KOCHA wa Singida Black Stars, Miguel Gamondi, amesema hawazi sana kuhusu presha ya mechi ya kesho dhidi ya Stellenbosch, huku akiweka wazi kwamba kiungo Khalid Aucho atacheza.
Mechi ya kwanza ambayo Singida Black Stars ilifungwa 2-0 ugenini na CR Belouzidad, Aucho hakuwepo huku ikielezwa alichelewa kupata visa ya kuingia Algeria akitokea kwenye majukumu ya timu ya taifa, lakini Gamondi amethibitisha kesho atakuwa sehemu ya kikosi kinachocheza dhidi ya Stellenbosch.
Singida Black Stars kesho Jumapili Novemba 30, 2025, itaikaribisha Stellenbosch kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar ikiwa ni mechi ya pili Kundi C katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ikitarajiwa kuanza saa 1:00 usiku.
“Aucho ni mchezaji ambaye atakwepo kwenye mchezo wa kesho, ni ngumu kusema hatakuwepo kwani ana uzoefu mkubwa na ni mchezaji mkubwa.
“Uwepo wa wachezaji kama Aucho na wengine wenye uzoefu wanaongeza upana wa timu kufanya vizuri, kwa hiyo tutegemee makubwa kwa sababu wamefanya mazoezi ya kutosha.”
Mbali na hilo, Gamondi amesema jambo la msingi kwenye mechi hiyo ni kusahihisha makosa yao, japokuwa sio rahisi lakini watapambana kupata matokeo mazuri.
“Kuwa na presha ni suala la hofu kwa wale ambao ni wageni kwenye hii michuano, licha ya kwamba tunawaheshimu sana wapinzani wetu, lakini tumejipanga kushinda.
“Kuwa nyumbani ni suala la kwanza na kupata matokeo mazuri ni suala lingine, lakini kikosi kipo tayari kimbinu ambapo tutakwenda kutumia nafasi zote tutakazopata.
“Namjua kocha wa wapinzani na ananijua, hivyo mechi itakuwa ya kimbinu kwelikweli, ila tutacheza kikubwa kwa kutengeneza nafasi na kuzitumia,” alisema Gamondi ambaye msimu wa 2023-2024 aliifikisha Yanga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa kocha wa kikosi hicho kabla ya 2024-2025 kuifikisha makundi, lakini akaondolewa kabla ya mechi za hatua hiyo hazijaanza kuchezwa.
