DILI limetiki. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya mabosi wa Singida Black Stars (zamani Ihefu) Uongozi wa Ihefu, umemalizana na kipa Metacha Mnata aliyekuwa Yanga na muda wowote kuanzia sasa inatarajia kumtambulisha rasmi.
Kipa huyo wa zamani wa Azam, Mbao na Singida Big Stars, alikuwa sehemu ya kikosi cha Yanga kilichotetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho kwa misimu miwili mfululizo, lakini tayari uongozi ulishaonyesha kutokuwa na mpango wa kumuongeza mkataba mpya kwa ajili ya ajili ya msimu ujao.
Kutokana na kufahamika Metacha kutokuwa kwenye mipango hiyo ya Yanga, fasta Singida BS iliyomnasa kocha wa zamani wa Simba na AFC Leopards, Patrick Aussems ikaamua kumalizana naye ili awepo katika kikosi cha timu hiyo kwa msimu ujao.
Kabla ya Singida BS kumalizana naye, kipa huyo anayeitumikia pia timu ya taifa, Taifa Stars alikuwa katika rada za mabosi wa klabu ya Azam FC iliyompelekea ofa ikimtaka asaini mkataba wa miaka mitatu, lakini dili lilikwama kutokana na dau nono alilowekewa na Singida iliyomsainisha mkataba wa muda mfupi.
Kiongozi mmoja wa Singida BS (jina tunalo), amesema haikuwa rahisi kufanikisha dili la Metacha, kwani kuna timu nyingi zilihitaji huduma ya kipa huyo mzoefu.
“Metacha ni kipa mzuri, tumeshinda vita ya kumpata dhidi ya timu ambazo,tunajua zilikuwa zinahitaji huduma yake, muda wowote atatambuliahwa,” amesema kiongozi huyo.
Nje na Metacha, imeelezwa kuwa, Singida BS ipo kwenye mazungumzo pia ya kumnasa kipa wa zamani wa Yanga, Simba na Singida Fountain Gate, Beno Kakolanya.
Kakolanya aliidakia Singida FG katika Ligi Kuu msimu uliomalizika hivi karibuni kabla ya kutibuana baada ya kususa mechi za mwishowe baada ya kutuhumiwa na viongozi wa timu hiyo kufanya kusudi kuikimbia mechi dhidi ya Yanga.