KOCHA wa Fountain Gate, Mohamed Ismail ‘Laizer’ amesema mechi ya keshokutwa Alhamisi dhidi ya Yanga hawataingia kinyonge bali wataonyesha ushindani mkubwa mbele ya mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara.
Mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara imepangwa kuchezwa keshokutwa Alhamisi saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar na Fountain Gate imetoka kufungwa 2-0 nyumbani na JKT Tanzania, huku Yanga inarejea katika mechi za ligi baada ya kutoka Algeria kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi dhidi ya JS Kabylie na kupata matokeo ya 0-0.
Akizungumza na Mwanaspoti, Laizer amesema amekuwa akiisoma Yanga kwa muda sasa na anaheshimu ubora wao, lakini wanajua kutumia udhaifu waliokuwa nao wakati anakiandaa kikosi hicho na kupambana kimbinu na stamina.
“Mchezo ujao dhidi ya Yanga hautakuwa mgumu kwetu wala mwepesi kwa wapinzani wetu kwa kuwa tumejipanga kutoa ushindani mkubwa, najua wametoka kucheza kimataifa hivyo wako vizuri.
“Sisi kazi yetu ni moja tu kuhakikisha tunatumia kila nafasi tutakazopata. Nimewaanda wachezaji kimbinu na uimara wa miili kwani wanakwenda kucheza na wapinzani wagumu.
“Nimeisoma Yanga kwa muda sasa, nawaheshimu ubora wao, lakini tunajua upungufu wao, kikosi chetu kinakwenda kupambana kimbinu na stamina ya mwili kwenye mchezo huu,” amesema.
