Damu ya bubu yamponza, ahukumiwa kunyongwa hadi kufa

Arusha. Damu ya bubu yamponza. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Dodoma kumhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa, Augustino Kenan, aliyekutwa na hatia ya mauaji ya Michael Mwimbwa.

Mahakama hiyo imewaachia huru washtakiwa wengine wawili, Emmanuel Joseph maarufu kama Ngosha na Emmanuel Efraim maarufu kama Bravoo, baada ya kuwakuta hawana hatia katika kesi hiyo ya mauaji.

Wote watatu walishtakiwa kwa mauaji kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, kosa walilodaiwa kutenda Februari 9, 2023 ambapo mwili wa marehemu ulikutwa katika shamba la Shule ya Msingi Manyoni mkoani Singida.

Mbali na ushahidi wa kimazingira, Mahakama hiyo ilimtia hatiani mshtakiwa huyo kutokana na maelezo yake ya onyo aliyoyatoa polisi ambapo Mahakama imenukuu sehemu ya maelezo hayo ambayo Augustino alikiri walishirikiana kumuua Michael kwa madai kuwa mshtakiwa wa tatu ambaye ni mfanyabiashara alihitaji damu ya bubu, hivyo walipomtafuta bubu walimpata Michael.

Alieleza kuwa walimvamia na kumkaba shingo yake na kwenda naye katika shamba la mahindi la shule ya msingi Manyoni na kisha kumpiga na kitu kizito na kisha kumkata kisogoni na juu ya jicho la kushoto kwa panga na baada ya kumuua walimvunja shingo yake.

Hukumu hiyo imetolewa na Jaji Evaristo Longopa Novemba 27, 2025 na nakala yake kuwekwa kwenye mtandao wa Mahakama.

Jaji Longopa amesema baada ya kupitia ushahidi wa pande zote mbili, Mahakama imemkuta Augustino na hatia huku ikiwaachia huru washtakiwa wenzake wawili baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha kesi dhidi yao, ambapo kupitia ushahidi wa kimazingira uliotolewa umeshindwa kuwaunganisha na mauaji hayo.

Wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, upande wa Jamhuri ulikuwa na mashahidi saba na vielelezo viwili ambapo uliwakilishwa na mawakili watatu huku utetezi ukiwakilishwa na mawakili wanne.

Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa Augustino alikamatwa Aprili 7, 2023, Ngosha na Bravoo wakikamatwa Aprili 8, 2023.

Shahidi wa kwanza alidai mshtakiwa wa kwanza alipokamatwa na kuhojiwa alikiri kutenda kosa hilo.

Shahidi wa pili, Thomas Mwimbwa alidai Februari 9, 2023 alipata taarifa za mauaji ya kaka yake ambapo Februari 10, 2023 alienda kuutambua mwili wake katika hospitali ya Wilaya ya Manyoni na kushuhudia ukiwa na majeraha ya kukatwa, mawili yakiwa kwenye jicho la kushoto na nyuma ya kichwa.

Shahidi wa tatu, Simon Mgumba alidai siku ya tukio alipata taarifa za kuwepo kwa maiti ya mwanaume karibu na shamba la Shule ya Msingi Manyoni ambapo alienda eneo la tukio na kushudia mwili ukiwa uchi na ulionekana kuwa umepigwa usoni na kichwani.

Shahidi wa nne, Salum Abdallah ambaye aliufanyia uchunguzi mwili huo, alieleza kuwa aliufanyia mwili huo uchunguzi kuanzia kwenye unyayo hadi kichwani na kuwa ulikuwa na majeraha makubwa mawili upande wa jicho la kushoto na lingine nyuma ya kichwa.

Alidai kuwa majeraha yalikuwa yakionyesha kuwa fuvu lilikuwa limepinda na shingo ilikuwa imenyongwa na kuhitimisha kuwa chanzo kilikuwa ni kupoteza damu nyingi kutokana na kupigwa na kitu kizito.

Shahidi wa tano, F5775 Sajenti Raphael, aliyemhoji mshtakiwa wa kwanza Aprili 7, 2023 alifanya maandalizi muhimu ya chumba kwa ajii ya mahojiano na kumjulisha mshtakiwa kuhusu haki zake ikiwemo kukaa kimya, kumwita ndugu au wakili na kuwa mshtakiwa alikubali kuandika maelezo ya onyo bila kuwa na ndugu au wakili.

Alieleza baada ya kukamilika kurekodi maelezo hayo mshtakiwa alisomewa na kuthibitisha kuwa ni sahihi na alisaini kwa alama ya dole gumba na kuwa alikiri kuhusika na mauaji hayo ambapo alisimulia namna kosa lilivyotendwa.

Shahidi wa sita, Masatu Magesa ambaye ni Hakimu wa Amani, alieleza kuuwa Aprili 11, 2023 aliandika maelezo ya ziada ya Augustino baada ya kutimiza matakwa yote na baada ya kurekodi alisoma yaliyomo kwa mshtakiwa kabla ya kusaini na kuwa alikiri katika maelezo hayo kuwa alitenda kosa hilo.

Shahidi wa saba, alieleza mahakama kuwa aliwahoji washtakiwa wa pili na wa tatu ambao wote walikana kutenda kosa hilo na kuwa Augustino pekee ndiye alikiri kutenda kosa hilo huku akidai kushirikiana na wenzake.

Akijitetea mahakamani hapo, Augustino alidai kuwa alikamatwa kwa nguvu na askari akiwa nyumbani kwake ambao walipekua chumba chake, wakachukua simu mbili za mkononi, mali yake na mkewe, wakamfunga pingu na kumpeleka Kituo cha Polisi Manyoni.

Alidai kupelekwa chumba cha mahojiano ambapo alilazimishwa kusaini nyaraka nyingi ambazo hakujua kilichokuwa kimeandikwa ndani yake na kuwa Aprili 13, 2023 alipelekwa Mahakama ya Mwanzo Itigi ambapo alijulishwa kuhusu tuhuma za mauaji ambazo alikana.

Aidha, aliieleza mahakama kuwa hakuwahi kiwataja popote washtakiwa wenzake na kuomba kuachiliwa huru kwani tuhuma dhidi yake hazikuwa za kweli.

Mshtakiwa wa pili (Ngosha), aliieleza mahakama kuwa alikamatwa Aprili 8, 2023 akiwa katika eneo lake la biashara, askari polisi watatu waliokuwa wamevaa nguo za kawaida ambao walichukua simu zake mbili, kumfunga pingu pamoja na fedha zake Sh270,000.

Alidai kuwa kabla ya kufikishwa mahakamani hakuwahi kujulishwa kosa linalomkabili na kukana kutowafahamu washtakiwa wenzake na kuiomba Mahakama imwachie huru kwani tuhuma dhidi yake si za kweli.

Mshtakiwa wa tatu, alidai kukamatwa na askari polisi bila kujua sababu ya kukamatwa kwake kwa siku kadhaa na kukana kuwafahamu washtakiwa wenzake na kuiomba Mahakama kumuachia huru kwani hakuna ushahidi wowote dhidi yake.

Jaji Longopa amesema baada ya kusikiliza pande zote mbili, Mahakama hii itaangalia iwapo upande wa mashtaka umethibitisha kesi hiyo pasipo kuacha shaka.

Amesema katika kesi za jinai ni wajibu wa jamhuri kuthibitisha kosa hilo kwa kiwango kisichotia shaka, ambayo ni masharti ya kifungu cha 3(2) (a) cha Sheria ya Ushahidi.

Jaji Longopa amesema baada ya ukaguzi wa kina wa ushahidi kwenye kumbukumbu katika kesi hii, hakuna shahidi wa Jamhuri aliyeona mauaji hayo yakitomea na kuwa ushahidi pekee ni wa kimazingira.

“Katika kesi hii, ushahidi pekee wenye nguvu unaopatikana ni ungamo la mshtakiwa wa kwanza, ambalo ni kukiri kosa ambapo pamoja na mambo mengine, aliwataja washtakiwa wenzake kuwa walishiriki kutenda kosa la mauaji. Hakika, sheria inatambua matumizi ya ungamo la kosa kutumika kama msingi wa hatia,” amesema.

Jaji amesema mbali na ushahidi uliomo kwenye maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa kwanza, hakuna ushahidi mwingine wowote wa kujitegemea kwenye rekodi unaomhusisha mshtakiwa wa pili na wa tatu kwa madai ya kutenda kosa.

“Hakuna hata mmoja kati ya mashahidi wote saba wa upande wa mashtaka aliyetoa ushahidi mwingine wowote unaothibitisha ushiriki wa mshtakiwa wa pili na wa tatu katika kutenda kosa hilo. Katika mazingira hayo, kiungo hiki kinatosha kuwaondolea hatia mshitakiwa wa pili na wa tatu kutokana na kosa walilofikishwa mbele ya Mahakama hii,” amesema.

Baada ya kupitia hoja za pande zote, Mahakama hiyo ilimhukumu Augustino kunyongwa hadi kufa huku ikiwaachia huru washtakiwa wenzake wawili kutokana na ushahidi dhidi yao kuwahusisha na kosa hilo kutothibitishwa.