Mwenyekiti mpya wa halmashauri ya wilaya ya Biharamulo, Apolinary Mugarula.
Mwenyekiti mpya wa halmashauri ya wilaya ya Biharamulo, Apolinary Mugarula.
Madiwani wa halmashauri ya Biharamulo wakila kiapo.
Msimamizi wa Uchaguzi, ambaye ni Das Biharamulo, Kassim Kirondomara, akitoa ufafanuzi kwa madiwani
Makamu mwenyekiti wa halmashauri ya Biharamulo, Ameria Nyakake.
…………..
BIHARAMULO
DIWANI wa Kata ya Nyakahura, Apolinary Mugarula, ameibuka kidedea katika uchaguzi wa nafasi ya Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera, huku akiahidi kuipaisha halmashauri hiyo kimaendeleo.
Hata hivyo, Diwani wa viti maalumu kata ya Nyarubungo, Amelia Nyakake, amefanikiwa kutwaa nafasi ya makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo.
Mwenyekiti na msimamizi wa mkutano wa Uchaguzi huo, ambaye ni Katibu tawala wa halmashauri ya wilaya ya Biharamulo (DAS) Kassim Kirondomara, amesema kutokana na kanuni na mwongozo wa uchaguzi wa viongozi hao, Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndicho pekee kilichowasilisha majina ya wagombea wa nafasi hizo.
Hatua hiyo inatokana na kata zote 17 za halmashauri ya wilaya hiyo kutwaliwa na CCM katika Uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025.
Akisoma matokeo ya kura zilizopigwa, amesema mgombea wa nafasi ya Uenyekiti wa halmashauri hiyo, Mugarula amepata kura za ndiyo 25 kati ya kura 25 zilizopigwa sawa na aslimia 100
Aidha makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Nyakake amepata kura 25 sawa na aslimia 100 ya kura zote zilizopigwa.
Kutokana na matokeo hayo Msimamizi wa Uchaguzi huo, amemtangaza Mugarula kuwa mshindi wa nafasi ya Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, huku Nyakake akitwaa nafasi ya makamu mwenyekiti.
Akitoa shukrani kwa Madiwani kwa kumpigia kura nyingi za ndiyo, Mugarula ameahidi kuipeperusha halmashauri hiyo kimaendeleo, kusimamia maamuzi ya vikao vya Baraza la Madiwani, na kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kuhakikisha changamoto zilizopo zinatatuliwa kwa haraka zaidi.
Mugarula anachukua kiti cha Uenyekiti, baada ya kumalizika kwa awamu ya aliyekuwa mwenyekiti wa halmashauri hiyo,Leo Rushahu na Diwani wa kata ya Nyanza, baada ya mchakato ndani ya CCM kukamilika na Madiwani hao kufanya Uchaguzi mpya wa mwaka 2025.
Awali Madiwani hao walitanguliwa na kiapo cha uaminifu kilichotolewa mbele ya Hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya mwanzo Biharamulo mjini, Rogasian R. Massawe.
Baraza la Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera, linao Madiwani wanaotokana na Kata 17, Viti maalumu 6, Mbunge wa Jimbo 1 na Mbunge viti maalumu mkoa wa Kagera 1.
Mwisho.



