Dodoma. Wakati Jeshi la Polisi, likiendelea kuchunguza kifo cha Said Kabuga, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), aliyefariki dunia kwa kutumbukia kisimani, baadhi ya wenzake wameeleza awali alionekana mwenye mawazo akitaja fedha alizotumia kubeti.
Kabuga, mwanafunzi wa mwaka wa pili chuoni hapo, pia anatajwa kwamba alikuwa mpole na mkimya, hakupenda kujichanganya na wenzake, na hakuwa mhudhuriaji mzuri wa vipindi darasani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gallus Hyera, amesema taarifa za awali zinaonesha mwanafunzi huyo alijitupa kisimani.
Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo, Jumatano, Novemba 26, 2025, ikielezwa simu na vifaa vingine vimekutwa juu ya kisima hicho.
“Ni kweli taarifa hizo tunazo, lakini kinachoonesha ni kwamba alijitupa kisimani mwenyewe kwa kujiandaa, na bado kuna mambo tunayachunguza,” amesema Kamanda Hyera.
Akizungumza na Mwananchi, Ally Waziri, aliyekuwa karibu na Kabuga, amesema alikuwa mkimya na mwenye marafiki wachache, jambo ambalo huenda likawa sababu ya kutokufahamika kwa wanafunzi wengi.
“Ni rafiki yangu, nilifahamiana naye jeshini. Aliniambia ni mwenyeji wa Mkoa wa Tanga. Hakuwa na marafiki wengi kutokana na haiba ya upole aliyokuwanayo,” amesema.
Waziri amesema jana, Novemba 25, alionekana mchangamfu, lakini baadaye jioni alibadilika akawa mtu mwenye mawazo.
“Naomba msiniandike jina langu, lakini jamaa alibeti jana fedha za ada, na baadaye alianza kulalamika kuwa itakuwaje kwa wazazi wake. Hata chakula cha jioni hakula kutokana na hofu,” amesema mmoja wa wanafunzi.
Amesema mwenzao (Kabuga) alitoka usiku, wakati wamelala, akaenda eneo la kisima kilicho jirani, akaweka vifaa vyake na kujitumbukiza.
Kwa upande wake, Ally Amani amesema alimuona Kabuga akielekea kisimani, huku akimulika kwa kutumia tochi ya simu akiwa na shati begani bila kifaa cha kubebea maji.
Amesema kwa kawaida watu wanaokwenda kuchota maji kisimani hapo huwa na vyombo vya kuyabeba.
Muda mfupi baadaye, amesema alisikia kelele, hivyo alishuka kutoka ghorofani na kuekekea kisimani, ambako alikuta simu na vifaa vya kusikilizia muziki vikiwa nje ya kisima hicho, huku mwanafunzi huyo akiwa ametumbukia ndani.
“Nilipofika pale, nilikuta simu, shati na vifaa vya kusikilizia muziki, ila yeye hakuwapo. Nikaenda kutoa taarifa kwa walinzi,” amesema.
Amesema baada ya walinzi kupata taarifa, walijaribu kumuokoa, lakini walishindwa kutokana na wingi wa maji kwenye kisima, baada ya muda, askari walifika na kuopoa mwili wake.
Mkurugenzi wa Uhusiano UDOM, Rose Mdime, amesema kifo cha mwanafunzi huyo wamekipokea kwa mshtuko na simanzi.
Amesema hawezi kusema mengi, kwani wameliachia Jeshi la Polisi liendelee na uchunguzi.
“Tunatoa pole kwa familia, wazazi na wanafunzi wenzake kuhusu kifo hicho. Tunaomba wanafunzi wawe wapole na waliachia Jeshi la Polisi kufanya kazi yao,” amesema.
Kabuga alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa pili, akisoma Shahada ya Uandishi wa Habari na Uhusiano wa Umma.
