Uturuki. Papa Leo XIV ametembelea Msikiti wa Sultan Ahmed, unaojulikana pia kama ‘Blue Mosque’ uliopo Instabul nchini Uturuki.
Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki Duniani amefanya ziara hiyo leo Jumamosi Novemba 29, 2025 ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku tatu nchini humo.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Vyombo vya Habari ya Vatican, “Papa amefanya ziara hiyo kwa ukimya, katika hali ya utulivu na usikivu, kwa heshima ya kina kwa mahali hapo na kwa imani ya wale wanaokusanyika humo kwa sala.”
Papa aliwasili kwenye msikiti huo leo Jumamosi asubuhi akiwa amefuatana na Waziri wa Utamaduni na Utalii, Mehmet Nuri Ersoy; Mufti wa Mkoa wa Istanbul, Emrullah Tuncel na Imamu wa Msikiti wa Sultan Ahmed, Kurra Hafiz Fatih Kaya. Ndani ya msikiti, muezzin Musa Aşgın Tunca alimwongoza Papa katika matembezi mafupi kujionea mandhari ya msikiti.
Msikiti huo ambao ni moja ya misikiti maarufu katika jiji la Istanbul, ulijengwa mwaka 1617 na Sultan Ahmed I katika sehemu ya eneo lililokuwa Makao Makuu ya kale ya Constantinople.
Lengo lilikuwa msikiti huu uwe mahali patakatifu muhimu zaidi katika Dola ya Uthmaniyya. Nyaraka nane, ambazo sasa zinahifadhiwa katika Maktaba ya Topkapi, zilieleza hatua mbalimbali za ujenzi wake.
Zaidi ya vigae 21,000 vinavyopamba kuta za jengo hilo, vingi vyenye rangi ya buluu na samawati, ndivyo vilivyolipa msikiti huo jina maarufu la Blue Mosque.
Papa baada ya kutembelea Blue Mosque, atafanya kikao cha faragha na viongozi wa Makanisa ya eneo hilo na jumuiya za Kikristo katika Kanisa la Kiorthodoksi la Kisyriani la Mor Ephrem.
Kiongozi huyo anakuwa Papa wa tatu kutembelea Blue Mosque, akiifuata nyayo za watangulizi wake wa karibu, Papa Francis (2014) na Benedict XVI (2006).
Ziara ya Benedict ilikuwa mara ya pili tu katika historia kwa Papa kutembelea msikiti, baada ya ziara ya kihistoria ya Yohane Paulo II katika Msikiti wa Umawiyya mjini Damascus wakati wa Safari yake ya Kitume nchini Syria mwaka 2001.
Pia leo ataungana katika ibada ya Doxology pamoja na Patriarki Mkuu wa Kiorthodoksi wa Kiekumene, Bartholomew I wa Constantinople katika Kanisa la Kipatriarki la Mtakatifu George, Baba Mtakatifu.
