Mashujaa, Dodoma vita nzito leo

LIGI Kuu Bara inaendelea leo kwa mechi moja kupigwa Uwanja wa Lake Tanganyika, mjini Kigoma kwa wenyeji Mashujaa kuikaribisha Dodoma Jiji katika pambano la kisasi kutokana na rekodi za timu hizo mbili katika ligi hiyo.

Mashujaa iliyotoka kupata ushindi wa bao 1-0 nyumbani mechi iliyopita dhidi ya Mbeya City, inakutana na Dodoma iliyotoka kupasuka kwa mabao 2-0 mbele ya Namungo, huku rekodi za timu hizo katika ligi misimu miwili iliyopita ikishindwa kuchekana.

Msimu uliopita uliokuwa wa pili kwa Mashujaa kucheza Ligi Kuu, ilishinda kwenye uwanja huo wa nyumbani bao 1-0, lakini ikapasuka 3-1 ugenini likiwa ni pambano la mwisho kukutana likipigwa Desemba 28 mwaka jana.

Kabla ya hapo mara Mashujaa ilipopanda daraja ilianza kwa sare ya 1-1 ugenini dhidi ya Dodoma kabla ya kushinda nyumbani kwa mabao 3-0, japo linalotoa picha pambano la leo ni gumu kutabirika, licha ya rekodi kuwabeba wenyeji wakicheza Lake Tanganyika.

LIGI 02

Kocha Salum Mayanga ataendelea kuwategemea nyota kama Jaffar Kibaya alioyefunga mechi iliyopita, David Ulomi, Crispin Ngushi na wengine ili kukabiliana na Dodoma Jiji yenye mastaa wakali kama Abdi Banda, Idd Kipagwile, Salmin Hoza, David Mwanakikuta kusaka pointi tatu.

Kimahesabu haitakuwa mechi rahisi kwa timu zote, licha ya kwamba Dodoma imetoka kupoteza ugenini mbele ya Namungo na ikihitaji ushindi ili kuondoka nafasi ya 15 iliyopo kwa sasa ikiwa na pointi tano baada ya mechi saba tofauti na Mashujaa yenye pointi 11 ikicheza pia mechi saba.

Hata hivyo, inapaswa kufanya kazi ya ziada mbele ya wenyeji kwani Mashujaa haijapoteza nyumbani katika mechi nne zilizopita, lakini Dodoma ikiwa n rekodi mbaya kwa mechi za ugenini ikiwa haijapata ushindi hata moja kati ya nne ilizocheza ikichapwa tatu na kupata sare moja.

LIGI 0

Mapema Kocha wa Dodoma, Amani Josiah alikaririwa mechi nne aliyoiongoza timu hiyo imempa mwanga wa kujipanga kwa pambano hilo la ugenini, akitegemea wachezaji wa kikosi hicho hawatafanya makosa kama yaliyowagharimu mechi iliyopita dhidi ya Namungo na kulala 2-0.

Kwa upande wa kocha Mayanga, amesema ameliandaa vyema jeshi hilo la Mashujaa kuendelea pale ilipoishia, lakini akili zikiwa ni kuona inaongeza dozi tofauti na mechi zilizopita ilipoambulia ushindi usiozidi bao moja.

Mashujaa katika mechi saba imeshinda tatu, kutoka sare mbili na kupoteza mbili mbele ya Pamba Jiji iliwafunga mabao 2-1 na kupigwa 1-0 na Singida Black Stars zote zikipigwa ugenini, huku Dodoma yenyewe imeshinda mechi moja tu na kupoteza nne na kutoka sare mbili, ikifunga mabao manne na kufungwa tisa tofauti na wenzao waliofunga matano na kufuingwa manne.