Dar es Salaam. Tanzania imechukua hatua madhubuti za kupunguza vifo vya watoto wachanga kupitia ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP) unaohusisha Hospitali ya Aga Khan, Chuo cha Tiba cha Chuo Kikuu cha Aga Khan na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana.
Ushirikiano huo, unaoungwa mkono na Chama cha Madaktari Bingwa wa Watoto Tanzania (PAT), unalenga kujenga uwezo wa madaktari na wauguzi wa watoto wachanga.
Hatua hiyo inalenga kuimarisha ustahimilivu wa awali kwa watoto wachanga, jambo ambalo wataalamu wanaeleza kama ‘kiungo kilichokosekana’ katika kupunguza vifo vya watoto wachanga.
Licha ya Tanzania kupiga hatua kubwa katika kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano katika miongo ya hivi karibuni, vifo vya watoto wachanga vimeendelea kuwa juu.
Kwa mujibu wa takwimu za UN Inter-Agency Group for Child Mortality Estimation (UN IGME 2023), Tanzania ina vifo 24 kwa kila vizazi hai 1,000, kiwango ambacho ni mara mbili ya lengo la Shirika la Afya Duniani (WHO) la kufikia vifo 12 ifikapo 2030.
Takwimu za kitaifa zinaonesha takribani nusu ya vifo vyote vya watoto chini ya miaka mitano hutokea ndani ya siku 28 za kwanza za maisha, mara nyingi kutokana na sababu zinazoweza kuzuilika kama vile kukosa hewa wakati wa kuzaliwa, uzito mdogo na maambukizi.
Hivyo, PPP inalenga kuimarisha utulivu wa awali wa watoto wachanga, saa na siku za mwanzo baada ya kuzaliwa, kupitia mafunzo kwa madaktari na wauguzi wa hospitali za msingi na vituo vya wilaya.
Baadhi ya mafunzo ni kuhusu ujuzi muhimu kama msaada wa kupumua, udhibiti wa joto, usimamizi wa maambukizi na matumizi ya vifaa vya kisasa vya watoto wachanga.
Akizungumza na Mwananchi jana, Novemba 24, 2025, daktari bingwa wa watoto ambaye pia ni mhazini wa PAT, Dk Naomi Mwamanenge, amesema mwelekeo huo umekuwa ukihitajika kwa muda mrefu.
“Tanzania sasa inaelekea kuboresha kiwango cha uhai wa watoto wachanga ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakipitwa, ilhali nguvu kubwa imekuwa kwa watoto chini ya miaka mitano,” amesema na kuongeza:
“Vifo vingi vya watoto chini ya miaka mitano vinatokana na changamoto wanazokutana nazo katika siku 28 za kwanza. Tumeona kupitia tafiti kwamba ukosefu wa ujuzi na matumizi hafifu ya teknolojia katika vituo vya ngazi za chini vinachangia kwa kiasi kikubwa vifo hivyo.”
Dk Mwamanenge, anayefanya kazi Hospitali ya Aga Khan, amesema Serikali imewekeza kwenye vifaa vya kisasa katika vituo vingi vya afya, lakini pengo la ujuzi bado lipo.
“Tunavyo vifaa, ndiyo; lakini madaktari wengi bado wanashindwa kuvitumia ipasavyo. Ndiyo maana programu hii ni muhimu. Tunawafundisha madaktari na wauguzi kutoka maeneo yote nchini ili waelewe nadharia na vitendo sahihi vya kuhudumia watoto wachanga tangu siku ya kwanza,” amesema.
Programu hiyo ya msingi kwa uangalizi wa watoto wachanga imeundwa kuhakikisha kiwango sawa cha huduma nchini.
“Mtoto akipelekwa Aga Khan au hospitali ya wilaya, ahudumiwe kwa ubora uleule katika hatua za awali. Ulinganifu huo ndiyo utakaookoa maisha,” amesema.
Wizara ya Afya imeweka kipaumbele katika kuimarisha huduma za watoto wachanga na wajawazito kupitia Mpango Mkakati wa Taifa (One Plan II) na katika kutekeleza mpango wa WHO wa Every Newborn Action Plan (ENAP).
Kupitia PPP hiyo, utekelezaji unakwenda sambamba na juhudi za Serikali za kusogeza huduma za kibobezi hadi ngazi za chini, kupunguza rufaa zisizo za lazima na vifo vinavyotokea wakati wa usafirishaji.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, zaidi ya asilimia 40 ya vifo vya watoto wachanga hutokea wakati wa kuhamishwa kutoka vituo vya msingi kwenda hospitali za juu.
Daktari bingwa wa watoto wachanga katika Chuo Kikuu cha Matibabu cha Aga Khan na mmoja wa wakufunzi wa programu hiyo, Dk Rukshar Osman, amesema: “Lengo letu ni kuongeza ujuzi wa madaktari na wauguzi wanaofanya kazi katika hospitali za ngazi ya I na II ili waweze kuokoa maisha ya watoto wachanga kabla ya kuwapeleka kwenye hospitali za juu.”
“Tumeweza kupunguza vifo vya wajawazito kwa kiasi kikubwa, lakini vifo vya watoto wachanga bado vipo juu—24 kwa kila vizazi hai 1,000. Kwa kuimarisha uwezo wa sekta ya umma, tunataka kubadili hali hiyo,” amesema.
Programu hiyo ya wiki kumi inachanganya masomo ya mtandaoni, nadharia na mafunzo kwa vitendo. Washiriki wa kundi la kwanza wanatarajiwa kurudi katika vituo vyao kama wakufunzi wa wenzao.
“Ustahimilivu wa awali unaokoa maisha. Mtoto akihudumiwa vizuri katika saa na siku za mwanzo, nafasi ya kuishi huongezeka,” amesema.
Dk Habakkuk Silas, kutoka Hospitali ya Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, amesema mafunzo hayo yamekuwa ya mabadiliko makubwa kwake.
“Fursa hii imekuwa baraka. Nimejifunza ujuzi wa vitendo, ikiwemo msaada wa kupumua eneo ambalo mara nyingi tumekuwa tukikosea bila kutambua,” amesema na kuongeza:
“Vifo vingi vinatokea kwa watoto kutoka vituo vya chini kwenda hospitali za rufaa. Kupitia mafunzo haya, sasa tunajua nini cha kufanya ngazi ya chini ili kuzuia vifo.”
