Dar es Salaam. Wakati kukiwa na maswali tata kuhusu upotevu na uharibifu wa mali katika Kanisa la Ufufuo na Uzima linaloongozwa na Askofu Josephat Gwajima, Jeshi la Polisi limesema limeanza kufuatilia malalamiko hayo.
Kanisa hilo lilifunguliwa Novemba 24, 2025 kwa agizo la Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba, akielekeza lipewe miezi sita ya uangalizi kuhusu kuzingatia miiko, masharti na sheria za uendeshwaji wake.
Agizo hilo la Serikali, limekuja zikiwa zimepita siku 175 tangu ilipotangaza kufuta usajili wa kanisa hilo kwa kile ilichoeleza limekiuka masharti ya usajili.
Hatua hiyo ya Serikali ilifuata siku chache baada ya Askofu Gwajima kuzungumza na vyombo vya habari akipinga masuala ya utekaji wa watu uliokuwa ukifanyika nchini huku akiwataka viongozi serikalini kukemea jambo hilo.
Baada ya tamko hilo, Wizara ya Mambo ya Ndani ilitangaza kulifungia kanisa hilo kwa madai ya kukiuka masharti ya leseni yake, hivyo Jeshi la Polisi likazungushia utepe kanisa hilo na waumini kuzuiwa kufanya ibada, jambo lililosababisha mvuto baina yao na Polisi waliokuwa wakililinda.
Baada ya kanisa kufunguliwa, Mchungaji kiongozi na mkuu wa utawala na fedha wa makanisa hayo nchini, Askofu Baraka Tegge aliwaeleza waumini kuhusu uharibifu wa mali za kanisa uliofanyika katika kipindi ambacho lilikuwa chini ya Polisi.
Alisema mali zenye thamani ya zaidi ya Sh2.7 bilioni zimeharibiwa na kuibiwa ikiwemo fedha taslimu Sh420 milioni zilizokuwa zimewekwa kwenye makabati maalumu.
Akizungumzia malalamiko ya upotevu wa mali za kanisa, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amelieleza Mwananchi kwamba wameanza kufuatilia malalamiko hayo.
“Ni kanuni ya kiutendaji, malalamiko yoyote yanayohusu Polisi, yakifikishwa kwenye mamlaka yoyote ya umma, uchunguzi hufanywa dhidi ya jambo linalosemwa. Tumekwishaanza kufuatilia malalamiko hayo,” amesema.
Wakati Jeshi la Polisi likieleza hayo, kumekuwa na maswali kuhusiana na uharibifu na wizi wa mali za kanisa hilo katika kipindi ambacho lilikuwa likilindwa na Polisi.
Swali linalogonga vichwa ni je, nani amehusika na uharibifu au wizi huo wakati wa ulinzi mkali wa Jeshi la Polisi?
Wakati kukiwa na sintofahamu hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando alilitaka kanisa hilo kufanya tathmini ya hasara iliyopatikana kwa kuwa hakukuwa na makabidhiano yoyote, kisha wampelekee taarifa, baada ya hapo atatoa maelekezo.
Swali ni je, kanisa hilo likiwasilisha tathmini yake juu ya mali zilizoharibiwa na kuibiwa, Serikali itafanyaje kuhakikisha zinarejeshwa ili huduma katika kanisa hilo ziendelee kama kawaida?
Alipotafutwa na Mwananchi kujua kama amepokea ripoti ya tathmini kutoka katika kanisa hilo na hatua zinazofuata, Msando amesema bado hajapokea taarifa hiyo kutoka kwa uongozi wa kanisa kama alivyoelekeza.
“Sijapokea taarifa yao kuhusu uharibifu unaodaiwa kufanyika,” amesema Msando katika mawasiliano yake na mwandishi wa gazeti hili.
Swali jingine katika sintofahamu hiyo ni uhalisia wa thamani ya Sh2.7 bilioni na tathmini imefanyika lini tangu DC Msando alipoelekeza ifanyike?
Deogratus Masawe, mkazi wa Temeke amesema ni vigumu kuthibitisha kama ni kweli kiwango cha mali kilichotajwa na uongozi wa kanisa ni halisia, lakini uharibifu na wizi lazima vimetokea kwa kuwa vingine vinaonekana kwa macho.
“Mchungaji wa kanisa amesema uharibifu huo umefikia kiasi cha Sh2.7 bilioni, ingawa jambo hili linaonyesha ukubwa wa hasara unaodaiwa, thamani hiyo bado haiwezi kuthibitishwa bila uchunguzi wa mali.
“Madai haya yanaweza kuwa makadirio au tathmini na kwa hivyo yanahitaji uthibitisho wa kina kutoka kwa mamlaka zisizo na upande,” amesema Masawe.
Mwanazuoni huyo amesema kukosekana kwa ripoti huru na ukaguzi wa mali kunasababisha changamoto katika kuthibitisha kiwango cha uharibifu.
Masawe amesema mali za kanisa zinaweza kuchanganywa na mali za watu binafsi, na baadhi ya mali zilizoharibiwa au kupotea zinaweza kuwa matokeo ya usimamizi duni wa ndani, badala ya uharibifu wa moja kwa moja kutokana na kufungwa kwa kanisa.
“Ingawa kanisa linaendelea kudai hasara, Serikali na polisi wanapaswa kuzingatia uwajibikaji wao ikiwa mali ilipotea au kuharibiwa wakati limefungwa, kuna jukumu la kisheria la kurudisha mali au kutoa fidia,” amesema.
Vilevile, swali la msingi kujua ni kwamba nani hasa alikabidhiwa mali zote za kanisa wakati kilipokuwa chini ya ulinzi wa Polisi na je, utunzaji wake ulikuwaje?
