Arusha. “Nawaomba Watanzania, wananchi wenzangu mnisaidie niweze kupata matibabu kokote ya kuwekewa kitu cha kutolea mkojo, nateseka sana naombeni mnisaidie maana nimeumia sana, vijana wenzangu, kinamama naombeni mnisaidie .”
“Hali yangu siyo nzuri sana ninaomba Watanzania wanisaidie kulipa gharama za matibabu, wanishike mkono ili niweze kulipa kwani nimeambiwa hadi jana gharama ni zaidi ya Sh1.5 milioni,”
Hayo ni maombi ya Baraka Melami (40), mkazi wa Kijiji cha Olevolosi, Kata ya Kimnyaki wilayani Arumeru ambaye anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Selian baada ya kujeruhiwa kwa kukatwa uume na mkewe, Anna Melami (30).
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Novemba 26,2025, Melami ambaye bado amelazwa hospitalini hapo, ameomba Watanzania kujitolea kumsaidia kulipa gharama za matibabu.
“Hali yangu siyo mbaya sana lakini ni mbaya labda Mungu anisaidie, ninaomba Watanzania wanisaidie kulipa gharama za matibabu hapa hospitali, naomba wanishike mkono niweze kulipa deni na nimeambiwa na ndugu yangu anayenihudumia kuwa gharama zimefikia zaidi ya Sh1.5 milioni,”amesema.
Akisimulia namna tukio hilo lilivyotokea, Melami amedai kuwa usiku saa saba kasoro wakiwa wamelala na mke wake, mke wake alianza kumtomasa na kumshika sehemu za siri ambapo alichukua kisu na kumkata sehemu hizo za siri na kutupa chini ya uvungu wa kitanda.
“Usiku alianza kunitomasa na iliposimama akachukua kisu akaikatia yote, akanifunika na blanketi kubwa akaanza kuninyonga, nikapambana naye hadi nikaweza kutoka naye nje nikipiga kelele, watu wakaja kunisaidia wakanitoa na kunileta hospitalini.”
“Hamna ugomvi wowote tunafanya kazi ya kuuza dukani kwetu, tulilala vizuri hakuna aliyekuwa na shida na mwenzake. Mimi nina mtoto mmoja tu na kwa kuwa tuna kitanda kimoja hapa kingine kipo dukani mara nyingi mke wangu alikuwa analala na mtoto kule, akihitaji tendo la ndoa anakuja tunalala huku,”amesema.
Melami ameeleza kuwa mchana kabla ya tukio hilo, walichimba choo nyumbani kwao, wakaendelea na biashara ya kuuza duka hadi jioni walipofunga na kurudi nyumbani kulala.
Amedai baada ya tukio hilo mkewe alijifanya amepoteza fahamu ndugu na majirani walitoka na wakawachukua wote wawili na kuwapeleka hospitali na wakati anajaribu kumnyonga alimwambia anataka kumuua halafu na yeye anajiua kwa kunywa sumu.
“Hatujagombana karibu miezi mitatu na baada ya kufika hapa wakauliza hiyo sehemu ya siri ilipo na ndugu zangu walirudi nyumbani kuitafuta na walipoileta madaktari walisema imeshapoa haifai kurudisha tena,”
Amedai kuwa siku hiyo mkewe alifungulia redio kwa sauti kubwa tofauti na siku zingine ambapo baada ya tukio hilo kutokea hata alipokuwa akijaribu kupiga kelele kuomba msaada nje sauti haikuweza kusikika.
Akizungumzia kukamatwa kwa mkewe, Melami alimuomba Rais Samia kuamuru Jeshi la Polisi kumuachia mkewe kwani amemsamehe japo hataishi naye tena.
“Kwenye hili kuna la kujifunza unaweza ukalala ndani na mke wako lakini haujui alichojipanga kukufanyia cha muhimu zaidi ni watu kupata nuru na ufahamu kuishi na wake zao, maana hakuna anayejua hisia za mtu, huyu mwanamke ameshikwa na Serikali, kwao mimi nimeoa najua udhaifu wao hawana chochote nakuomba kama mama Rais Samia Suluhu Hassan aamuru Polisi wamuachie,”amesema na kuongeza
“Kwa sababu ameshaniharibu na sitaweza kuishi naye naomba umuachie aende nyumbani kwao, amenifanyia jambo baya, amenijeruhi moyo wangu lakini namsamehe aende kwao.”
Melami amesema wamekaa na mkewe muda mrefu na wamejaaliwa mtoto mmoja.
Mdogo wa mwathirika wa tukio hilo, Paulo Melami amedai kwa kuwa kaka yao ameamua kumsamehe mke wake na wao wanaomba aachiwe huru akapambane na maisha yake.
“Sisi tunaomba Polisi watusaidie ile sehemu iliyokatwa tuletewe wazee watambukie kimila, kwani sidhani kama maisha yake yatasonga mbele kama kawaida. Nikiwa kama mdogo wake wa tatu sisi tunaomba huyo mwanamke aachiwe huru akapambane na maisha yake.”
Mama wa mwathirika atoa neno
Kwa upande wake mama wa kijana huyo, Natanywak Melami ameeleza kuwa ana uchungu kutokana na tukio hilo kwa kuwa kijana wake hawezi kuzalisha tena na katika jamii hiyo hawajawahi kuona au kusikia tukio la namna hiyo.
“Sisi kabila ya Kimasai ukishika mwanaume shingo ni kosa, heri mwanaume akupige. Mimi nina uchungu kwa sababu sasa hivi Baraka hana kazi (hawezi kuzalisha), mimi sijamsamehe mkewe kwa sababu amefanya kitu ambacho Masai hajawahi kufanya,” amesema na kuongeza.
“Hakuna ugomvi wakati huu, zamani walikuwa na ugomvi wanagombana mwanamke akawa anaenda kwa babake akarudi nikabembeleza kijana wangu hamna ugomvi kwa sasa mwaka huu hawakuwa na ugomvi kabisa.
“Ni shetani kwani hajawahi kuleta malalamiko kabisa, mimi siwezi kusamehe huyo ni mnyama tu siko tayari kumsamehe nina uchungu, watu wanajaa hapa kwangu wakisikitika,”amesema.
Mwenyekiti wa Kitongoji anapoishi Melami na mkewe, Jonas Lendiki amesema alipigiwa simu saa nane usiku kuwa kuna mtu amefanyiwa ukatili katika eneo hilo.
“Nilipotoka nilikuta ameshapelekwa hospitali na katika eneo hili haijawahi kutokea tukio la namna hii na watu kama wana migogoro ya ndoa wasijichukulie sheria mkononi kama huyu alivyofanya,” amesema.
Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mwinyi Ahmed Mwinyi amekiri kuwa na taarifa za tukio hilo na mshtakiwa amekamatwa na anashikiliwa na Jeshi la Polisi.
Amesema kuwa ofisi yake itatuma timu ya wataalamu wa afya kwenda kumuona mgonjwa huyo ambapo na yeye pia ataenda kumuona.
“Kwa sasa suala hilo linashughulikiwa na vyombo vya ulinzi na usalama ngazi ya wilaya,”amesema Mwinyi.
