Dar es Salaam. Madiwani 19 wakiwemo wa viti maalumu wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, Dar es Salaam leo Jumanne, Desemba 2, 2025 wamekula kiapo kuwatumikia wananchi huku wakiahidi kuwatafutia fursa za kiuchumi vijana na kina mama.
Sambamba na hilo, suala la maji, barabara, umeme usimamizi wa miradi mipya pia ni ahadi zilizotolewa na madiwani hao katika ofisi za manispaa ya Ubungo zilizopo Luguruni.
Wakiapa mbele ya wananchi waliohudhuria, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo, kamati ya siasa Wilaya pamoja na wageni waalikwa wamesema jukumu lililopo ni kuwatumikia wana Ubungo.
Aidha, katika kikao hicho cha kiapo, Diwani wa Goba, Laurence Mlaki amechaguliwa kuwa Meya wa Manispaa ya Ubungo ambapo amepata kura za ndiyo 19.
Meya Mlaki amesema watabuni vyanzo vya mapato, fursa kwa vijana na kinamama ili wakuwe kiuchumi. Amesema yuko tayari kuwatumikia wanaUbungo kwa moyo wake wote.
“Lengo letu Ubungo kukusanya Sh50 bilioni kwa mwaka tunataka pia kubuni vyanzo vingine vya mapato ili kufikia malengo yetu. Tutatengeneza fursa kwa vijana kinamama waweze kujiajiri ili kuendesha maisha yao,” amesema.
Kwa upande wake, Naibu Meya ambaye ni Diwani wa Manzese, Ally Bakari aliyeshinda kwa kupata kura 19 pia amesema ataleta umoja na mshikamo kwa watu wote wakiwemo madiwani na watumishi.
Ikumbukwe jana Jumatatu, wajumbe wa Chama cha Mapinduzi (CCM), ambao ni madiwani wa Manispaa ya Ubungo walimchagua Mlaki kugombea nafasi ya Mstahiki Meya.
Mlaki sasa anakuwa Meya nafasi iliyokuwa ikitumikiwa na Jaffary Nyaigesha.
Katika uchaguzi huo uliofanyikia ofisi za wilaya za chama hicho alichaguliwa kwa kura 17 huku akiwashinda Zaidi Muliro aliyepata kura moja na Ashura Sengondo aliyepata kura mbili.
Diwani wa Mabibo, Ashura Sengodo amesema atashughulikia changamoto mbalimbali ikiwemo vivuko.
Naye, Diwani wa Kibamba, Otaigo Mwita amesema kazi iliyo mbele yake ni utatuzi wa changamoto za majina ya barabara pamoja na kuwakwamua wanakibamba kiuchumi.
“Changamoto kubwa ni kuunganisha barabara za ndani pamoja na vivuko, maji safi na salama, zahanati vyote hivi tutaenda kufanyia kazi,” ameeleza.
Awali, Mkurugenzi wa manispaa hiyo, Aron Kagurumjuli ambaye ndiye Katibu wa kikao hicho, amesema kura zilizopigwa ni ndiyo au hapana kwa kuwa hakukuwa na mgombea kutoka chama kingine.
