Simba yaifuata Stade Malien na matumaini kibao

SIMBA inatarajiwa kuondoka alfajiri ya kesho Alhamisi Novemba 27, 2025 kwenda Bamako nchini Mali kuwahi pambano la pili la Kundi D la Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Stade Malien, huku mastaa wa timu hiyo wakiwa na matumaini makubwa ya kufanya vizuri baada ya awali kuanza na kichapo nyumbani mbele ya Petro Atletico.

Simba inaondoka na karibu mastaa wote tegemeo, ikiwaacha baadhi ya wachezaji wakiwamo wale majeruhi na wenye matatizo binafsi ambao ni Kibu Denis, Awesu Awesu, Abdulrazak Hamza, kipa Moussa Camara, huku kiungo Mohamed Bajaber akiwa katika hatihati ya kuondoka.

Wawakilishi hao wa Tanzania walianza vibaya mechi za makundi la kufungwa bao 1-0 na Petro Atletico ya Angola wikiendi iliyopita na sasa inaenda kukutana na Stade Malien iliyolazimisha suluhu ugenini dhidi ya wababe wa Afrika, Esperance ya Tunisia, wiki iliyopita jijini Tunis.

Kwa mujibu wa mmoja wa viongozi wa Simba ni kwamba, kikosi karibu chote kipo freshi na kocha ameteua wachezaji wa kuondoka nao ambao ni tegemeo isipokuwa wale wenye matatizo binafsi na majeruhi, huku Bajaber aliyekuwa kwenye msafara ikielezwa alikuwa hatihati kusafiri.

“Bajaber amepatwa na dharura asubuhi ya leo na kulikuwa na hatihati ya kuungana na wenzake, japo jina lake lilikuwa miongoni mwa wachezaji wanaotakiwa kusafiri, ila wengine wapo freshi isipokuwa wenye dharura binafsi na majeruhi,” kimesema chanzo hicho.

Kwa wanaokumbuka katika mechi iliyopita, kiungo Yusuf Kagoma hakuwepo kabisa katika kikosi kilichocheza na kuzua sintofahamu labda ni majeruhi, lakini daktari wa timu hiyo, Edwin Kagabo amethibitisha hakuna kitu kama hicho na kwamba alikuwa mazoezini na wenzake.

“Kagoma leo alikuwepo mazoezini na hana majeraha yoyote na ameshirikiana na wenzake mwanzo mwisho kabla ya kocha kutoa muda wa maandalizi ya safari,” amesema Dk Kagabo na kuongeza kuwa, hana rekodi mpya ya majeruhi ukiondoa wale wa awali yaani kina Camara na Hamza.

“Ninachofahamu mimi wachezaji wote wako fiti kwa ajili ya kufanya majukumu yao, kwa kweli sina taarifa yoyote mpya zaidi ya walewale wa mwanzo.”

Kagoma mwenyewe kathibitisha kuwa sio majeruhi kama ilivyodhaniwa na kukosekana katika mechi iliyopita ni mipango ya kocha tu na hilo ni jambo la kawaida katika timu yoyote.

Simba itavaana na Stade Malien, ikisaka ushindi ili kuepuka kuyarudia yale iliyokumbana nayo msimu wa 2022-2023 ya Ligi ya Mabingwa hatua ya makundi kwa kupoteza mechi mbili mfululizo dhidi ya AC Horoya ya Guinea kwa bao 1-0 na Raja Casablanca ya Morocco (3-0).