Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba ametoa onyo kwa watumishi wa Serikali na wasimamizi wa sera wanaokiuka kanuni za usalama barabarani, akisema mwenendo huo unachochea ‘kutokuwa na usawa’ katika utekelezaji wa sheria baina yao na wananchi wa kawaida.
Amesisitiza kanuni za usalama barabarani nchini Tanzania zinawahusu watu wote kwa usawa na hazipaswi kutekelezwa kwa upendeleo.
Ajali zinazohusisha magari ya Serikali zinaonekana ni jambo la kawaida nchini zikiendelea kusababisha vifo na hasara, huku baadhi ya madereva wakijiona wako juu ya sheria na hivyo hawastahili kuchukuliwa hatua.
Kutokana na hali hiyo, askari wa usalama barabarani wameripoti changamoto katika kuwaadhibu madereva wa magari yenye namba za Serikali, hali inayowafanya kuwa miongoni mwa wanaokiuka sheria za usalama barabarani kwa kiwango kikubwa.
Kupitia kauli ya Mwigulu alipokuwa akizungumza leo Jumatano, Novemba 26, 2025 wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Usafiri Endelevu Ardhini, inaonekana huenda Serikali imeanza kulichukulia suala hili kwa uzito.
“Natoa maelekezo kwa Wizara ya Uchukuzi na wadau husika kupitia sheria zetu na kubaini kama kuna zilizopitwa na wakati au hazitoshelezi. Kama zinahitaji marekebisho, yafanyike. Lakini kama bado zinatosha, basi ni lazima kila mtu aziheshimu,” amesema.
Dk Mwigulu pia amewakosoa baadhi ya madereva wa Serikali wanaopuuza sheria za usalama barabarani, licha ya kuwa kanuni hizo zilipendekezwa na kuidhinishwa na taasisi za Serikali.
“Hakuna aliye juu ya sheria. Wizara husika, polisi na wadau wengine wa usafiri lazima wahakikishe kanuni zote za usalama barabarani zinatekelezwa kwa haki na bila upendeleo,” amesema.
Ameeleza masikitiko yake kwamba baadhi ya maofisa wa Serikali wamekuwa miongoni mwa wanaoongoza kwa makosa ya barabarani.
“Mtu yeyote atakayekiuka sheria lazima akumbane na hatua stahiki,” ameongeza.
Waziri Mkuu amesifu kaulimbiu ya mwaka huu ya maonyesho hayo, Nishati Safi na Ubunifu katika Usafirishaji’, akibainisha kuwa inatoa mwelekeo sahihi wa kuboresha huduma za usafiri ili ziwe salama zaidi, zenye ufanisi, na rafiki kwa mazingira.
Maadhimisho hayo yaliyoanza Novemba 24 yatahitimishwa Novemba 29, 2025.
Amesema kuwa kutumia teknolojia mpya na vyanzo mbadala vya nishati kama umeme, gesi na nguvu za jua kutaboresha ufanisi na kupunguza gharama za usafiri.
Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema ubunifu na teknolojia sasa vinapewa kipaumbele katika sekta ya usafiri na usafirishaji nchini.
Profesa Mbarawa amewahimiza wawekezaji wa ndani na nje kuunga mkono Reli ya Kisasa (SGR), hususan katika ununuzi wa injini, akibainisha Serikali imefungua fursa za ushirikiano na sekta binafsi.
Ameongeza kuwa hatua hiyo itawawezesha wadau kubadilishana mawazo, kutathmini maendeleo na kukuza huduma za usafiri zenye ubunifu, zinazoongozwa na teknolojia na rafiki kwa mazingira.
Amesema wizara itaendelea kushirikiana kwa karibu na wadau, hususan katika kusukuma matumizi ya nishati safi.
“Tunaendelea kuwakaribisha wadau wa ndani na nje, ikiwemo taasisi za maendeleo na taasisi za ubunifu, kushirikiana na serikali kadri tunavyosonga mbele katika matumizi ya nishati safi na teknolojia za kisasa katika usafiri endelevu,” amesema.
Ametaja mafanikio mbalimbali, yakiwemo SGR inayoendeshwa kwa umeme na mfumo wa Mabasi ya Mwendo Kasi (BRT) unaotumia gesi asilia katika njia ya Mbagala.
Ameongeza kuwa wamiliki wadogo wa teksi na waendeshaji bajaji wameanza kutumia gesi asilia, hatua ambayo ni muhimu kuelekea usafiri endelevu.
Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Habibu Suluo, amesema sekta ya usafiri wa ardhi nchini Tanzania inaendelea kubadilika, ikiwa na maboresho katika usalama, mifumo ya kidijitali na ushirikiano kati ya wasimamizi na watoa huduma.
“Watoa huduma sasa wanaweza kufanya kazi zao kwa uhuru na kujiamini,” amesema Suluo, akibainisha mafanikio kama kurejeshwa kwa kibali cha safari za saa 24, hatua iliyotekelezwa kwa mara ya kwanza baada ya zaidi ya miaka 20.
“Sasa Watanzania wanaweza kusafiri muda wowote, wakiwa na uhakika kamili wa usalama,” amesema.
