwa kupata wawakilishi 10 kwenye uchaguzi huo pamoja na wawakilishi wa viti maalumu wanne, hivyo wanakidhi vigezo vya kuingia kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Tayari Rais Mwinyi ametangaza baraza lake la mawaziri huku akiacha wazi nafasi za mawaziri wanne kwa ajili ya chama hicho licha ya kwamba kinastahili kupata mawaziri watatu kulingana na idadi ya viti kilivyovipata.
Wizara walizoachiwa ACT Wazalendo ni pamoja na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Wizara ya Afya na Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale.
Akizungumzia ACT Wazalendo kuachiwa Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale, Dk Mwinyi alisema wamefanya hivyo kwa utashi mwema kuwaachia wenzao wizara hiyo inayoongoza uchumi wa Zanzibar.
“Sekta kuu ya uchumi hapa Zanzibar ni utalii, basi tumeona tuwe na good will (matashi mema), sekta kiongozi tuwape wao,” alisema Rais Mwinyi.
Novemba 13, 2025 wakati akitangaza mawaziri wake, Dk Mwinyi alisema: “Hizi nafasi zitabaki wazi kwa mujibu wa katiba mpaka pale kipindi kitakapokwisha ambacho kikatiba ni siku 90.”
Hivyo, ACT Wazalendo kina wajibu wa kufanya uamuzi wa kuingia SUK au la ndani ya siku 90 zilizowekwa kikatiba na muda huo ukipita, basi Dk Mwinyi atalazimika kujaza nafasi hizo kwa kadiri itakavyompendeza.
Katika ombwe hilo la kushiriki ama kutoshiriki kwa chama hicho cha upinzani, mjadala umekuwa ni upi umuhimu wa SUK kwa maisha ya Wazanzibar na mustakabali wa maendeleo na amani yao kwa miaka ijayo.
Wadau mbalimbali wa siasa wanajadili faida za ACT Wazalendo kuingia kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa, ikiwamo kujenga umoja wa kitaifa na kuepusha vurugu zilizojitokeza Januari 2001 baada ya uchaguzi mkuu wa 2000.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA), Profesa Mohamed Makame Haji, anasema hatua ya ACT–Wazalendo kujiunga na SUK ni muhimu katika kuimarisha misingi ya maridhiano, utulivu na ustawi wa nchi huku akisisitiza kuwa hatua hiyo inaendana na matakwa ya wananchi na misingi ya Katiba.
Kuhusu nafasi ya serikali ya umoja wa kitaifa katika historia ya Zanzibar, Profesa Haji anasema mfumo huo umejengwa kutokana na matukio ya kiuchaguzi na uzoefu wa uendeshaji wa serikali uliowalazimu Wazanzibari kupitisha maridhiano ya kikatiba.
“Maridhiano hayo yamepita kwenye misingi ya kisheria na kikatiba hadi kufikia kupata maoni mbalimbali ya wananchi. Hatimaye Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 ilifanyiwa marekebisho mwaka 2010 na kuweka maridhiano kama msingi wa kikatiba,” anasema.
Kwa mujibu wa Profesa Haji, anasema mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa unataka chama kitakachoshinda uchaguzi kutoa Rais, wakati chama kitakachofuata kwa wingi wa kura kutoa Makamu wa Kwanza wa Rais, sambamba na mgawanyo wa nafasi za uwakilishi na baraza la mawaziri.
Anasema umuhimu wa ACT–Wazalendo kuingia serikalini ni kuendeleza matakwa yaliyowekwa na wananchi kwenye marekebisho ya Katiba ya mwaka 2010, na kuonyesha heshima kwa misingi ya kitaifa iliyokubaliwa pamoja.
“Kujiunga kwao litakuwa jambo zuri na kielelezo cha heshima ya kitaifa. Ni kuonyesha yaliyoamuliwa na wananchi na kudumishwa,” anasema.
Profesa Haji anabainisha faida nyingine kuwa ni kupunguza mivutano ya kisiasa na kuongeza tija ya uendeshaji wa serikali, kwa kuwa ushirikiano wa vyama hutengeneza mazingira ya amani, umoja na uamuzi wa pamoja.
“Kwa hali tulizonazo Watanzania na Wazanzibari, tunashuhudia mafanikio yanayopatikana pale vyama vinaposhirikiana kuongoza Serikali, ikiwamo kupunguza mizozo,” anasema.
Akifafanua zaidi, Profesa Haji anasema ushiriki wa vyama vyenye uwakilishi katika uamuzi wa serikali huleta umiliki wa pamoja na huongeza ufanisi katika uongozi, jambo linalorahisisha utekelezaji wa mipango ya maendeleo.
“Itasaidia kuleta mshikamano na kuimarisha umoja na amani. Panapokuwa na mvutano hakuna jambo la maana linaloweza kufanyika kwa ustawi wa wananchi,” anasema.
Anasema serikali ya umoja wa kitaifa ni nguzo muhimu kwa Zanzibar kubakisha amani iliyopo na kurejesha matumaini ya wananchi kupitia serikali inayowasikiliza na kushirikisha pande zote.
Anasema kutoshiriki kwa ACT–Wazalendo kutawaathiri zaidi wananchi wa kawaida, kuliko viongozi wa juu wa chama.
“Viongozi wakishirikiana hata wananchi wanapata haueni. Kuna wepesi wa kutekeleza mambo ya kijamii na kiuchumi kwa kushindanisha hoja za sera,” anasema.
Profesa Haji anahitimisha kwa kusisitiza kuwa vyama vya siasa vinapaswa kuzingatia dhamira ya kuleta maendeleo kwa wananchi kwa kushirikiana, akisema:
“Kama vyama vitakuwa na dhamira moja ya kuleta maendeleo, itakuwa vizuri kujenga serikali ya kitaifa kwa maslahi ya wengi.”
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Faraja Christoms anasema ushirikishwa kwa viongozi wa upinzani katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa kuna uwezo mkubwa wa kutuliza mihemuko ya kisiasa na kuongeza uwazi katika utendaji wa Serikali.
Akizungumza jana, Dk Christoms anasema kuwa hatua hiyo inaweza kuwapa utulivu wafuasi wa vyama vya upinzani kwani viongozi wao wanapata nafasi ya kushiriki moja kwa moja katika uongozi wa nchi.
“Itasaidia kupunguza mihemuko ya kisiasa kwa wafuasi wao na viongozi wao wakiwa serikalini. Kama kuna ubovu au utendaji mbaya, na wao wanakuwa wananyoshewa kidole,” anasema.
Dk Christoms anasema ushiriki wa viongozi wa upinzani katika serikali una manufaa makubwa kwa mustakabali wa demokrasia ya nchi, kwani unawaandaa kuiongoza serikali siku zijazo.
“Viongozi wa upinzani mbeleni wanaweza kuongoza Serikali, kwa hiyo ushiriki wao kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa; kwanza, unawajengea imani kwa wananchi na uzoefu wao unaonekana,” anasema.
Anasema ushiriki huo unarahisisha kwa wananchi kupima uwezo wa viongozi wa upinzani wanapopewa dhamana za kiutendaji.
“Ni rahisi kwa wao kupimika kama wanaweza kuachiwa nchi au la. Lakini pili, chama kilichopata kura nyingi kina nguvu ya kuwaambia wananchi jinsi wizara chache walizopewa viongozi wa upinzani zinavyofanya kazi,” anasema.
Pia, anasema kushirikisha vyama vya upinzani imeelezwa kuwa ishara ya kuimarika kwa misingi ya demokrasia na ushirikishwaji katika uongozi wa taifa.
SUK ni kwa ajili ya wananchi
Mchambuzi wa siasa, Hamduny Marcel, anasema iwapo ACT-Wazalendo hawatajumuika katika SUK, wataonekana kuvunja Katiba ya Zanzibar, licha ya kukiri kuwa bado haijawa wazi hatua za kisheria zinasemaje ikiwa chama hicho kitaamua kujiondoa kwenye mchakato huo.
Kuhusu wajibu wa kisiasa na kikatiba wa vyama vya siasa Zanzibar, Marcel anasema mfumo wa SUK si suala la hiari kwa vyama pekee, bali ni matakwa ya Katiba ambayo yanaeleza wazi kuwa chama chochote kitakachopata angalau asilimia 10 ya kura za urais kina haki ya kutoa Makamu wa Kwanza wa Rais na kushiriki katika uongozi wa baadhi ya wizara.
“Uundwaji wa SUK si utashi tu wa vyama, bali ni kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ambayo inasema chama kikipata asilimia 10 ya kura zote kina haki ya kutoa Makamu wa Kwanza na kuongoza baadhi ya wizara,” anasema Marcel.
Anaongeza kuwa hatua ya ACT-Wazalendo kutoshiriki SUK itakuwa kurudisha nyuma jitihada za kuimarisha demokrasia Zanzibar ambako kwa miaka ya hivi karibuni kumeshuhudiwa maendeleo katika ushirikishwaji wa kisiasa.
“Wasipojiunga, itakuwa moja kwa moja wanarudisha nyuma juhudi za Zanzibar katika ujenzi wa demokrasia kwa hatua ambayo tayari walishaipiga mbele,” anasema.
ZEC ilitangaza waliojiandikisha kupiga kura visiwani humo ni 717,557 lakini waliopiga kura 609,096 sawa na asilimia 84.88. Kati ya kura hizo zilizoharibika ni 8,863 sawa na asilimia 1.46.
Ukilinganisha na matokeo ya mwaka 2020, Dk Mwinyi ameshuka kwa asilimia mbili, mwaka huo alipata asilimia 76.27 dhidi ya aliyekuwa mshindani wake wa karibu wa ACT-Wazalendo, hayati Maalif Seif Sharif Hamad ambaye alipata asilimia 19.87.
Mpinzani wa karibu wa Dk Mwinyi, Othman Masoud Othman wa ACT- Wazalendo alipata kura 139,399 sawa na asilimia 23.22 kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).
Wagombea wa vyama vingine na kura walizopata ni Laila Rajab Khamis wa NCCR- Mageuzi kura 1,643, Juma Ali Khatib wa Ada- Tadea 1,455, Ameir Hassan Ameir wa Makini 1,435 na Hamad Rashid Hamad wa ADC 1,345.
Wengine ni Mfaume Khamis Hassan wa NLD kura 1,301, Hamad Mohamed Ibrahim wa UPDP 1,299, Said Soud Said wa AAFP 1,238, Khamis Faki Mgau wa NRA 1,161 na Hussein Juma Salim wa TLP.
