Room to Read lataja suluhu ya vikwazo vya kielimu kwa wasichana

Kwa miaka mingi mtoto wa kike amekuwa akibaki nyuma kielimu kutokana na mila, tamaduni, changamoto za kifamilia, mfumo dume, umaskini na ukosefu wa miundombinu rafiki shuleni. 

Wengi hukumbana na vikwazo kama kukosa vifaa vya kujisitiri wanapofika usichana, kukosa uhuru wa kuhudhuria vipindi, ndoa na mimba za utotoni, pamoja na ukatili wa kijinsia. 

Hali hii hupunguza uwezo wao wa kujifunza, kujiamini na kutimiza malengo yao.

Ni katika mazingira haya ndipo shirika la kimataifa Room to Read, linalojikita kukuza stadi za kusoma, kuandika na kuwawezesha wasichana kielimu, limekuwa msaada muhimu. 

Kwa Tanzania, shirika hili limefanya kazi kwa zaidi ya miaka 13 likishirikiana na Serikali, halmashauri, shule na jamii ili kuhakikisha mtoto wa kike anapata fursa sawa, mazingira salama na programu zinazomjengea uongozi, stadi za maisha na kujiamini.

Mwananchi limefanya mahojiano na Mkurugenzi mkaazi wa shirika hilo kwa hapa nchini,  Joan Minja, anayeeleza hali ya elimu kwa wasichana na mfumo mzima wa utoaji elimu nchini.

Swali: Tueleze historia ya shirika la Room to Read?

Jibu: Shirika la Kimataifa la Room to Read lilianzishwa takriban miaka 25 iliyopita. Ilikuwa ni ndoto ya mtu mmoja raia wa Marekani aliyekwenda India kupumzika na safari yake ikabadilika kuwa mwamko mkubwa wa kijamii.

Akiwa huko alikutana na mwanamama mmoja akiwa na mtoto wake, akijaribu kumsomea vitabu ambavyo havikuwepo.

Walipoongea, yule mama alionesha kuwa anahitaji vitabu kwa ajili ya kumsaidia mtoto wake. Mwanzilishi wetu alianza kumtumia vitabu, lakini baadaye aligundua kuwa vitabu peke yake havitoshi, mtoto anahitaji mazingira rafiki, hususan chumba cha kusomea kama maktaba.

Hapo ndipo lilizaliwa wazo la kuanzisha maktaba katika jamii zenye uhitaji. Baada ya muda waliona pia kwamba vitabu havitakuwa na maana iwapo watoto hawatajua kusoma na kuandika. Ndipo wakaamua kuingia kwenye mifumo ya elimu moja kwa moja. Wakakubaliana kutumia lugha ya nchi husika, kuandaa vitabu vya hadithi vinavyoendana na utamaduni wa eneo husika, kutoa mafunzo kwa walimu, na kuibua utamaduni wa usomaji kwa watoto wadogo.

Hapa Tanzania, Room to Read ilianza katika wilaya za Bagamoyo mkoani Pwani na Mvomero mkoani Morogoro.

Swali: Kwa muda mrefu watoto wa kike waliachwa nyuma kielimu. Unazitazamaje juhudi za kuwaendeleza hivi sasa?

Jibu: Ni kweli kabisa, mtoto wa kike aliachwa nyuma kwa miaka mingi na kumekuwa na juhudi nyingi zinazofanywa na serikali na wadau kuhakikisha anapata haki yake ya elimu licha ya changamoto anazokutana nazo.

Sisi Room to Read ni mfano wa mashirika yasiyo ya kiserikali yanayojitahidi kuhakikisha msichana anapata haki hiyo. Serikali nayo imeweka kipaumbele kuhakikisha watoto wote wanakwenda shule bila ubaguzi.

Uandikishaji wa wanafunzi unaonyesha usawa wa kijinsia umekuwa ukizingatiwa.

Hata hivyo, pamoja na jitihada hizi, bado mtoto wa kike anahitaji msaada zaidi. Ana mahitaji ya kipekee yanayoweza kumfanya ashindwe kuhudhuria masomo kama mtoto wa kiume.

Kwa mfano, changamoto za kibaiolojia zinazosababisha wasichana wengi kukosa shule siku tano hadi saba  kila mwezi. Tunaona haja ya jamii kuelimishwa kuhusu namna ya kumsaidia msichana na hata wavulana nao.

Pia miundombinu ya shule ni muhimu: je, ina mazingira salama na yenye faragha kwa mtoto wa kike? Vifaa vya kujisitiri vinapatikana? Taulo za kike zinapatikana kwa urahisi?

Hivyo tunasema fursa sawa zipo, lakini fursa kulingana na mahitaji bado zinahitaji kuimarishwa.”

Swali: Ni sababu zipi zinazowarudisha wasichana nyuma kielimu?

Jibu: Sababu kubwa ni mila na tamaduni. Jamii nyingi bado zinamuona mtoto wa kike kama mtaji. Baadhi ya familia huozesha wasichana wakifikia umri wa baleghe na pesa za mahari hutumika kumsomesha mtoto wa kiume. Wanaamini msichana ataenda kutumikia familia ya mume, hivyo kumwekeza kielimu ni hasara.

Ukatili wa kijinsia kama kupigwa, kubakwa au kupewa kazi nyingi nyumbani nao unachangia kushusha ari ya masomo. Wasichana wengi hawana watu wa mfano (role models) wanaowaonesha kuwa inawezekana kufanikiwa.

Kutokana na changamoto hizo, Room to Read tunamjengea msichana stadi za maisha, ustahamilivu, uongozi na fikra tunduizi. Tunataka aweze kukabiliana na changamoto ambazo haziwezi kuepukika kirahisi, mfano umbali wa kwenda shule. Hivyo tunamwekea misingi ya kujiamini na kutambua vipawa vyake.

Swali: Mmekuwa mkihamasisha uwezo wa watoto kusoma na kuandika. Mmefanikiwa kwa kiasi gani kufikia dhamira yenu hiyo?

Jibu: Zaidi ya kuhamasisha, tumekuwa tukijenga uwezo wa walimu kupitia mafunzo ya utendaji, kuanzisha maktaba za kisasa shuleni, na kuandaa vitabu bora vya hadithi kwa lugha ya Kiswahili, vinavyokidhi umri wa watoto.

Tumeandaa matini rejea kwa walimu na tunaendelea kusimamia maktaba zinazosaidia wanafunzi kuboresha stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu. Hadi sasa tumefikia wanafunzi zaidi ya milioni 2 na walimu 19,415.

Tumeanzisha maktaba 392 katika shule za serikali. Kila mwezi tunarudi shuleni kutoa usaidizi endelevu ili kuhakikisha tunapata matokeo bora.”

Swali: Kwa nini Watanzania wanaelezwa kutokuwa na utamaduni wa kujisomea?

Jibu:Hili linatokana na mambo kadhaa:

Kwanza, hatuanzishi utamaduni wa usomaji mapema, tunasubiri mtoto aanze shule ndipo tushinde tukimhimiza.

Pili, tanzu ya uandishi haijawekewa kipaumbele. Waandishi wengi wanaandika kwa kujitolea tu.

Tatu, gharama za vitabu na vifaa vya kujisomea ni changamoto kwa familia nyingi.”

Swali: Nini kifanyike kuwawezesha watunzi wa vitabu ili kufanya kazi zao kwa ufanisi?

Jibu: Kwanza, ni muhimu kuwathamini waandishi. Wakijua kazi yao inathaminiwa, ubunifu huongezeka. Pia wanapaswa kupatiwa mafunzo ya mara kwa mara kuhusu namna ya kuandika vitabu bora kwa watoto.”

Sisi tumewaandaa waandishi kupitia mafunzo ya kila mwaka ya uandishi, uchoraji na mbinu za kuandaa vitabu bora vya watoto. Mpaka sasa tumewafikia waandishi 69. Tumeandaa pia miongozo ya mfumo wa ‘visual’ inayowaonyesha na kuwafundisha kwa vitendo namna ya kuandika vitabu vinavyovutia mtoto.”

Swali: Ni vikwazo gani mmekuwa mkikumbananavyo katika harakati zenu?

Jibu:Vikwazo vikubwa ni mabadiliko ya mara kwa mara ya watendaji serikalini. Unafanya kazi na ofisa elimu leo, baada ya miaka miwili anastaafu au kuhamishiwa sehemu nyingine. Hivyo tunalazimika kuanza upya kuwaeleza malengo na mbinu zetu.

Hata hivyo ushirikiano wa Serikali umekuwa mkubwa na unatupa nguvu kuendelea.”

Swali: Je, unadhani ni hatua sahihi kwa mtalaa mpya kusisitiza kusoma, kuandika na kuhesabu kwa wanafunzi wa darasa la kwanza na pili?

Jibu: Ndiyo. Ili kupata wahandisi, madaktari, marubani na wataalamu wengine, msingi lazima uwe imara. Huo msingi unaanzia katika kujua kusoma, kuandika na kuhesabu. Mtalaa wa sasa umeendana na mabadiliko ya kiulimwengu na unaweka mkazo kwenye ‘Foundation Learning’. Ni hatua muhimu sana.”

Swali: Una maoni gani kwa jumla kuhusu mfumo wetu wa elimu; tunapatia wapi na tunakosea wapi?

Jibu: Kwanza, mabadiliko ya mtalaa wa 2023 ni hatua nzuri, unatoa elimu ya ujuzi na unaziangalia tofauti za wanafunzi. Pia umeongeza mchepuo wa amali ili kusaidia wanafunzi wa fani za ufundi.

Lakini bado tunahitaji vitendea kazi vya kutosha, vitabu vya kutosha, kampeni za kuhakikisha mwanafunzi mmoja anapata kitabu kimoja, pamoja na kuzingatia mahitaji maalum kwa watoto wenye uhitaji maalum.”

Swali: Nini kifanyike ili elimu ya ujuzi  ifanikiwe?

Jibu: Kitu kikubwa ni kuwajengea uwezo walimu tarajali na walimu waliopo kazini. Walimu wakipewa mafunzo ya kufundisha kwa mtazamo wa ujuzi, mfumo huu utafanikiwa. Lazima tuwekeze katika walimu, vifaa, maabara, vitabu na mazingira bora ya kujifunzia.”