Dar es Salaam. Mwanaharakati maarufu kwenye mitandao ya kijamii ya X na Instagram anayeishi Marekani, Mange Kimambi, amefunguliwa mashtaka ya uhujumu uchumi nchini Tanzania.
Katika kesi hiyo, anakabiliwa na shtaka moja la utakatishaji fedha haramu, kiasi cha Sh138.5 milioni.
Kesi imepangwa kutajwa Desemba 4, 2025, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Hassan Makube wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam. Shauri hilo lilifunguliwa na upande wa Jamhuri Agosti 28, 2025.
Mange kupitia mitandao hiyo ya kijamii, leo asubuhi ya Desemba 2, 2025 ameonekana kupitia video iliyosambaa akithibitisha kupewa taarifa kuhusu kufunguliwa kwa kesi hiyo, akisema Serikali ya Tanzania imedhamiria kumrejesha nchini.
Katika kesi ya jinai namba 000021172 ya 2025, kosa analodaiwa kutenda linaangukia kifungu 12(1)(d) na 13(a) cha Sheria ya Utakatishaji Fedha sura 423 ya 2019, ikisomwa pamoja na Sheria ya Uhujumu Uchumi.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Jamhuri inadai kati ya Machi 1 na Machi 31, 2022, kwenye maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, alijipatia Sh138.5 milioni akifahamu fedha hizo ni zao la uhalifu.
Katika hati hiyo, inadaiwa Mange alijipatia fedha hizo kwa kufanya kazi ya uandishi wa habari bila kuwa na ithibati, pia kudai fedha hizo kwa vitisho.
Sheria ya kurejeshwa kwa mtuhumiwa (Extradition Act Chapter 368) ya mwaka 2019, kosa la utakatishaji wa fedha ni miongoni mwa makosa ambayo yanaipa nguvu Tanzania kuomba kurejeshwa nchini mtuhumiwa wa kosa la jinai.
