Arusha. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Arusha, imetupilia mbali maombi ya makada watatu wa Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), waliokuwa wakiomba kuwasilisha maombi ya marejeo ya Mahakama kupinga mkutano mkuu wa chama hicho uliofanyika mwaka huu na kuchagua viongozi.
Mahakama hiyo imefikia uamuzi huo baada ya kukubaliana na pingamizi lililowasilishwa na wakili wa wajibu maombi hayo kuwa maombi hayo ni batili kwa kuwa hayajakidhi matakwa ya kisheria.
Maombi hayo yaliwasilishwa makada watatu wa chama hicho ambao ni Issa Magere, Geofrey Steven na Kinanzaro Mwanga.
Wajibu maombi walikuwa ni Bodi ya Wadhamini wa chama hicho, Mwenyekiti wa TLP Taifa, Richard Lyimo, Katibu Mkuu wa chama hicho Yustas Rwamugira na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini.
Uamuzi huo umetolewa leo Jumatano Novemba 26,2025 na Jaji Dafina Ndumbaro,aliyekuwa akisikiliza maombi hayo namba 26901/2025 ambapo shauri hilo lilipangwa kwa ajili ya kutajwa.
Waleta maombi waliwakilishwa na Wakili Roland Kimbi huku wajibu maombi wakiwakilishwa na Wakili Baraka Sulus.
Baada ya maombi hayo kutajwa, Wakili Baraka aliieleza Mahakama kuwa maombi hayo ni batili kwa kuwa hayajakidhi matakwa ya kisheria kwa kushindwa kumjumuisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) katika shauri hilo.
Amesema ni takwa la kisheria chini ya kifungu cha 6(3) cha Sheria inayoratibu mashauri au kesi dhidi ya Serikali kinachoelekeza ni lazima kumjumuisha AG, ambaye katika shauri hilo angemwakilisha Msajili wa Vyama vya Siasa.
Wakili huyo aliiomba Mahakama kuondoa maombi hayo mahakamani hadi yatakapotimiza takwa hilo la kisheria, pingamizi ambalo halikupingwa na Wakili wa waleta maombi hayo.
“Shauri limekuja leo kwa ajili ya kutajwa lakini tukaona ni busara ili kuokoa muda wa mahakama, shauri hili ni batili kwani halijakidhi matakwa ya kisheria. Halijakidhi matakwa hayo kwa sababu ni takwa la kisheria pale ofisi ya Serikali inaposhtakiwa lazima umlete mahakamani AG.”
“Kama tunavyofahamu Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ni ofisi ya umma, hivyo ilikuwa ni takwa la kisheria la lazima kumjumuisha AG ili aweze kumwakilisha Msajili wa Vyama vya Siasa,” ameongeza.
Baada ya hoja hiyo, Jaji Ndumbaro alikubaliana na maombi hayo na kutupilia mbali maombi hayo bila gharama.
Katika maombi hayo, waleta maombi walikuwa wakiiomba Mahakama kuwaruhusu kuwasilisha maombi ya marejeo wakijikita katika maombi mawili ambayo ni mkutano Mkuu wa TLP haukufanyika kwa kufuata misingi ya katiba ya chama hicho, hivyo kufanya uchaguzi huo kuwa batili.
Nyingine ni viongozi waliochaguliwa kuwa batili akiwemo Mwenyekiti wa Taifa kwani akidi ya mkutano huo haikutimia na baadhi ya wajumbe walioshiriki hawakuwa halali, hivyo kuwasilisha maombi hayo ili wafanye marejeo.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya Mahakama hiyo, Wakili Kimbi ameeleza kuwa baada ya uamuzi huo hatua itakayofuata ni kurejesha maombi hayo tena mahakamani hapo baada ya kukidhi matakwa ya kisheria.
Lyimo aliyekuwa Katibu Mkuu wa TLP, alichaguliwa Februari 5,2025, katika nafasi ambayo ilikuwa ikikaimiwa na Hamad Mkadamu baada ya Agustino Mrema kufariki dunia Agosti 21,2022.
Mkutano huo ulifanyika jijini Dar es Salaam ambapo pia ulihudhuriwa na Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza.
Mkutano huo pia uliridhia kuwafuta uanachama wanachama 21 wa chama hicho wakiwemo viongozi waliodaiwa kufanya majaribio ya kuandaa mikutano miwili ya kuchaguana ili kuziba nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Mwenyekiti, marehemu Mrema kinyume na katiba ya chama hicho.