Himid Mao freshi, Aziz KI apewa saa 24

PRESHA kubwa kwa viongozi wa Azam na Wydad ilikuwa ni hatma ya afya ya viungo wao, Himid Mao na Stephanie Aziz KI waliogongana katika mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika baina ya timu hizo iliyochezwa jana Ijumaa Novemba 28, 2025 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar na kulazimika kutolewa uwanjani dakika ya 76, kisha kukimbizwa hospitali.

Taarifa iliyotolewa na Wydad, imesema Aziz KI alipata maumivu ya kichwa na akashindwa kutembea kutokana na kugongana na Himid katika mechi hiyo ambayo Azam ilipoteza kwa bao 1-0.

Taarifa hiyo imesema baada ya kiungo huyo kuwahishwa hospitali na kupatiwa matibabu, amepewa saa 24 ya kuwa chini ya uangalizi huku madaktari wakiendelea kufuatilia maendeleo yake. Kwa upande wa Himid, baada ya kuwahishwa hospitali, jana asubuhi aliruhusiwa kutokana na afya yake kutengemaa.

Akizungumza na Mwanaspoti, Aziz Ki amesema hakuwa anona kitu baada ya kuanguka chini kutokana na tukio hilo la kugongana.

Kiungo huyo wa zamani wa Yanga, amethibitisha kwamba anaendelea vizuri akiweza kutambua mambo mbalimbali kwa macho tofauti na ilivyokuwa kabla.

“Kwasasa naendelea vizuri, namshukuru Mungu, sikuwa natambua kitu wakati nilipoanguka, lilikuwa tukio baya kwangu,” alisema Aziz KI.

“Nawashukuru madaktari walihakikisha nakuwa sawa, kiukweli niliogopa sana, nafurahi timu yangu ilishinda,” amesema Aziz KI.

Naye Daktari wa Azam, Mbarouk Mlinga, amesema Himid ambaye aliwahishwa hospitali, maendeleo yake yako vizuri baada ya kuruhusiwa kutoka hospitali.

“Afya ya Himid inaendelea vizuri, tunawashukuri sana madaktari wa huduma ya kwanza pale uwanjani kwa kazi nzuri waliyofanya, alipofikishwa hospitali alifanyiwa vipimo vyote stahiki,” amesema Mlinga.

“Tunadhani alipata mtikisiko kutokana na kugongana, lakini anaendelea vizuri na bahati nzuri ameruhusiwa kutoka hospitali, tunaamini tutakapoanza mazoezi yetu naye atakuwa sawa kuendelea na majukumu yake.”